WIKI hii, Juni 12 dunia iliadhimisha siku ya kimataifa ya kupambana na ajira dhidi ya watoto, ambapo Shirika la Kazi Duniani (ILO) limetoa takwimu zinazoonesha kuwa watoto milioni 215 wanafanyishwa kazi, nusu yao katika mazingira hatari.
Watoto hawa hufanyishwa kazi katika majumba ya watu, machimbo ya dhahabu, wanatupa taka, ama wanasuka mazulia katika viwanda. Hawawezi kuandika hata jina lao, ama kusoma kitabu, kucheza kwao ni jambo ambalo hawalijui.
Zenabou Ilboudou ni dada mkubwa. Sio katika hali halisi, hapana, dada huyu mwenye umri wa miaka 20 anafanya kazi katika wakfu wa Terre des Hommes, kama dada mkuu, kwa wasichana, ambao wamekuwa wakifanyishwa kazi kama wafanyakazi wa ndani.
Amekuwa dada mkuu kwa sababu anafahamu tatizo hili, kwa kuwa yeye binafsi kwa muda wa miaka saba aliwahi kufanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou. Wakati akianza kazi hiyo alikuwa na umri wa miaka tisa.
“Asubuhi 11 anakuamsha mama mwenye nyumba, ili uanze kazi za ndani, na ananipa pesa kwa ajili ya kununulia vyakula vya nyumbani. Baada ya hapo hupika, na wakati baba mwenye nyumba hatapendelea mchuzi uliotengeneza, unaingia katika matatizo.
“Iwapo hutapigwa, utagombezwa na kutukanwa. Mchana kupata chakula ni taabu. Sehemu yako ya kulala mara nyingi ni jikoni ama sakafuni,” anasema.
Burkina Faso pamoja na nchi nyingine za Afrika, kuna maelfu kadhaa ya wafanyakazi wa nyumbani ambao wamefikwa na madhila yaliyomfika Zenabou Ilboudou.
Wengi wao wako katika umri kati ya miaka 9 na 14, wakati walipoanza kutafuta kazi. Wengi wao wanakimbia kutoka katika familia zao kwa sababu wazazi wao hawana fedha, ama wameuzwa.
Masharti ya kazi kwa kiasi kikubwa ni kinyume na ubinadamu, watoto wanatumiwa kama watumwa, hupigwa, hufanyiwa mambo mabaya, ama kudhalilishwa kingono.
Halima Fogo hivi sasa ana umri wa miaka 21. kwa muda wa miaka sita alikuwa akifanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani, na amekuwa akidhalilishwa kingono mara kwa mara na waajiri wake wanaume.
“Wakati baba mwenye nyumba akitoka kazini na kurudi nyumbani, kwa kuwa mke wake hayuko nyumbani, anaanza. Hunipa vishawishi, na kusema iwapo nitalala nae, mwishoni mwa mwezi ataniongezea mshahara,” anasema Halima.
Ni vishawishi ambavyo ni kinyume na ubinadamu, ni ahadi za uwongo. Zaidi ya hayo, sehemu kubwa ya watoto wanaofanyishwa kazi, kiasi ya theluthi moja, hata hivyo hupata sehemu ndogo ya mshahara wao, ama hawapati kabisa.
Burkina Faso, wasichana wengi wanafanya kazi katika kile kinachoitwa sekta isiyo rasmi, katika sekta hii hakuna mkataba ama mafao ya kijamii.
Wakati huo huo, Serikali ya Burkina Faso inatambua matatizo haya na inajaribu kubadilisha mwelekeo huo, kwa kushirikiana na mashirika kadhaa ya kijamii nchini humo, na hata pia mashirika ya kimataifa kama Terre des Hommes ama Shirika la Umoja wa Mataifa ya Kuwahudumia Watoto (UNICEF).
Herman Zoungrana, meneja mradi wa Terre des Hommes nchini Burkina Faso, anaelezea kile shirika hilo inachokifanya.
“Kwa hivi sasa tuna mpango unaowahusu wasichana 700, ambao wameweza kwenda shule katika vijiji wanakotoka, pamoja na mradi wa mafunzo ya kazi unaowahusu karibu wasichana wengine 100. Na wengine zaidi ya 100 wanasoma katika shule ya sekondari katika mji wa Tougan, kaskazini magharibi ya Burkina Faso,” anasema Zoungrana.
Shirika la Kazi la Kimataifa nchini Burkina Faso linasema: “Hata hivyo, kwa bahati mbaya hili ni tone tu linalodondoka katika jiwe lenye joto. Zaidi ya watoto 500,000 wanafanyishwa kazi.”
Na hii si tu katika majumba ya watu binafsi. Karibu nusu wanafanya kazi katika takribani machimbo 600 ya dhahabu nchini humo.
Mikono midogo ya vijana hawa hutumika kuvunja vunja mawe ili kuweza kupata dhahabu. Miili midogo ya vijana hawa hutumika kupenya katika mashimo madogo ya machimbo ya dhahabu.
Mapafu yao huvuta hewa chafu ya kemikali zenye sumu za sianidi, ama kemikali za asidi salfuriki. Hawana muda wa kupumzika, wanafanya kazi mpaka usiku wa manane. Malipo kwa watoto hawa ni ya shida, hupewa chakula tu.
Shule nyingi katika eneo lenye machimbo ya dhahabu zina wanafunzi wachache. Watoto wameamua kuwa hawana muda wa kwenda shule.
UNICEF imefanikiwa kuwapeleka watoto 7,000 shuleni na hii ni hali ya kutia moyo.
Na mafanikio haya si rahisi kila mara. Kwa sababu kazi katika machimbo ya dhahabu inawavutia watoto wengi licha ya ugumu wake.
Wanafikiria kufanya kazi ya kuvunja mawe na kupata dhahabu kidogo ili kupambana na umasikini unaowakabili.