BARAZA la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania, limesema Watanzania wana akili lakini hawazitumii kufanya mipango ya kuletea maendeleo.
Badala yake limesema wanatumia akili hizo kufanya mipango mibovu na hivyo kuiuza nchi kwa wajanja.
Maaskofu hao, wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Rais wa Baraza hilo, Mhashamu Yuda Thadei RuwaiIchi, wametoa tamko hilo kwenye ujumbe wao wa Kwaresma wa mwaka huu, wenye kaulimbiu ya “Kwangu Mimi Kuishi Ni Kristo” (Flp 1: 21), uliosainiwa na maaskofu wa majimbo yote 32 nchini.
Katika ujumbe huo ulioandikwa Februari 11, mwaka huu na kusambazwa nchi nzima, maaskofu hao walisema inashangaza kuona hadi leo Watanzania wengi hawajatambua umuhimu wa kufanya kazi na pia kuwa utajiri wa nchi, hutokana na jasho la wananchi wenyewe.
“Tuna mapori yenye rutuba, misitu, mabonde, mito, maziwa, bahari, milima na madini ya kila aina. Tusipoyatolea jasho kwa kufanya kazi, yatabaki hivyo hivyo, nasi tutaendelea kulalamika juu ya umaskini,” lilisema tamko hilo.
Kwa mujibu wa tamko hilo, Watanzania wana nguvu ambazo hazitumiki au zinatumika bila maarifa.
Maaskofu hao walisema ni jukumu la Watanzania kufanya kazi kwa bidii na uzalendo katika sekta zote zikiwamo za elimu tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Kuhusu suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe, tamko hilo lililaani mauaji hayo yanayotokana na imani za kishirikina kwa lengo la kujipatia utajiri.
“Tunalaani vikali vitendo vilivyosambaa sehemu nyingi nchini vinavyodhalilisha uhai wa binadamu kama vile utoaji mimba, watu kuwaua maalbino, wazee na watoto, kuchuna ngozi za binadamu kwa imani za ushirikina na uchu wa kupata utajiri bila kufanya kazi, mambo yote haya yanaashiria kujengeka kwa utamaduni wa kifo katika jamii yetu.
“Sheria ya Mungu inatuambia usiue, tusiue mtu yeyote katika kipindi chochote cha maisha yake kwa lengo lolote lile. Tusiue mtu wa sura yoyote, wa rangi yoyote, wa umri wowote na wa asili yoyote, kwani binadamu wote tumeumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu,” ilisomeka sehemu ya tamko hilo.
Wakizungumzia suala la uchangiaji wa elimu ya juu, maaskofu hao walipendekeza serikali iweke mazingira ya vyuo vikuu katika mpangilio wa kutosha na kufaa kwa elimu ya juu ili wanachuo wasome kwa utulivu.
“Hatujaweza kufikia lengo hilo kikamilifu katika nchi yetu. Lakini utulivu katika vyuo hautegemei tu ukamilifu wa miundombinu. Sehemu kubwa inategemea namna jamii yote ya chuo inavyojipanga kinidhamu na kimaadili. Dhana ya kudhani kwamba ni wajibu wa utawala kufanya kila kitu na kudai maslahi kila mara haitupeleki mbali. Tunahitaji ushirikiano na kusikilizana pande zote,” walisema maaskofu hao.
Kwa upande mwingine, walisema Serikali na mamlaka za vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu, wawatendee haki wanafunzi kwa kuwatimizia madai yao halali na ya haki kwa kutazama upya sera ya uchangiaji wa elimu ya juu.
Walisema migomo na vurugu vyuoni, huchangia kuharibu sifa ya nchi na kuichafua katika sura ya kimataifa.
Kuhusu suala la kutosema ukweli, maaskofu hao walitahadharisha kuwa “mahali pasipokuwa na ukweli hapana utulivu, hakuna amani, badala yake kuna hofu, wasiwasi, mahangaiko, kutoaminiana; hakuna utulivu wala usalama.”
“Harakati za kuishi zinakuwa jambo la patashika, mwenye nguvu anatumia mabavu kupata mradi wake na mnyonge kwa bahati mbaya hapati kitu,” walisema.
Walisema wananchi wanapenda kuona viongozi wakiwa waaminifu kwa kuwa uaminifu ni tabia inayokubali kuwajibika kupokea majukumu waliyopewa na kuyatimiza kwa makini.
“Wananchi wanafurahi wakiona viongozi wao na Serikali inatimiza majukumu iliyopewa au iliyoahidi kwa wananchi wake,” lilisema tamko hilo.
Wakizungumzia tatizo la rushwa, maaskofu hao walisema watu wengi wanaendelea kutoa na kupokea rushwa, licha ya juhudi za Serikali na dini kukemea uovu huu.
“Hali hii inachukiza kweli, lakini tufanye nini? Ubovu huu umekomaa kiasi kwamba jamii nzima inatembea na donda hili, bila kujali maumivu yake, yaani ni kama jamii imekubali kuishi katika upotofu.
“Wanajua ni kitu kibaya, lakini kimaisha wanakimeza, ndiyo kusema kuwa Watanzania wengi dhamiri zao zimekufa, hazioni kuwa rushwa ni dhambi. Tubadilike,” wamesisitiza.
Pia walisisitiza suala la kuishi na kuthaminiwa, uhuru wa kuabudu na uraia, kwamba ni haki za msingi ambazo Watanzania hawana budi kuziheshimu kwa kuwa zimefafanuliwa na kuthibitishwa na Katiba ya Nchi, Sheria, na Hati ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu.