WIKI zilizopita katika makala hii tulieleza kuwa kazi ni msingi wa maendeleo ya mtu yeyote mwenye uwezo wa kimwili na kiakili, kutegemea na mahitaji ya kazi yake.
Pamoja na kusema kuwa katika kazi kuna ukomo usio halali kisheria na ulio halali. Leo tunaendelea na baadhi ya mambo yanayohusu kufanyika kazini kisheria na yasiyohusu kufanyika.
Migomo kazini
Katika kipindi hiki, migomo imekuwa suluhisho la mwisho kwa wafanyakazi pale wanapoona mambo hayaendi sawa upande wao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria hizi, mgomo ni haki ya kila mfanyakazi, lakini vilevile taratibu lazima zifuatwe.
Kwanza, mgogoro uwe wa masilahi, uwe umekwisha kupelekwa Tume ya Usuluhishi na Maamuzi, ikiwa pamoja na kujaza fom CMA F.1.
Pia uwe haujatatuliwa mpaka kufikia mwisho wa kipindi cha usuluhishi kwa mujibu wa sheria. Mgomo uwe umeitishwa na chama cha wafanyakazi baada ya kupiga kura kwa mujibu wa katiba ya chama na uonekane kuwa watu wengi wanaunga mkono mgomo na mwisho wafanyakazi wawe wametoa kwa mwajiri notisi ya saa 48 ya kusudio la kugoma.
Pamoja na taratibu hizo zote, lakini wafanyakazi wa sekta za huduma muhimu kama umeme, afya, uzoaji taka n.k hawaruhusiwi kushiriki katika mgomo mpaka masharti maalumu yazingatiwe.
Kufungiwa nje
Wakati wafanyakazi wanaruhusiwa kugoma, waajiri kwa upande wao wanaruhusiwa kuwafungia nje wafanyakazi na kuwe kihalali kisheria.
Lakini katika migomo yote hiyo ni lazima iendane na sheria nilizozitaja hapo juu ingawa yapo mambo yasiyokubalika kufanyika wakati wa mgomo au kufungiwa nje.
Haya ni pamoja na kuweka vizuizi kwa lengo la kushabikia mgomo au kuzuia mgomo halali, kutumia nguvu kazi mbadala, kuwafungia waajiri ndani ya maeneo yao ya kazi au kuwazuia waajiri wasiingie maeneo ya kazi.
Wafanyakazi wana haki ya kuanzisha, kujiunga na kuunda vyama vyao. Wafanyakazi au waajiri wanaotaka chama kisajiriwe wanatakiwa na msajiri wa vyama hivyo ndani ya miezi sita tangu kuundwa kwake kwani kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Zaidi ya Tume ya Usuluhishi na Maamuzi, pia kuna taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya kazi. Hizi ni pamoja na Taasisi ya Huduma Muhimu, Bodi ya Mishahara na Idara ya Usimamizi wa Kazi na Huduma za Ukaguzi.
Kwa ujumla, sheria hizi zimezungumzia mambo muhimu sana kwa wafanyakazi. Kwa kiwango kikubwa imeelezea masuala ya mikataba ya ajira, aina zake, aina za wafanyakazi wanaonufaika na sheria hizi na wale ambao nao hawajauhusishwa na sheria hizi.
Hata hivyo, kuna upungufu kadhaa ambao sheria hizi zinao. Kwa mfano, sheria hii imerudisha nadharia iliyoondolewa na sheria ilizozifuta.
Hii ni ile nadharia ambayo imetengenezwa na sheria za Mahakama za Uingereza (maarufu kama Common Law), ambayo mwajiri alikuwa na uwezo wa kusitisha ajira ya mfanyakazi wake kwa sababu yoyote ile inayoeleweka kwake.
Nadharia hii hakika ilifutwa na sheria ya Ulinzi wa Ajira ( Security of Employment Act), lakini ndani ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, ambayo ndani ya kifungu 36 (a) (i) imeikubali kama njia mojawapo ya kusitisha ajira.
Hili ni tatizo, kwani kwa jinsi nadharia hii ilivyo, uhakika wa ulinzi wa ajira za wafanyakazi wengi zitakuwa mashakani.
Vilevile, kuhusu suala la mikataba ya ajira, sheria hii imesahau baadhi ya wafanyakazi. Kwa mfano, wafanyakazi wa majumbani wanaofanya kazi ndani ya nchi hawajaguswa kabisa na sheria hii.
Badala yake, imeweka mkazo zaidi kwa wafanyakazi wa majumbani wanaofanya kazi nje ya nchi. Kwa kweli hili ni tatizo, kwani wafanyakazi wa majumbani wanaofanya kazi ndani ya nchi wanastahili kulindwa na sheria kama walivyo wafanyakazi wengine wote hapa nchini.
Hitimisho
Sheria mpya za kazi ndio mustakabali kwa haki za wafanyakazi na maendeleo ya familia zao na nchi nzima kwa ujumla. Itakuwa ni busara kama vyombo husika vitayachukulia kwa uzito stahili.
Upungufu unaotolewa na wadau mbalimbali ili mwisho wa siku wafanyakazi nchini wapate kile kinachoitwa maisha bora kwa kila Mtanzania.