HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 27 julai 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti
SIDO na mkakati wa kusaidia waganga wa jadi kutangaza dawa

Ezekiel Musuguru

 

UKIAMBIWA uchague moja kati ya afya na mali, utachagua nini? Kama ukiwa na akili timamu ni wazi utachagua afya.

Tukumbuke kuwa wakoloni walipokuja kututawala walitukuta tunao waganga wa jadi wakitibu maradhi ya aina mbalimbali ili tuwe na afyra bora.

Lakini walipofika katika nchi yetu, kosa moja walilolifanya ni kudharau na kupuuza elimu yetu ya jadi kwa kutudhalilisha.

Walipiga marufuku mambo mengi ya jadi wakayaita ya kishenzi na kutupachika yale ya kwao ili tuakisi.

Laiti wangejifunza na kufanya utafiti wa elimu ya jadi wangegundua mambo mengi mazuri, hivyo kuyaboresha.

Walikuwapo wazee wenye vipaji maalumu lakini walipuuzwa na kukatishwa tamaa hadi wamekufa bila kuacha kwa yeyote na hivyo vipaji vyao havikurithiwa na yeyote katika kizazi cha leo.

Hutaamini kuwa mtu akivunjika mguu mganga wa jadi aliweza kuunga mfupa kwa kutumia kivuli cha ngonjwa huyo, akapona na kutembea vizuri.

Hata kule Kigoma walikuwepo wazee waliokuwa na uwezo wa kuivuta mvua ikanyesha wakati wakiihitaji.

Nakumbuka mtu wa fani hii aliitwa ‘umuvurati’, sina hakika kama watu wa fani hii bado wapo hadi hii leo.

Waganga wa jadi hadi leo tunawatambua na wanasaidia kutoa dawa za kinga na tiba ya maradhi ambayo vipimo vya kisayansi katika maabara vimeshindwa kupata chanzo chake.

Kama wezi wa mifugo wanaweza kunasa katika zizi wakashindwa kuondoka na wakalala kwenye zizi siku sita bila kujua mlango wa kutokea, hii maana yake nini kama si sayansi ya jadi?

Kwa kweli tunafanya makosa kuwaua wazee wakongwe wenye elimu ya jadi kwa kudhani kuwa wote ni wachawi, wazee hao ni hazina kubwa kwetu.

Ingefaa tuwaenzi, tuwape zawadi, tuwatumie ili waturithishe na mambo hayo ili tuyatumie katika kufanya utafiti na tuone kwa namna gani tunaweza kuyatumia katika mazingira ya leo.

Kwa kutambua umuhimu wa mambo yote haya, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO) limekuwa likiwatambua watafiti wa dawa za asili kama wajasiriamali na wafanyabiashara baada ya kuthibitishwa dawa zao kuwa zinatibu.

Hivi karibuni SIDO imeanzisha vituo vya habari katika mikoa mbalimbali nchini ili wajasiriamali pamoja na waganga wa jadi waweze kutangaza kazi zao, ili wawasiliane na wengine duniani kupitia tovuti ya SIDO kwenye mtandao ili kukuza masoko au kuboresha biashara zao.

Katika mabanda niliyotembelea wakati wa maonyesho ya biashara katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyoko katika Barabara ya Kilwa, zamani vikiitwa maarufu kwa jina la Sabasaba ni SIDO.

Mtu wa kwanza kukutana naye ni Dk. Eustance Nyakubhalo. Nilipomuuliza kwa nini yuko pale akasema amekwenda kutangaza dawa ya kutibu ugonjwa wa kisukari.

Watu wote tuliokuwepo hapo tulivutika sana kwani ugonjwa wa kisukari umekuwa ukisumbua watu kwa siku nyingi na watu wengi hawajajua kuwa kumbe iko dawa ya kutibu kisukari.

Baada ya kusoma vibali vyake kutoka kitengo cha afya na tiba asili cha Chuo Kikuu Muhimbili tulikubali kuwa yeye ni mganga halali na mazungumzo yakaanza.

Nyakubhalo anasema zaidi ya watu 300 wamekwisha kutumia dawa yake iitwayo ‘Umugoboka’ wakapona kabisa.

Anasema dawa hiyo amekwisha kuionyesha kwenye sherehe za utamaduni wa Mtanzania zilizowakilishwa kitaifa na kabila la Wahangaza na Washubi, Mei, 2009 katika viwanja vya makumbusho ya Taifa, Kijitonyama Dar es Salaam.

Anasema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye alikuwa mgeni mwalikwa katika hafla hiyo ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kujega Hospitali ya Pansiansi mkoani Mwanza na kupata fursa ya kuonyeshwa na kupewa maelezo kuhusu ubora wa dawa ya ‘Umugoboka’.

“Tunaomba viongozi waendelee kugeukia dawa hii… ni kweli inatibu ugonjwa wa kisukari, itangazwe rasmi kuwa Dk. Nyakubhao ndiye mgunduzi wa kwanza wa dawa hii,” anasema mganga huyo wa jadi.

Hivi karibuni tumemsoma Dk. Rahabu Rubago, ambaye dawa yake ya kutibu vidonda vya tumbo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeitambua na sasa inatumika kutibu ugonjwa huo ambao awali haukuwa na tiba.

Hizi ni habari za kufurahisha na kutia faraja kwa ugonjwa huu ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitusumbua sumbua.

Ugonjwa mwingine ambao bado unasumbua watu ni pumu. Magonjwa mengine ya kisasa yanayosumbua watu ni yale ya moyo, figo na ukimwi.

Inapaswa watafiti wasikate tamaa, waendelee na waongeze juhudi hadi dawa za kutibu maradhi haya zipatikane.

Katika miaka ya 1950 na 1960 kulikuwepo ugonjwa ulijulikana kwa jina la Buba. Ulitesa watu wengi. Ndui pia ni ugonjwa uliokuwepo miaka ile. Nao ulisumbua lakini ulipatiwa dawa na sasa magonjwa hayo yamebakia ni simulizi kwa watoto wetu, kwao yamefutika na wanayasoma tu katika vitabu vya historia ya afya.

Naipongeza SIDO kwa kutoa taaluma ya kubuni na kutengeneza vifungashio vya dawa za asili ili zikae muda mrefu pasipo kuharibika au kupoteza ubora wake.

Naipongeza pia serikali kwa kufuta vibali na leseni zote za waganga wa jadi ili wahakikiwe upya.

Fani hii sasa imekuwa ikiingiliwa na matapeli kila siku, kila mtaa ambapo huzuka mabango ya waganga wa jadi huku wakidai wana uwezo wa kutibu maradhi mbalimbali.

Ni vema waganga wa jadi wote wanaojiamini waende kuzipeleke dawa zao Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye kitengo cha Afya na Tiba Asilia ili zithibitishwe.

Kama nilivyodokeza awali, SIDO inawatambua waganga hawa kama wajasiriamali na juhudi zao zinatambulika kuwa zina mwelekeo na mchango mzuri katika jitihada za kupunguza na hatimaye kufuta umaskini nchini.



juu