BONDIA nguli nchini, Rashid Matumla ‘Snake Boy’ amefikia uamuzi wa kupromoti watoto kwa kutumia mikanda yake kadhaa aliyowahi kuinyakua.
Akizungumza na Tanzania Daima Matumla alisema ameamua kutumia mikanda yake hiyo ‘kupromoti’ watoto wake pamoja na watoto wengine wenye umri chini ya miaka 17 ili kuibua vipaji vya watoto katika mchezo huo.
“Nimeamua kupromoti watoto baada ya kuona watoto ni msingi mzuri na kutaka kuwapa moyo wa kuupenda mchezo huo kwa kuwa sasa umeanza kuporomoka kutokana misingi mibovu kwa watoto ambako wengi huanzia ukubwani,” alisema Matumla.
Matumla alisema hata yeye alianzia mchezo huo akiwa mdogo akiwa chini ya kocha Habib Kinyogoli hadi kufikia alipo sasa.
Alisema mpambano ambao atawashindanisha watoto ataanzia kwa watoto wake aliowataja kwa jina la Daudi, Mussa na Afrika Matumla, lakini alisisitiza na kuwataka watoto wengine kutoka katika sehemu mbalimbali kujiunga na mchezo huo.
Familia ya Matumla imekuwa na mwendelezo mzuri wa kuzalisha mabondia kutoka katika familia yake na hata kwa watoto ambao wanawazunguka wakiwa kwenye makazi yao Keko Magurumbasi.