HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

TAKUKURU yambana ofisa mtendaji aliyekula sh 60,000


na Jumbe Ismailly, Singida

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imempandisha kizimbani aliyekuwa ofisa mtendaji wa kata ya Minyughe, katika halmashauri ya wilaya ya Singida, Abdala Omari Majengo, kwa tuhuma za kutumia shilingi 60,000 mali ya mwajiri wake kwa matumizi yake binafsi.

Afisa mtendaji huyo ambaye kwa hivi sasa amehamishiwa katika kata ya Mungaa, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini Singida.

Mwanasheria wa TAKUKURU mkoani Singida, Boniface Kamwesigile, alidai kwamba Feb 2, 2011 mshtakiwa huyo alighushi risiti yenye namba 618185 ya Feb, mbili mwaka jana kwa lengo la kujipatia shilingi 60,000 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Aidha Mwendesha Mashtaka huyo pia alidai kwamba katika risiti hiyo iliyolenga kumdanganya mwajiri wake, mshtakiwa huyo aliandika kuwa amelipa posho kwa wanamgambo watano na kisha kununua mafuta ya kuendeshea pikipiki ya umma aina ya petroli.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo Novemba 2010 akiwa katika kijiji cha Misake, alitumia madaraka yake vibaya kwa kumfukuza kazi Mwenyekiti wa Kitongoji, Joseph Ipunze Dwash.

Hata hivyo Majengo alikana mashtaka yote yanayokabili na yupo nje baada ya kudhaminiwa na Mhasibu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Abdallah Masudi Babanyikwa hadi Julai 18, mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.



juu