HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
alhamis, 11 machi 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Simba yajichimbia Zenji

•  Uli, Okwi waachwa Dar

na Dina Ismail

 

KIKOSI cha Simba jana kilikwenda Zanzibar kusaka makali kwa ajili ya mechi ya Jumapili dhidi ya Azam FC huku ikiwaacha jijini Dar es Salaam nyota wake, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Okwi na Anthony Matangalu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana, Meneja wa Simba, Innocent Njovu, alisema Okwi na Matangalu, wameachwa kutokana na kusumbuliwa na homa ya matumbo.

Kuhusu Mwakingwe, Njovu alisema amebaki kutokana na hali yake kutokuwa fiti, kwani ndiyo kwanza ametoka katika dozi ya malaria, hivyo anatarajiwa kuungana na wenzake leo.

Njovu alisema Simba wamepiga kambi eneo la Mbweni, nje kidogo ya Zanzibar, kujiandaa kwa mechi ya Jumapili na michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Njovu alisema ukiondoa nyota hao, wengine wapo katika hali nzuri na jana jioni walitarajiwa kuanza mazoezi katika viwanja vya Chuo cha Polisi.

Alisema lengo la kambi hiyo, si kushinda mechi ya Jumapili na kutangaza ubingwa mikononi mwa Azam FC tu, bali kusaka makali ya kuiangamiza Lengthens ya Zimbabwe iliyotinga hatua ya kwanza kwa kuing’oa AS Adema ya Madagascar.

Kuhusu mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Yanga na Mtibwa Sugar, Njovu alisema hesabu zao ni kushinda zote ili kuweka rekodi ya kutofungwa.

Alisema kutokana na maandalizi mazuri na mipango bora kwa ujumla, wataendelea kushinda na kuweka rekodi ya kutofungwa katika ligi hiyo iliyoanza Agosti 23 na itakayofikia tamati Machi 27.

Mechi dhidi ya Azam FC imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, kwani kama Simba itashinda, watakuwa mabingwa kwa kuwa watafikisha pointi 56 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote.



juu