HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 19 mei 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
KICHENI PATI: Maadili hayafuatwi

Mwandishi wetu

 

KITCHENI Pati ni sherehe mahsusi anayoandaliwa mwali ama binti ambaye ameshakua mwenye uwezo wa kupata mtoto. Kwa sisi Waafrika tunasema ameingia katika kundi la watu wazima.

Binti huyu amejivua ‘gamba’ la utoto na sasa yuko katika matarajio ya kuanza maisha yake mpya, kwa kuolewa na kupata jina jipya au cheo kipya kama ‘mke’ au ‘mama’ ndani ya nyumba yake, si-mtoto tena, ingawa upo msemo wa kuwa ‘mtoto’ kwa mama au kwa wazazi hakui ni mtoto tu.

Utaratibu stahiki wa sherehe hiyo kwa miaka ya hivi karibuni haufuatwi kabisa, yawezekana ni kutokana na walengwa wengi, nikimaanisha wanawake, kutoyajua; au kutenda tofauti kwa makusudi kabisa ili kukidhi malengo na matakwa yao ya starehe.

kiasilia, yaani ule uasilia wa uanzishaji wake tafrija hiyo ni tofauti na unavyofanywa sasa.

Huko ughaibuni kwa lugha ya mtaani, Ulaya, tafrija hii ilianzishwa na wasichana au mabinti wa rika la mwali mhusika wakichanganyika na wasichana wengine wachache ambao wameolewa, lakini si kwa miaka mingi, na wale ambao bado hawajaitwa kina mama yaani watu wazima.

Madhumuni hasa ya tafrija hii ni kumuaga na kumtakia kila la heri binti mwenzao, na pili kumzawadia vyombo na vifaa mbalimbali vya kutumia jikoni pindi tu anapoanza maisha mapya akiwa ni mke wa ‘mtu’.

Tafrija hii inaandaliwa kwa gharama za hiyari kwa kila msichana – rafiki, na hata vinywaji na vitafunwa kila mmoja wao analeta kile anachotumia mwenyewe au kile cha ziada kwa ajili ya wengine; kwa lugha ya ‘kinyamwezi’ wanaiita ‘bottle party’ kutokana na ule mtindo wa kuja na kinywaji chako.

Je, wazazi wa binti mhusika walikuwa wanahusishwa na tafrija hiyo? HAPANA! Wao wanachoombwa ni nafasi tu ya kutumia pale nyumbani, hivyo wazazi hao wanaondoka kwa muda unaohitajika na kurudi mara tatrija husika itakapomalizika.

Yawezekana pia wazazi hao wawili yaani baba na mama (kama wapo) wakawezeshwa na hao mabinti kwa kulipiwa mahali iwe ni hotelini, au klabu kwa vinywaji vichache vya kuanzia. Gharama za tafrija hiyo haziwahusu wazazi hao hata kidogo.

Je, tafrija hizo zinafanywa wakati gani? Mara nyingi huwa ni kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni au saa 1:00.

Hebu tuangalie, ‘kitchen parties’ tunazozishuhudia hapa kwetu wakati huu. Ni kweli zinahusisha kumzawadia ‘binti’ mhusika vyombo au vifaa vya jikoni pamoja na hivyo uandaaji wake unahusisha wazazi kwa baadhi ya gharama, unahusisha mabinti na kina mama yaani watu wazima labda ni marafiki wa mama wa binti huyo; zinafanywa katika kumbi za starehe na hata wazazi wa kike na ndugu za bwana harusi-mtarajiwa wanaalikwa. Jambo la kushangaza anatafutwa mwanamama maalumu kuja kutoa ‘kunga za ndoa’ kwa mwari- muhusika siku hiyo. Jambo ambalo si mahala pake asilaani. Mama huyo huitwa au hujiita ‘somo’ na analipwa ujira fulani.

Kinachofanyika hapo ni sikitiko kwa kina mama wengi wenye staha na heshima zao; kwani wengi wa hao ‘ma – somo’ hutumia lugha zisizo na kificho wala staha, lugha nachelea kusema zilizopitiliza haiba ya utu wa mwanamke mbele ya kadamnasi, wakidhani na kuamini ya kuwa ‘binti’ hajafundwa huko kwao kwa yale wanayoamua kumtolea somo wakati huo.

