HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 15 mei 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti

JK atetea takrima

•  Apuuza uamuzi wa Mahakama Kuu

na Irene Mark

 

RAIS Jakaya Kikwete amekiri kwamba serikali yake haiwezi kukomesha takrima ambayo baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakiitafsiri kuwa ni rushwa ya uchaguzi iliyopewa jina zuri.

Rais Kikwete anatoa kauli hiyo baada ya miaka minne tangu Mahakama Kuu ilipofuta vifungu vya sheria vilivyokuwa vinatetea sheria ya takrima.

Rais alitetea takrima jana mbele ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini, muda mfupi kabla ya kufunga mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Alisema ni vigumu kudhibiti takrima.

Serikali iliwaita viongozi hao kujadili masuala ya uchaguzi na sheria zake, katika hali iliyotafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini kama njia ya serikali kujipatanisha na viongozi kwa maslahi mapana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete alisisitiza, “Suala la takrima ndugu zangu… mmh, hili nalo gumu (kicheko kidogo), gumu kwa maana ya… mfano pale Kilimanjaro, Askofu Shao, anajua kwamba ili uzungumze na wazee lazima wawe wanakunywa kitochi (mbege).

“…(kicheko tena) Kilimanjaro pale kuna mazingira maalum ndiyo maana wana CHADEMA wanafanya hivyo, wana CCM wanafanya hivyo hivyo, hata wana TLP nao wanafanya!” alisisitiza Rais Kikwete.

Kauli ya Rais Kikwete inakinzana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliotolewa Aprili 24, 2006, kufuta vifungu vya 119(2) na 119(3) vya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000 vilivyokuwa vinaruhusu matumizi ya takrima katika uchaguzi.

Uamuzi huo ulisomwa na Jaji Natalia Kimaro aliyekuwa mwenyekiti wa jopo la majaji watatu: Thomas Mihayo na Salum Massati, waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo ya Kikatiba.

Jaji Kimaro alisema kuwa mahakama ilifikia uamuzi huo kwa kuwa vifungu hivyo vinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.

Kadhalika, mahakama hiyo ilikifuta pia kifungu cha 130(a-d) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 inayoipa Mahakama Kuu mamlaka ya kutamka kuwa takrima ilitolewa ‘kwa nia njema’ na hivyo mtoaji kutokuwa na hatia.

Jaji Kimaro alisema mahakama iliridhika na maelezo ya walalamikaji ambao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Shirika la Kitaifa la Msaada wa Sheria (nola) na Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) kuwa vifungu hivyo vinapingana na Katiba kwa kuwa vinawanyima baadhi wa raia haki ya kushiriki kiusawa katika uchaguzi kama ilivyoelezwa na Katiba.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, jopo liliridhika kuwa vifungu hivyo vilikuwa vya kibaguzi na kwamba vilikuwa vinaathiri uhuru wa wapiga kura ambao baadhi yao ni maskini na hawana uelewa wa haki zao za kupiga kura.

Jaji Kimaro alisema Bunge lilivunja ibara ya 13(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokataza kutungwa kwa sheria yoyote ya kibaguzi.

Alisema vifungu hivyo vilikuwa vya hatari kwa maendeleo ya taifa na vinaweza kulipeleka taifa kubaya na hivyo vinapaswa kufutwa mara moja ili ‘watu wajue kuwa viongozi bora hawapimwi kwa uwezo wao wa kifedha.’

Awali akitoa uamuzi kuhusu pingamizi zilizowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali akidai kuwa LHRC, nola na LEAT hawana uwezo wa kisheria kufungua kesi hiyo, alisema pingamizi hilo limetupwa kwa kuwa taasisi zina haki ya kufungua kesi ya katiba kama alivyo mtu binafsi.

Alisema kuwa pingamizi jingine lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa takrima haiwezi kulinganishwa na rushwa kwa kuwa haijielezi kinaga ubaga kuwa ni rushwa, alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikaji, Alex Mgongolwa na Issa Maige, kuwa kilicho muhimu katika suala hilo si maelezo ya kinaga ubaga bali matokeo ya kitu chenyewe.

Akisoma uamuzi wa nyongeza kukubaliana na uamuzi uliosomwa na Jaji Kimaro, Jaji Thomas Mihayo alisema anakubaliana na uamuzi huo kwa kuwa kwa mujibu wa desturi za Kiafrika, mwenyeji huwa ndiye mwenye wajibu wa kuwakirimu wageni na sio mgeni kukirimu wenyeji na kuwa inapotokea mgeni kukirimu mwenyeji ni suala la kibiashara.

Naye Jaji Massati alisema kwa kuwa Katiba ya nchi katika ibara za 13(1), 13(2) na 21 inatoa uhuru kwa raia kushiriki katika shuhguli za kisiasa vifungu 119(2) na 119(3) vya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 vinapingana na Katiba moja kwa moja na anaridhia vifutwe.

