HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 30 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Idadi ya wagonjwa wa kisukari yaongezeka


na Stella Ibengwe, Shinyanga

 

IDADI ya wagonjwa wa kisukari imeongezeka mkoani Shinyanga kutokana na wakazi wake kula vyakula vingi vya wanga na kutofanya mazoezi.

Taarifa hiyo ilitolewa na Muuguzi Mkuu kitengo cha magonjwa ya kisukari katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Ruth Nkola, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wako katika mafunzo ya vitendo ya siku nne ya namna ya kuandika habari za afya mkoani humo.

Alisema kuwa ugonjwa wa kisukari ni hali ya sukari mwilini kuzidi kiwango cha kawaida na kwamba katika hali ya kawaida ya afya, mtu kabla hajala anatakiwa awe na sukari kiasi cha 4-6.1 (MM1/2) kwa kipimo cha MM ½ na kipimo cha MM 4-6.5.

Ikiwa mtu amekula zaidi ya hapo, atatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa kitabibu.

Akizungumzia takwimu za ongezeko la wagonjwa wa kisukari mkoa wa Shinyanga, Nkola alisema kuwa tangu mwaka 2003 kilipoanzishwa kitengo cha wagonjwa hao hospitalini hapo mpaka kufikia mwaka huu, idadi ya wagonjwa ni 708.

Nkola alibainisha kuwa ongezeko hilo lilizidi kuanzia mwaka jana ambapo wagonjwa wanne wamekuwa wakiripoti kliniki ya wagonjwa wa kisukari kila mwezi ikilinganishwa na mwaka 2003 walipokuwa wakikaa miezi miwili hadi mitatu bila kupokea mgonjwa.

Aliongeza kuwa ugonjwa huo unawapata watu wengi kuanzia umri wa miaka 40 na kuendelea ambao huuguwa kisukari aina ya pili kwa kuwa wengi wao hawafanyi mazoezi na tabia ya ulaji wa vyakula bila mpangilio hasa vyenye wanga.

Kisukari aina ya kwanza ambacho huwapata watoto wenye umri wa miaka sita ni hatari zaidi kwa wagonjwa ambao hulazimika kuchoma sindano ya insulini maisha yote kwani ugonjwa huo hauna tiba.



juu