HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatatu, 22 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Kaduguda arejeshwa Simba SC


na Makuburi Ally


WANACHAMA wa klabu ya Simba, jana walimrejesha katika uongozi wa klabu hiyo, Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda au Kagabo’, aliyekuwa amesimamishwa tangu Juni 8 kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Katika Mkutano huo Mkuu uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Al-Muntazir jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama wapatao 449, waliomsamehe Kaduguda na kumrejesha.

Mkutano huo uliokuwa na ajenda kuu mbili ambazo ni mapato na matumizi na hatima ya Kaduguda aliyefungiwa kwa kile kilichodaiwa utovu wa nidhamu.

Baada ya kufungua mkutano, Dalali alimkaribisha Mweka Hazina wa Simba, Idd Senkondo, aliyesoma ripoti ya mapato na matumizi kuanzia Desemba 20, 2006 hadi Julai mwaka huu.

Senkondo alisoma taarifa hiyo, ya ripoti kwa utulivu, lakini kwa bahati mbaya haikuwapa mwanya wa kuijadili ripoti hiyo, kutokana na kukosa wasaa wa kuitafakari kabla ya kuipitisha.

Senkondo alisema mapato kwa muda wa miezi 20, ni sh 943,236,220.75 wakati matumizi ni sh 940,931,000.31 huku wakiwa na akiba ya sh 10, 572,890.20, zilizoko Benki.

Baada ya Senkondo kuwasilisha taarifa hiyo na wanachama kuipitisha, ulifika muda wa Dalali kuwasilisha tuhuma za Kaduguda kwa wanachama kabla ya dakika chache umeme ukazimika ukumbini hapo hali iliyosababisha Dalali kuwasilisha tuhuma na Kaduguda kujitetea pasi na kipaza sauti.

Akiwasilisha tuhuma hizo, Dalali ‘Field Marshal’ alisema Oktoba 7, na Novemba 11 mwaka jana Kaduguda alipigana na mkewe.

Wakati tuhuma zake nyingine alizifanya Aprili 10, mwaka huu alipomkaba dereva wa basi wakati walipokuwa wakitokea mkoani Kagera, tukio ambalo lilitaka kusababisha ajali kwa wachezaji. Dalali, aliwaeleza wanachama kuwa, Aprili 15 alipigana na mkewe baada ya mechi kati ya Simba na Toto Africa, Uwanja wa Taifa.

Dalali alisema Juni 8, 2006, Kaduguda alimtukana matusi ya nguoni mfadhili wa Simba, hali iliyowafanya wajumbe wa Kamati ya Utendaji kumsimamisha uongozi baada ya kukataa kuitikia wito wa barua mbili za wito wa kujieleza.

Mara baada ya kuwasilisha tuhuma hizo, wanachama wa klabu hiyo walizusha mzozo uliodumu kwa dakika sita kama Kaduguda apewe nafasi ya kujieleza kuhusiana na tuhuma hizo au la, lakini hatimaye ikakubalika kuwa apewe nafasi hiyo.

“Simba Oyee, Simba Oyee,”, ndivyo alivyoanza utetezi wake Kaduguda ambaye alizikana tuhuma zote, akisema kuwa zimepikwa ili wamchafue, hali ambayo haikumtisha Kaduguda.

Baada ya kusema kuwa yeye hana hofu wala wasiwasi wa kuondoka Simba, lakini ukweli ni kuwa anaondoka kutokana na kutetea masilahi ya Simba.

“Ndugu zangu nawaombeni tusikilizane. Kosa langu kwa Simba ni kuhoji mambo ambayo yana masilahi kwa Simba, hilo ndilo kosa langu hadi nimesimamishwa. Wacha niwaambie ukweli halafu muamue ninyi,” alisema Kaduguda.

Kaduguda alielezea kikao cha Mei 12, mwaka jana kilihusu tathmini ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita na Simba ikakosa nafasi ya kuwakilisha katika michuano ya kimataifa.

Kaduguda alisema katika mkutano huo uliofanyika Reagency Msasani jijini Dar es Salaam ambako alihoji kuuzwa kwa wachezaji watatu Edwin Mukenya, George Owino na Moses Odhiambo.

Kaduguda alisema kikao hicho kilikuwa ni cha Kamati ya Utendaji na kundi la marafiki wa Simba ‘Friends of Simba’ ambako alitaka apatiwe maelezo akiwa ni Katibu Mkuu.