Alisema pia kuwa hakuna haja hata ya kufanya mjadala kuhusu uhalali wa takrima kwa kuwa takrima inapingana na Katiba ya nchi.

Katika hotuba yake jana, Rais alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha viongozi wa dini kuacha kuhubiri siasa makanisani au misikitini kwa maelezo kwamba watazua mfarakano kati ya waumini wao na badala yake waongeze hamasa kwa kueleza sifa za kiongozi mzuri bila kulionea haya jambo hilo.

“Kwangu viongozi wa dini sawa na mawakili. Nawaomba muwahimize waumini wenu kuwachagua viongozi wazuri wala msilionee haya kulisema. Nawaomba msihubiri siasa kwenye madhabahu wala mimbari; mtapata matatizo,” alisema Rais Kikwete aliyebainisha kutoridhishwa na mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma.

Alisema, haridhishwi na suala la mporomoko wa maadili kwa viongozi wa serikali na taifa kwa ujumla ndiyo maana wapo watendaji kutoka taasisi mbalimbali huku akisisitiza uchaguzi huru na haki kisha kuwataka wananchi wote kurekebisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Aidha, alikubaliana na mapendekezo ya viongozi hao wa dini kuwa serikali yake itaweka mkakati wa kukutana nao mara mbili kwa mwaka huku akifafanua kwamba utaratibu huo utafanyika kwa awamu akimaanisha Wakristo peke yao na Waislam peke yao kisha mkutano wa mwisho utakuwa wa wote.

Kadhalika, rais aliwataka Watanzania kuheshimu tofauti za dini au kabila zilizopo kati yao na kusema zisitumike kuleta tofauti itakayovuruga amani ya taifa iliyojengwa kwa zaidi ya miaka 40 huku akisisitiza kwamba sheria za nchi zinatoa uhuru wa kuabudu na kuzuia mmoja kukejeli dini ya mwingine.

“Tusigeuze tofauti zetu kuwa chanzo cha uhasama. Tuzidishe ushirikiano… hakuna mwenye uwezo wa kubadili tofauti hivyo lazima tutengeneze utaratibu wa kuishi pamoja,” alisema Rais na kuomba dua za viongozi hao ili uchaguzi mkuu uwe huru na haki.

Alisema, serikali inaweza kufanya au kutoa kauli ikaleta mtafaruku kutokana na tafsiri za watu lakini yote hiyo ni ubinadam, hivyo aliwaomba viongozi hao kuwa wavumilivu kwenye vipindi vigumu na kuutambua mchango wa dini katika sekta ya afya, elimu na huduma za maji.

Kuhusu uchache wa wawakilishi wa dini ya Kiislam, Rais alisema huo ni mkutano wa mwanzo na kuahidi kuiendeleza mikutano hiyo.

“Wenzenu wengi wamenitumia ujumbe kwamba wamebaguliwa, nimepokea sms nyingi wanalalamika lakini niliwaeleza kwamba huu ni mwanzo. Simu yangu ile ipo wazi muda wote watu wananitumia sms nawapigia wengine wananipigia kunieleza matatizo yao mbalimbali nazungumza nao nanyi nawaomba msisite kufanya hivyo.”

Rais Kikwete alilazimika kusema hayo kutokana na malalamiko ya viongozi wa Kiislam kutoka Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), kuhusu kubaguliwa kwa viongozi wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislam ambao hawakupata mwaliko hali iliyofanya Waislam kuwakilishwa na masheikh 15 tofauti na uwakilishi wa zaidi ya viongozi 40 kutoka dini ya Kikristo.

Hata hivyo, katika siku ya kwanza ya mkutano huo (juzi) Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo aliwataka radhi Waislam wote na kukubali kuongeza idadi yao.

Licha ya kukubaliwa huko, masheikh kutoka Jumuiya ya Taasisi za Kiislam waligoma kuhudhuria mkutano huo kwa maelezo kwamba hawako tayari kwa kuwa wameshtukizwa.

Akizungumzia hilo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema masheikh kutoka taasisi nyingine chini ya jumuiya hiyo hawakuridhishwa na aina ya mwaliko hali iliyowalazimu kuwachukua masheikh wengine 15 kutoka Bakwata na kufanya idadi yao kuzidi 30.

“Jana (juzi) baada ya kuwaleza kwamba nao wanatakiwa walisema hawawezi kuja… walisema wao sio sawa na mshumaa unaotumika wakati hahuna umeme na sisi tukaona kweli lipo tatizo, kifupi walitaka mwaliko kama uliopelekwa Bakwata. Sasa katika kuokoa jahazi tumewaleta wenzetu wa Bakwata,” alisema Sheikh Alhad.

Mkutano kati ya viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini na serikali ulilenga kutoa elimu ya uraia hususan kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu iliuandaa kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (NEC), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Tofauti na siku ya kwanza, jana viongozi wa serikali waliokuwepo ni Mkuu wa Mkoa, William Lukuvi, Waziri wa Tamisemi, Celina Kombani, makatibu wakuu wote kutoka wizara zinazohudumu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.



juu