HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Tendwa ajikoroga


na Stella Mushi

 

MSAJILI wa vyama vya siasa nchini John Tendwa amekanusha kauli aliyopata kuitamka siku za nyuma kuwa atafuta vyama vya siasa ambavyo uhai wake unalegalega.

Mwanzoni mwa mwaka huu wakati akikipa usajili wa kudumu Chama cha Jamii (CCK) Tendwa alikaririwa akisema kuwa wanatarajia kuanza mchakato wa kuhakiki uhai wa vyama vya siasa ili kubaini kama viko hai na vile visivyokidhi malengo kufutiwa usajili.

Hata hivyo jana Tendwa wakati akikipa usajili wa muda Chama cha Ukombozi wa Umma alidai kuwa alikaririwa vibaya na baadhi ya vyombo vya habari na kwamba kauli yake haikueleweka na kufafanua kwamba alikuwa na maana kuwa hivi sasa wapo katika mchakato wa kupanua wigo wa kuvipatia ruzuku vyama hivyo kwa mujibu wa sheria.

“Sasa kwa kutotimiza kwao matakwa ya kisheria maana yake wanatuomba kimya kimya tuwafute na tutawafuta maana vipo vyama ambavyo havipo pande zote za muungano, kwa maana ya kuwa na wanachama bara bila Zanzibar.

“Nawaambia mapema kabisa, tunakuja na tutakagua bara na Zanzibar…kadiri chama kilivyosema kina wanachama sehemu fulani huko huko tutakwenda na kamwe hawatatudanganya, tutawapa taarifa,” aliwahi kukaririwa Tendwa katika gazeti hili toleo la Januari 28 mwaka huu.

Hata hivyo jana katika kile kinachoonekana kujichanganya Tendwa ambaye alianza kueleza idadi ya vyama kwamba ipo 19 venye usajili wa kudumu akasema kuwa kati ya hivyo vyama nane ndivyo vinapokea ruzuku kutokana na kutambulika katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

“Tutabadilisha utaratibu wa kuzungumza na vyama vipya vya siasa ambavyo haviingiliani na vyama vingine ili viweze kupata usajili wa kudumu kama vyama vingine,” Tendwa alikaririwa katika kauli yake mpya na kukana ile ya kwanza.



juu