ZAIDI ya wanafunzi 600 wa kike mkoani Kagera wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata ujauzito kwa kipindi cha mwaka 2009/2010.
Ofisa Maendeleo wa Mkoa wa Kagera, Charles Mafimbo, alisema hayo juzi alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Karagwe katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Rugu, Kata ya Rugu, wilayani Karagwe.
Alisema wanafunzi hao walipata ujauzito huo mwaka jana, hivyo kuchangia kushuka kwa kiwango cha elimu mkoani hapa.
Mafimbo alisema tatizo la mimba kwa wanafunzi ni mwamko duni wa wazazi katika suala la elimu pamoja na walimu wengi kujihusisha na miradi yao binafsi wakati wa kazi na kutokuwa na sifa za kufundisha.
Aidha, alieleza kusikitishwa kwake na taarifa za matokeo ya kidato cha pili mwaka huu ambayo yamesababisha Wilaya ya Karagwe kuwa wilaya ya mwisho kimkoa na kitaifa.