Kuhusu mchezaji Edwin Mukenya aliyehamishwa kutoka Yanga kwenda Simba kwa ada ya dola 10,000 za Marekani lakini hakucheza hata mechi moja kati ya 42 ambazo Simba ilipaswa kucheza msimu mzima na hakuwepo Dar es Salaam bila taarifa ya Katibu Mkuu.

Kaduguda alisema suala hilo lilikosa jibu, ambako mmoja wa wafadhili alimuuliza kiasi ambacho Kaduguda alitoa wakati mchezaji huyo anatoka Yanga kwenda Simba.

Kaduguda alijibu kwa kuwa yeye ni Katibu Mkuu ni mchango tosha kuhoji kutokana na dhamana aliyopewa na wanachama ili afahamu jambo hilo.

Alisema Mukenya kama angesajiliwa kwa ajili ya familia ya mfadhili huyo, yeye asingehoji kwa sababu hana mamlaka ya kuhoji masuala ya familia, lakini kwa kuwa amesajiliwa na Simba ana haki ya kuhoji.

Kaduguda pia alihoji suala la mchezaji George Owino aliyecheza raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom lakini hakucheza hata mchezo mmoja wa raundi ya pili ambako alitaka kujua alipo mchezaji huyo na suala hilo likakosa jibu.

Aidha alisema swali hilo lilikosa jibu kutoka pande zote mbili uongozi na Friends of Simba lakini baadaye cha kushangaza Owino anaonekana anacheza Yanga kila mtu anashuhudia, kutokana na hilo ni nani alisaini fomu ya uhamisho wakati Katibu Mkuu hajasaini.

Pia alielezea kuhusu suala la mchezaji Odhiambo aliyeuzwa timu ya APR ya Rwanda kwa dola za Marekani 5,000 za Marekani, kiasi ambacho yeye alikipinga kutokana na thamani ya pesa kuwa ndogo ukilinganisha na mchezaji huyo.

“Nilimpigia simu Dalali ili twende ili tukaonane na viongozi wa APR ili tujadiliane ili waongeze dau ambalo lingesaidia kununuliwa wachezaji wengine wawili,” alisema.

Kaduguda alisema walimpigia Evans Aveva akawaambia wakutane ofisini kwake lakini walipokwenda hawakumkuta na kukaa zaidi ya saa nne wakiwasubiri APR na Avave bila ya mafanikio.

“Nilimwambia Mwenyekiti wangu tuondoke na turudi kesho asubuhi lakini cha kushangaza asubuhi alipofika Makao Makuu akaambiwa Mwenyekiti ameshasaini fomu za kumuuza kwa dola 5,000 za Marekani tangu saa sita usiku,” alisema.

Kaduguda alisema alipomuuliza Dalali, alimwambia wangechelewa kuchukua fedha hizo Friends of Simba wangechukua fedha zote na wasingeambulia kitu.

Alisema kutokana na ukweli kwamba ‘Mungu si Athumani’ viongozi pamoja na timu ya APR ilikuja nchini katika mashindano ya Kagame ambako alikutana na uongozi wa APR na kuelezwa kuwa mchezaji huyo alinunuliwa kwa dola za Marekani 25,000 na wala si 5,000 kama alivyodai Dalali.

Baada ya kuwasilisha utetezi wake, Dalali alitoa nafasi kwa wanachama kutoa maamuzi ambako zilipigwa kura za wazi, kura chache zilimkataa na nyingi zilitaka arejeshwe kundini.

Kutokana na maamuzi hayo ya wanachama Dalali alitangaza kumaliza tofauti zao na kwamba wamempokea na watafanya naye kazi bega kwa bega.

“Kaduguda njoo hapa nipe mkono,” Kaduguda aliitikia wito huo na kwenda meza kuu na kumpa mkono kisha wakakumbatiana na baada ya hapo akuwakumbatia viongozi wengine.

“Mimi uongozi wangu si wa kidikteta, kwani unaona nimetoa tuhuma na nimetoa nafasi ya kujieleza na kuwapa nafasi wanachama muamue, kwani sisi si kama zilivyo baadhi ya klabu,” alisema Dalali.

Kabla ya mkutano huo kuanza, Kaduguda alipofika ukumbini hapo saa nne asubuhi alimsalimia Dalali lakini Dalali alikataa huku akisema: “Unanisalimia nini wakati umenitangazia kuwa mimi mwizi, halafu unanisalimia.”


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)