KABLA na baada ya kupata uhuru, hayati Mwalimu Julius Nyerere alionekana mwanaharakati mwenye mapenzi na nchi yake na hakuvumilia ukandamizaji wa haki za binadamu.
Nyerere alikuwa kiongozi wa kweli kwani kwa kutumia njia ya amani, aliipatia Tanzania uhuru pasipo umwagaji wa damu.
Tunapoongelea viongozi wababaishaji hatuwezi kumtaja Nyerere, kwani ni kosa kama lile la kuua.
Kuanza kwa vyama vingi mwaka 1992 kulituonyesha mwanzo wa makucha ya viongozi wababaishaji. Kitendo cha kuanzisha vyama vingi licha ya kudaiwa na wengi kuwa ni demokrasia kinatuonyesha tofauti pamoja na itikadi zilizokuwa kwenye vichwa vya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tumekuwa tukishuhudia vyama vikiandaa vipeperushi vingi pamoja na kanga, kofia, na tisheti ili tu kunasa ufahamu wa Watanzania ambao wengi kweli bado hawajapata fursa ya kupanuka kimawazo.
Kuanzisha chama kimoja na kukihama baada ya muda ni jambo tuliloshuhudia likifanywa na hawahawa wanaojiita wanasiasa. Tumeshuhudia kiongozi mkubwa kabisa aliyepata kushika nafasi nyeti katika nchi hii akikihama chama tawala CCM na kuanzisha chama cha upinzani.
Alipoona chama kimechuja akajiunga na chama kingine ili kuendelea kujenga jina na umaarufu. Watanzania msimamo wa wanasiasa wetu uko wapi, ukiacha kujinufaisha wenyewe na mahubiri yao yenye ulaghai? Je, Watanzania tutaendelea kwa kubadili vyama au kwa kuwa na sera zenye utekelezaji zaidi kuliko nadharia?
Watanzania tuwe makini na wanasiasa wetu ambao ndio wanaounda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limeshindwa kutupa hatima ya matatizo kibao ambayo yanagusa maisha ya kila Mtanzania.
Vipi Epa, Richmond na Mgodi wa Kiwira! Watanzania tujue lipi basi juu ya utendaji wa viongozi wetu ambao kwa asili ni wanasiasa?
Tunahitaji kujua matatizo haya kama yamefikia hatima. Au mmeamua kuyazika ili kuwalinda wenzenu au kuogopa kuwa pengine kivuli cha kashfa kinaweza kuwaangukia? Tuelezeni tusiwape wakati mgumu Oktoba mwaka huu.
Madai ya kurekebisha katiba tumeyazoe sasa kutoka kwa viongozi wetu, hasa wale wa upinzani.
Nani ana jukumu la kukubali katiba? Si Bunge? Mimi najua ni Bunge. Je, wanasiasa hawa wameshindwa kutoa mapendekezo bungeni ya kubadili katiba au wanakuja kuyatangaza kwenye vyombo vya habari na hadhara kujipatia umaarufu? Watanzania, tuwaweke wanasiasa wetu pagumu katika uchaguzi mwaka huu.
Kupotosha mambo na kuwachanganya wananchi ni miongoni mwa sifa za wanasiasa wetu. Niliwahi kuhudhuria kikao kimoja cha kampeni na kiongozi mmoja alidiriki kusema fedha zilizokuwa zikilipwa kwa Kampuni ya Richmond ni sawa na kumlipa kila Mtanzania shilingi milioni tatu kwa siku, kitu ambacho si kweli, lakini kimetokana na uongozi mbaya uliojaa matakwa ya kisiasa ya kudhoofisha upande mwingine.
Wanasiasa wetu wamekuwa wakionekana zaidi maeneo yao wakati wa uchaguzi au karibu na kampeni za uchaguzi. Wakati mwingine wanafurahia maisha kivyao chini ya mwamvuli wa kura zetu.
Hawa wanasiasa tumewafanya wafalme wa kweli kutokana na maamuzi yetu, ila hatima yao ipo mikononi mwetu. Wamekuwa wakija na zawadi na vijimisaada ambavyo wamevibariki na kuviita takrima ili kutupoteza akili.
Watanzania yatupasa tuwatake viongozi wetu watujengee miundombinu ya kutuletea maendeleo na si vimisaada vya hongo ambavyo ni kama tone la maji safi katika bahari ya maji machafu.
Hivi ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania ililenga shabaha za kisiasa na kushinda uchaguzi au kubadili kweli mwelekeo wa maisha ya Watanzani? Tutizame hili kupitia barabara mbovu, kilimo cha jembe la mkono na tena kutegemea mvua asilimia 100, ukosefu wa nyumba za walimu, ukosefu wa ajira na hata wafanyakazi wa serikali kutotimiziwa madai yao.
Watanzania yatupasa kuwa makini uchaguzi huu unaokuja ili tuwapate viongozi wanaofaa kwa maendeleo yetu. Tuepuke takrima, kwani ni tone la maji safi katika bahari ya maji machafu.
0769286227/0656438724
tom.thecritic@hotmail.com
Mwandishi wa mtazamo huu msomaji wa gazeti hili.