KWA mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha (chapisho la Oxford) lililotolewa Zanzibar, ‘muungano’ ni hali ya kushikana na kuwa pamoja. Kamusi ya Karne ya 21 (chapisho la Longhorn) itumikayo zaidi Tanganyika, yaeleza kuwa ‘muungano’ ni mshikamano wa pande mbili au zaidi kuwa kitu kimoja.
Kamusi hizi mbili zinatoa tafsiri ya ‘muungano’ kuwa ni kushikana/mshikamano. Tafsiri ya ‘mshikamano’ kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha ni ushirikiano wa watu katika jambo.
Kamusi ya Karne ya 21 imefafanua vizuri zaidi kwa kueleza kuwa ‘mshikamano’ ni hali ya kuwa na msimamo na ushirikiano katika kutimiza lengo fulani.
Tafsiri zote zinasisitiza umoja, yaani kuwa na muungano; ushikamano, ushirikiano. Pia ni mjumuiko wa watu, taasisi au nchi. Hii ndiyo tafsiri sahihi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuhusu Jamhuri ya Muungano na Watu yasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Sasa kama kifungu hiki kinafuatwa mbona kuna Katiba mbili ya Tanzania na ya Zanzibar? Tangu lini nchi moja ikawa na Katiba mbili? Hali inayojitokeza sasa kule Zanzibar inaathiri Muungano na kutia shaka kama kuna mshikamano na umoja wa kweli baina ya pande hizi mbili.
Ibara ya 2 (1) yasema: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.” Mbona Zanzibar inataka iwe na mipaka yake ya bahari na mafuta yatakayogunduliwa eneo la Zanzibar yasiwe chini ya Muungano? Hii ni nchi moja kweli au mbili?
Imeelezwa kwenye Katiba ya Tanzania ibara ya 3 (1) kuwa “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.” Kama demokrasia inafuatwa, iweje wananchi wawekewe mipaka ya kuujadili Muungano bila kueleza hisia zao kwa uhuru? Ujamaa unaoelezwa kwenye ibara hii u’wapi? Mbona ulizikwa Zanzibar na sasa badala ya ujamaa ni ubepari na ufisadi ‘kwa kwenda mbele’?
Kama serikali ya Tanzania haina dini rasmi kwa nini Wakristo hawatakiwi Zanzibar? Makanisa yanachomwa moto kwa kutotakiwa katika visiwa ambavyo ni sehemu ya Muungano. Dini ni imani inayohusiana na mambo ya kiroho baina ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Kwa nini basi wafuasi wa dini moja waonekane hawafai kuwepo eneo jingine la Jamhuri ya Muungano? Ingekuwaje kama Waislamu wangefukuzwa katika maeneo ya Wakristo wengi?
Muungano ni jambo moja na imani ni jambo jingine. Kwa nini Wakristo waingiliwe katika imani yao kwa kisingizio cha kutoukubali Muungano? Kwani Muungano ulipandikizwa na Makanisa hata leo yachomwe moto? Hakuna sehemu yoyote kwenye Biblia Takatifu wala Kurani Tukufu inayohalalisha matumizi ya nguvu na unyanyasaji ili kuwaingiza waamini wa dini nyingine na maamuma (mtu asiyekuwa na uamuzi kwa analoambiwa) kujiunga na Ukristo au Uislamu.
Je, Muungano huu uliotiwa saini Aprili 26, 1964 ulipata ridhaa ya wananchi kwa kupigiwa kura ya kuukataa au kuukubali? Nakumbuka nilipokuwa mwandishi wa gazeti maarufu (wakati ule) lililoitwa Ngurumo, tulipata habari za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kupitia gazeti la Tanu lililoitwa The Nationalist likieleza habari hiyo kwa mistari isiyozidi kumi katika ukurasa wake wa mbele.
