KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo, alitangaza kikosi cha wachezaji 27 watakaoshiriki fainali za Afrika kwa nyota wa ndani, zitakazopigwa nchini Ivory Coast kuanzia Februari 22.
Katika kikosi hicho, Maximo amewaita kwa mara ya kwanza wachezaji Mwinyi Kazimoto wa JKT Ruvu na Zahoro Pazi wa Mtibwa Sugar.
Mbali ya hao, Maximo aliyetua nchini Agosti 19 mwaka 2006, amewarejesha kikosini Abdi Kassim (Yanga), Farouk Ramadhan (Miembeni), Erasto Nyoni (Azam FC), Jabir Aziz (Simba) na Salvatory Ntebe wa Azam FC.
Wengine walioitwa katika kikosi hicho kitakachoanza kampeni Februari 22 dhidi ya Senegal ni Deogratius Boneventure (Simba), Shaaban Dihile (JKT Ruvu) na Shadrack Nsajigwa (Yanga).
Wamo pia Salum Swed (Mtibwa Sugar), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Simba), Juma Jabu (Simba), Amir Maftah (Yanga) na Nurdin Bakari (Yanga).
Wengine ni Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Haruna Moshi (Simba), Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Jerson Tegete (Yanga), Mrisho Ngassa (Yanga) na Kigi Makasi (Yanga).
Nyota wengine ni Henry Joseph (Simba), Athumani Idd ‘Chuji’ (Yanga), Nizar Khalfan (Moro United), Geofrey Bonny (Yanga) na Uhuru Seleman wa Mtibwa Sugar, huku Meshack Abel akitemwa.
Kikosi hicho kimetangazwa ikiwa ni siku 20 kabla ya kuanza kwa fainali hizo ambazo ni mara ya kwanza kufanyika kwa lengo la kukuza viwango vya wachezaji wasio wa kimataifa.
Katika michuano hiyo, Stars iliyo kundi B, imepangwa na timu za Zambia, Senegal na Ivory Coast huku kundi B, likiwa na timu za Zimbabwe, Ghana, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Stars ilipata tiketi hiyo baada ya kuzing’oa timu za Kenya, Uganda na Sudan katika kampeni ya kutafuta nafasi.