KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimelaani kufumbiwa macho kwa vitendo vya rushwa vinavyoripotiwa kufanywa na baadhi ya wagombea katika harakati za kujinadi kwa wanachama wao pamoja na sheria hiyo kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete Machi 17, mwaka huu.
Hayo yalielezwa jana kwa waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na Mtafiti wa LHRC, Onesmo Olengurumwa, wakati akitoa ripoti kuhusu hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.
“Sheria hii haifanyi kazi, rushwa katika uchaguzi imeshika hatamu, kwani bado pesa ni sehemu ya kumfanya mtu awe kiongozi, kila siku inaripotiwa kuwepo kwa watu kutoa pesa ili kuchaguliwa na hakuna utekelezaji wowote unaofanywa,” alisema Olengurumwa.
Alisema katika kuendeleza suala hilo baadhi wa watu wameshabuni mbinu kwa kutumia njia ya utumaji pesa ya M-Pesa kutuma pesa ili wachaguliwe.
Kuhusu uandikishaji katika daftari la wapiga kura, alisema katika zoezi hilo ilibainika kuwa watu wengi walifanya udanganyifu kwa kujiandikisha zaidi ya mara moja na kwa Dar es Salaam peke yake watu zaidi ya 500 walibainika na kituo hicho kinaamini kwamba jambo hilo limetokea pia mikoani.
Alisema Tume ya Uchaguzi nchini na Zanzibar (NEC na ZEC) zilishindwa kufikia malengo katika uandikishaji, mfano kwa Zanzibar pekee watu karibu 100,000 hawakuandikishwa.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu wanafunzi wengi wa vyuo vikuu hawatapiga kura kutokana na muda wa kufungua shule kusogezwa mbele hivyo suala hilo litaathiri upigaji kura kwao, kwani wengi walijiandikisha wakati wakiwa vyuoni.
Kuhusu idadi ya watu waliokufa mikononi mwa vyombo vya dola alisema kwa mwaka huu idadi hiyo imeongezeka kutoka 15 mwaka jana hadi kufikia 25 katika nusu ya mwaka huu (miezi sita).
Kuhusu watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili, alisema matukio hayo kwa sasa yanaongezeka kwa kasi hivi sasa kwa wazazi au walezi kuwafanyia watoto wao vitendo hivyo na kwa Dar es Salaam ripoti hiyo inaonyesha kwamba watoto 150 wamefanyiwa vitendo hivyo.
Alisema ripoti ya shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utafiti (REPOA) inaeleza kwamba asilimia 20 ya watoto wenye umri chini ya miaka 17 wameajiriwa kufanya kazi za hatari ikiwemo migodini, mashambani na wengi wao wanatoka Wilaya ya Kilwa-Lindi, Unguja Kaskazini, Micheweni na Ilemela.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Farancis Kiwanga alisema lengo la utafiti huo ni kutekeleza mkataba wa kimataifa kuhusu haki za binadamu pia kupima walichofanya ili kuipa uelewa jamii kuhusu ukiukwaji huo unavyofanyika.
Kwa mujibu wa Kiwanga, hufanya tafiti hizo kila mwaka kwa kugusa nyanja zote na kwamba wanafurahi kwamba utafiti wao husaidia, kwani wanaporudi kwa mara nyingine katika maeneo ambayo huwa na matatizo hukuta mabadiliko.