BODI ya Mashindano ya Miss Utalii Tanzania, imeanza kuonesha cheche zake kwa kishindo baada ya kufumua mfumo mzima wa uongozi na mashindano hayo nchini.
Katika kikao chake kilichofanyika mwishoni mwa wiki, chini ya Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Abubakari Omari Abubakari, bodi hiyo imechukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuboresha na kuimarisha mashindano hayo yenye manufaa makubwa kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kitaifa na kimataifa.
Abubakari alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, bodi hiyo imeazimia kuchukua hatua katika nyanja mbalimbali za mashindano hayo, kuanzia mfumo wake, uongozi, utawala na uendeshaji mzima.
“Baadhi ya mabadiliko hayo ni kuwa, Miss Tourism Tanzania Organization, ni taasisi ambayo kuanzia sasa itaendeshwa kwa mfumo wa kitaasisi, ambayo sasa badala ya kuwa ya mashindano ya urembo pekee, inakuwa ni ya kuhamasisha na kutangaza utalii, utamaduni, mazingira, elimu, afya ya jamii, bidhaa za Tanzania, uvuvi, wanyamapori, madini, hifadhi za bahari, sera za taifa za utalii, utamaduni, kilimo, mazingira, umasikini, vijana, wanawake na watoto, utalii wa michezo na utalii wa mikutano,” alisema.
Alisema, mafanikio hayo yatafikiwa kupitia mashindano ya Miss /Binti Utalii Tanzania, Miss Tourism Tanzania International, Miss Tourism University World, Miss Heritage World, Tanzania Beauty and Model Management, National Parks Marathon, Tanzania Great Safari and Tour na Tanzania Cultural Carnival and Festival kila mwaka.
Aliongeza kuwa, kuanzia mwaka huu, pamoja na shindano la kitaifa la Miss Utalii Tanzania, fainali za taifa zitakwenda sambamba na Miss Tourism Tanzania International, ambako washiriki wa Tanzania watapanda jukwaani kuwania taji la taifa, sambamba na washiriki waalikwa kutoka nchi mbalimbali duniani, ambako washindi wake watakuwa mabalozi wa Tanzania katika mabara na nchi zao.
“Bodi imefanya uchambuzi wa kina wa wakurugenzi na waandaaji wa ngazi mbalimbali na kupitisha azimio la kuwataka waandaaji wa majimbo (vitongoji), wilaya, mikoa, mikoa maalumu ya vyuo vikuu, kanda na kanda maalumu za vyuo vikuu, kuomba upya na kutoa fursa kwa watu na kampuni mbalimbali kuomba kuandaa katika ngazi yoyote nchini,” alisema.