TIMU ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, leo inashuka dimbani kuwakabili Ethiopia katika mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta.
Timu hizo zinakutana huku wenyeji Twiga Stars wakitoka kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili zilizopita,
mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mazingira hayo yanaifanya Twiga Stars chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa, kucheza kwa juhudi kubwa kupata ushindi katika mechi hiyo ya mwisho.
Akizungumzia mechi hiyo ya leo, Mkwasa alisema jana kuwa vijana wake wako fiti tayari kupigania ushindi na mwishowe kuitwaa tiketi ya fainali hizo.
Kama Twiga Stars itafanikiwa kutwaa tiketi ya fainali hizo, itakuwa mara ya pili kwake kwani mara ya kwanza ni mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
“Tumejiandaa vizuri kwa mechi ya kesho (leo), tunataka kusawazisha makosa yote ya mechi iliyopita. Tunaamini hata uwepo wa Mwasikili (Sophia) aliyerejea kutoka nje kumeongeza nguvu,” alisema Mkwasa.
Alisema kwa kutambua kuwa wako nyuma kwa bao moja, wataingia uwanjani na kucheza soka ya kushambulia zaidi kupata ushindi wa kutosha kuwavusha.
Mkwasa nyota wa zamani wa timu za Yanga
na Taifa Stars, alisema wanajua wapinzani wao watakuwa wakishambulia na kulinda mabao
yao, lakini watajitahidi kuwadhibiti.
Aidha Mkwasa alisema kwa matunzo na
mafunzo waliyopewa wachezaji kwa kipindi
chote cha kambi kuelekea mechi ya leo, hata wakifungwa, hawatakuwa na kisingizio.
“Tunasema, mechi ya kesho (leo), ni bora punda afe, lakini mzigo ufike, mechi hii ni muhimu sana kwetu, tunapigania tiketi ya kucheza fainali hizo mara ya pili tukiwa nyumbani,” alisema.
Naye, Kocha Mkuu wa Ethiopia, Abreham Haimanot, akizungumzia mechi hiyo, alisema vijana wake wapo fiti na hana shaka ya ushindi.
Alisema licha ya kikosi chake kwa kiasi kikubwa kusheheni nyota chipukizi wengi wao wakiwa wanafunzi, ni wenye uwezo mkubwa.
Katika hatua nyingine, Benki ya Posta Tanzania (TPB), jana ilitoa kitita sha sh mil. 3 kwa timu hiyo kama kuwaongezea ari wachezaji wa timu hiyo.