MAMLAKA ya Mapato (TRA) Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya imeweka mkakati mpya wa kutatua kero na malalamiko yanayotolewa na wananchi ili kusiwepo na msuguano wakati wa zoezi la ulipaji kodi na ukadiriaji wake.
Hali hiyo imejitokeza baada ya wafanyabiashara kulalamikia suala la utoaji elimu kwa walipa kodi kuwa haiwafikii ipasavyo wafanyabiashara wadogo wanaoibuka na kujikuta wakifanya biashara zao bila kujua hazipaswi kulipiwa kodi.
Mfanyabiashara huyo, Mpaluka Mdude, mkazi wa Ichenjezya, alisema ipo haja kwa wafanyabiashara kupatiwa elimu ya kutosha, ili iwe rahisi kwa serikali kukusanya mapato yake.
“Sisi kama wafanyabiashara wadogo tumekuwa tukifanya biashara bila kujua taratibu, hivyo ni jukumu la TRA kutupatia mafunzo ya walipakodi, ili kuondoa mgongano na kudhani kuwa vijana ni sehemu ya wakwepa kodi kumbe elimu ni ndogo,” alisema Mdude.
Naye Golden Mwashiuya, mkazi wa Mlowo alisema TRA itafanikiwa kukusanya mapato yake endapo vitendo vya rushwa na unyanyasaji vitaepukwa na watumishi wasiokuwa waaminifu.
Meneja wa TRA Wilaya ya Mbozi, Deogratius Moshi akizungumzia mikakati ya uboreshaji wa huduma kwa wateja, alisema ili kuondoa kero na malalamiko ya walipa kodi, elimu kwa mlipa kodi imekuwa ikitolewa mara kwa mara sambamba na matumizi ya vyombo vya habari.