HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 16 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Jinsi ya kukabiliana na hasira za ghafla kwa mtoto

Lwitiko Peter Sr

 

KATIKA makala iliyopita, tulianza kuangalia suala la watoto wanaopatwa na hamaki na hasira za ghafla.

Tuliona ni nini kinaweza kusababisha hali hii. Pia tulianza kuangalia mzazi anapaswa kufanya nini kukabiliana na hali kama hii.

Leo tuendelee na kuangalia hatua zaidi ambazo mzazi anaweza kuzichukua iwapo atakuwa na mtoto mwenye kupata hasira za ghafla.

Moja kati ya mambo muhimu kuyazingatia ni kwamba, hali hii isikufanye mzazi uanze kubadilisha taratibu za malezi kwa mtoto wako kama njia ya kutaka kumridhisha asifanye fujo.

Kwa kawaida, kila mzazi anakuwa na utaratibu wake wa malezi unaohusisha kanuni ambazo yeye na mtoto wanapaswa kuzizingatia na kuzifuata.

Iwapo utabaini kuwa kanuni na taratibu hizi si sababu ya mtoto kuwa na hasira kali, basi usizibadilishe.

Kama ukifanya hivyo, itakuwa sawa na kumdekeza mtoto. Utamjengea kiburi kuwa akitaka kitu chochote kifanyike basi aanzishe zogo kwa hasira kali.

Kanuni zibadilishwe pale tu itakapobainika kuwa zenyewe ndizo chanzo cha mtoto kuwa na tabia hiyo ya hasira.

Lakini katika kipindi hiki, mzazi anapaswa kuangalia zaidi tabia nzuri za mtoto na kumzawadia anapofanya jambo zuri.

Mathalani, iwapo mtoto anapopatwa na hasira hizi ghafla anakuwa na tabia ya kupiga kelele, kujigaragaza au kurusharusha vitu hovyo, hakikisha kuwa anapoelezwa na kuacha kufanya hivyo, asifiwe kwa kuwa msikivu.

Huu ni wakati ambao mzazi anapaswa kuwa karibu zaidi na mtoto. Anapaswa kuzungumza na mtoto kwa upendo mkubwa.

Iwapo mzazi utaonesha upendo mkubwa kwa mtoto, kuna uwezekano mkubwa akabadili tabia yake.

Haya tuliyoyaona ni yale ambayo mzazi anaweza kuyafanya iwapo hali hii itatokea. Lakini pia zipo njia za kuzuia hali hii isitokee.

Kama mtoto alishaanza kuonesha tabia hii, unapaswa kuanza kuchunguza na kubaini ni nini hasa kinamsababishia hali hiyo.

Ukishabaini, ni vema ukajitahidi kuepusha hali hiyo kutokea ili mtoto asipatwe na hasira hizo.

Kama mtoto anapatwa na hasira kwa sababu anazuiwa kufanya jambo fulani ambalo halimo kwenye utaratibu, basi hakikisha kuwa unaziweka biskuti katika sehemu ambayo mtoto hataziona.

Wakati mwingine, wazazi huwa wanawachosha watoto na hawawapi muda wa kupumzika wa kutosha.

Hivyo, hakikisha kuwa ratiba ya mtoto kucheza na kupumzika inafuatwa kwa ukamilifu.

Ni vema mtoto awe na ratiba ya kulala wakati wa adhuhuri kabla hajaingia kwenye michezo ya jioni.

Hii itaupatia ubongo wake na mwili mapumziko na kumwandaa kuwa na nguvu kwa ajili ya shughuli nyingine.

Hakikisha pia mtoto anakuwa ameshiba wakati wote. Wapo wazazi ambao mtoto akirudi shuleni, kama huko shuleni wanapatiwa chakula, basi yeye hajali kumpatia mtoto chakula.

Hakikisha anaporudi shuleni mtoto aulizwe iwapo anahitaji chakula au la. Kama una uhakika kuwa shuleni wanapatiwa chakula cha kutosha, basi anaporejea adhuhuri, ni vema apatiwe vitafunwa na kinywaji kama vile juisi.

Wakati mwingine, unapohisi kuwa mtoto anaelekea kupata hasira, unaweza kuanzisha jambo jingine ili kuachana na kile anachokifanya wakati huo, maana inawezekana kuwa hicho ndicho kinampatia hasira kali.

Kama unaona kuwa hali hii inakushinda kuidhibiti, ni vema ukatafuta msaada kutoka sehemu nyingine.

Mara nyingi inashauriwa kuwa kuzungumza na wazazi wengine kuhusiana na matatizo kama haya inasaidia sana.

Mara nyingi utakutana na mzazi ambaye alishakabiliana na tatizo kama hilo, na atakupa mwanga wa jinsi ya kukabiliana nalo.

Pamoja na wazazi wengine, unaweza kuzungumza pia na marafiki au walimu wake. Nao wanaweza kuwa na taarifa nzuri kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Iwapo huko kote hautapata ushauri utakaosaidia kumaliza tatizo hilo, basi ni vema ukaonana na wataalamu wa afya kwa ushauri zaidi.

Lakini kumbuka kuwa uwe na taarifa ya kina kuhusiana na tabia hizo za mtoto wako, na uwe umeshabaini ni nini kinaweza kuwa kinamsababishia hali hiyo.

Hii itamwezesha mtaalamu kujua hatua gani zichukuliwe ili kukabiliana na tatizo hilo.



juu