MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye, ametangaza vita dhidi ya watu wanaoweka kambi milimani na kufanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuchoma misitu katika wilaya hiyo.
Agizo hilo alilitoa juzi wakati akizungumza na wakazi wa Kata Masa wiliyani humo alipokuwa akikabidhi madume ya ng’ombe kwa baadhi ya wakazi hao.
Alisema kuna wananchi wamegeuza makazi yao na kuweka kambi milimani wakifanya kazi ya kuchoma miti hovyo na kuharibu mazingira kitendo ambacho kinasababisha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.
“Serikali haijaenda likizo katika hilo nitahakikisha watu wote wanachukulia hatua za kisheria ili tuweze kukomesha uharibifu huo,” alisema Kangoye.
Aliongeza kuwa kumekuwepo na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiharibu mazingira hayo bila kujali kwamba wanaweza kusababisha jangwa na hivyo kuruhusu kuwepo na njaa.
“Nasema hivi dola ipo, serikali ipo hivyo nyie mnaojifanya hamsikia na kuendelea kuchoma misitu hovyo hatutawavumilia,” alisitiza Kangoye.
Aidha, alisema wananchi wamekuwa wakiingiza na kulihusisha suala la uharibufu wa mazingira na siasa kitu ambacho si sahihi.