Vitendo vinavyoashiria matukio ya ngono huonyeshwa waziwazi, na wengine kati hao ‘ma- somo’ wakiwa na wafuasi ama mashabiki wao hufikia hatua ya kujiweka nusu- uchi, kuonyesha hata vivazi vyao vya ndani; na hao mashabiki wao wakiwashangilia kwa nderemo kali na hata kuwatunza kwa mtindo wa kupokezana; wenyewe wanaita ‘staili ya Ki-Nigeria; kutunza noti moja moja. unatunza nini? tukio lililo kinyume cha maadili stahiki ya mwanamke? Ni aibu tupu, ukweli ni kuwa tunawapotezea mabinti hao maadili stahiki ya kuanzia vijembe na mafumbo ya nyimbo za rusha roho- taarabu! Pia upo mtindo wa kuonyesha nguo alizoletewa ‘mwari’ huyo wanaita ‘kusasambua’ – huonyeshwa hadi nguo za ndani! Aibu.

Misemo potofu na michafu ya kama “mwanamke sharti uwe na kidumu; mwanamke mboga tatu au nne” ndizo zinazotawala. Ni lugha- potofu, zikimaanisha ‘mwanamke ukiwa na mumeo – yaani ndoo, uwe na ‘kidumu; yaani bwana wa nje ya ndoa; na ndio hiyo ‘mboga’ tatu au nne; yaani wanaume wengine wa kukuliwaza pindi unapokosana na mumeo. Huu ni ushetani na wala sio maadili mema.

Yapo mengi yanayowakera baadhi ya wahudhuriaji wa ‘kitchen parties’ hizo potofu, nasisitiza kusema ‘sio zote’; walengwa wanayajua wala sihitaji kuyaanika yote hapa, najua wale wanaokumbatia tabia na matendo hayo potofu na wapambe wao, wanatamani wanisute, waniulize ulihudhuria kufanya nini? Jibu ni kuwa iko mikanda ya video kibao wanayoita ‘laivu’ na tukiwa nje ya kumbi zenye baa tunasikia kila kitu kwenye vipaza sauti.

Nitawashtua na kuwaumbua mara wakijaribu kufumbua midomo yao; kwani wanahatarisha maisha ya ndoa za wari hao; najua kwa baadhi yao huu umekuwa ni mradi, ila ni mradi mchafu. Narejea kusema ‘sio kicheni pati’ zote!

Uvaaji wa baadhi ya wakorofi hao wa ‘kitcheni parties’ unatia kizunguzungu kwa kina mama wenye heshima zao; wanabaki wakikodoa macho ya mshangao na midogo wazi wakati wote. Wakorofi hao wenye majina mengi tu, huvaa nguo aina za ‘madira’ na wafikapo ukumbini huzivua na ndipo ‘viwalo’ vya ajabu hutawala, na wakipata ‘stimu’ yaani ulevi ndipo wanapoonyesha aina ya michezo na mitindo ya ajabu- ajabu bila soni kwa mualikwa yeyote, wakirushiana vijembe kati ya makundi yao.

‘Kitchen Parties’ sasa zinaanza saa 12 jioni hadi saa 6 za usiku . Je, mwari yule akipotoka kidogo kidogo huko kwa mumewe, mnategemea wakwe na wifi zake watasemaje? Je, hawatamhusisha na yale waliyoyashuhudia wakati wa tafrija yake? Je, hawatawahusisha na ninyi wazazi wake na ndugu wa karibu mlioandaa tafrija hiyo? Na je, wanaume wana husikaje na ‘kitchen parties’? Kimaadili hawahusiki wala kuhitajika uwepo wao kabisa!

Hata kama wao wenyewe na hao wanaowaalika wakijenga hoja ya uwepo wao, hazitakidhi mantiki ya tafrija hiyo kwa kuhudhuria kwao na kutoa mada asilaani; kwani wahusika wakuu wanajulikana kimaadili na hata kimaumbile. Nawasihi wanaume acheni kujihusisha na kitchen parties kwa heshima yenu.

Namalizia kuwaasa ya kwamba kitchen party sio kabisa mahali pa- kutoa mada za ‘kunga za ndoa’; kwani mada na masomo hayo yanatolea kwa siri sio mbele ya kadamnasi tena na watu maalumu katika jamii tukio hilo huitwa ‘Unyago’.

Nawapongeza wale wote wanaofanya kicheni pati zao kwa staili na utaratibu wenye staha kwa jamii husika.

Wazazi na ndugu wa ‘wari’ nawasihi jengeni ujasiri wa kuamua kuwa sasa basi, na mrudi kwenye sherehe stahiki kudumisha heshima ya mwanamke; na kumjenga mwari kiasili, kimaadili. Nidhamu na kumpa ‘soni’ ya mwanamke kwa matendo mema. Nitazungumzia ‘Bachelors Party’ wanayoita sasa ‘Bag Party’ nikipata wasaa. Namaliza! Ni mimi MC Mackie G. Mdachi – “MC Mkongwe”.



juu