Huenda wakati ule ilikuwa muafaka kuharakisha Muungano uliotiwa saini na Rais Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika na Rais Abeid Amaan Karume wa Zanzibar (Mungu awarehemu) kutokana na usalama wa nchi hizi mbili. Hali ilivyo sasa si kama ya wakati ule. Wananchi wameerevuka na wanajua kuchambua mambo.
Laiti wananchi wangeshirikishwa kuujadili na mwishowe kuupigia kura kuukubali au kuukataa, mtafaruku (hali ya kutoelewana) unaokua kila siku kati ya Tanganyika na Zanzibar usingekuwepo. Baya zaidi ni serikali ya CCM kukataza suala la Muungano wa Tanzania kujadiliwa wakati wa kutoa maoni ya Katiba mpya!
Jumapili ya Mei 27 asubuhi nikiwa ndani ya basi litokalo Gongo la Mboto kwenda Kivukoni jijini Dar es Salaam, niliguswa na mazungumzo ya Wazanzibari wawili waliokaa kiti kimoja nyuma yangu. Walisema wao (Wazanzibari) hawahitaji Katiba kwani tayari wanayo yao na kama ni kujadili Katiba ni suala la Watanganyika, kwani wao haliwahusu. “Tuna sirikali yetu siye … raisi wetu … Baraza letu la Wawakilishi … bendera yetu na wimbo wetu wa taifa. Watanganyika wabaki na huo Muungano wao siye hatuuhitaji …”
Watu hao wakaenda mbali zaidi, wakisema Kikwete amewanyima Wazanzibari haki ya kupokezana madaraka kati yao na Watanganyika. “Kikwete amekuwa rais kwa awamu mbili ambapo ingekuwa zamu ya Mzanzibari kuwa rais wa Tanzania lakini haikuwa hivyo!”
Kwa wanaofuatilia makala zangu, niliwahi kuandika kuwa Watanganyika hawapendwi Zanzibar. Katika ghasia za juzi, vipeperushi vinavyowataka Watanganyika wanaoishi visiwani humo waondoke, viliwekwa kwenye milango ya nyumba wanazoishi. Ndiyo maana wahenga walisema ‘akuchukiaye hakosi ila ya kukutia.’
Wanaharakati wa Kiislamu chini ya mwongozo wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) wamekuwa wakiupinga Muungano wa Tanzania kwa maandamano wakidai Zanzibar kuwa nchi huru. Lazima serikali ya Muungano itambue kuwa ‘mwanzo wa ngoma ni lele’ na katika hali hiyo, wananchi wapewe uhuru na haki ya kujadili hatima ya Muungano.
Serikali inaposema suala la Muungano silijadiliwe kwenye kutoa maoni ya Katiba mpya inafanya kosa kubwa lililoanza kuleta uhasama na madhara.
Muungano si wa viongozi bali ni wa wananchi ambao ndio wenye mamlaka ya kuukubali au kuukataa. ‘Humpendaje mtu kwa kuambiwa penda’? Yawezekana vipi kumpenda mtu kwa kuwa umeambiwa umpende? Haiwezekani kulazimisha hisia ya binadamu. Kama mtu hakitaki au hakipendi kitu ni vigumu kumfanya akipende kwani kupenda hutokana na hisia ya mtu mwenyewe.
Pamoja na hayo, Wazanzibari wasiwe na jazba kwani ‘mfukuzwa kwao hana pa kwenda.’ Hapa wanapata fundisho la umuhimu wa kuhusiana na jamaa zao vizuri pamoja na kuwathamini kwa kuwa ndio wanaoweza kuwategemea wapatwapo na shida.
Kama kufukuzana kutoka sehemu moja kwenda kwingine kukinyamaziwa, waathirika wakubwa watakuwa Wazanzibari walioenea kila pembe ya Tanganyika. Majumba na biashara zao watawaachia nani wakitakiwa kufunganya (funga pamoja vitu au mizigo kwa ajili ya safari) ili warudi kwao kama wanavyowafanyia wenzao wa Bara walioko visiwani? Halahala mti na macho!