HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 20 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Kabumba: Twiga wametuhuzunisha


na Abdallah Menssah

 

KATIBU wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (DWFA), Stephania Kabumba, ameelezea kuhuzunishwa na kipigo cha Twiga Stars cha bao 1-0 ilichopata Jumamosi iliyopita kutoka kwa Ethiopia.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi, Kabumba alisema kuwa, si tu kuwa kipigo hicho kimewahuzuzisha viongozi wa DWFA, bali pia kimewafadhaisha makocha wa timu hiyo, kutokana na kuwa, wachezaji walikuwa wakionesha mwelekeo mzuri katika mechi za ligi.

Kabumba alisema kuwa, kinachowafanya washindwe kuelewa zaidi, ni kuona wachezaji wao wakiwa katika hali ya ulegevu kupita kiasi, ambako alidai kuwa, walioonesha kucheza kwa kiwango cha kuridhisha walikuwa ni Kipa Fatma Omary na beki Sofia Mwasikili.

“Hata hivyo, tutakaa na wachezaji wetu na kuulizana nao vizuri, kuwa ni jambo gani liliwapata ghafla siku ile hata wakawa katika hali ile inayofadhaisha na ambayo hakuna aliyeitegemea,” alisema Kabumba.

Akizungumzia kauli ya Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniphace Mkwasa, aliyodai kuwa kiwango cha wachezaji wake kimefika kikomo, Kabumba alisema kuwa, anaamini kocha huyo alighadhabishwa na matokeo hayo.

Hata hivyo, katibu huyo alisema, bado anaamni kuwa, kikosi hicho kina nafasi ya kufanya vema katika michuano mingine, iwapo tu maandalizi mazuri zaidi yatafanyika.

Kutokana na matokeo ya Jumamosi, Ethiopia imefanikiwa kutinga fainali za Mataifa ya Afrika (AWC), kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.



juu