HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Darasa la kwanza kupunguziwa masomo


na Gordon Kalulunga, Mbeya

 

SERIKALI imesema inatarajia kupunguza idadi ya masomo ya darasa la kwanza kutoka saba yanayofundishwa sasa.

Kauli hiyo ya imetolewa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mullugo, alipokuwa akizungumza na wamiliki na wakuu wa shule za sekondari mkoani Mbeya katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Mbeya Day.

Mullugo alisema kwa sasa wako katika mchakato wa kuangalia idadi ya masomo yanayopaswa kupunguzwa.

Alisema wanafunzi wa darasa la kwanza wamekuwa wakitwishwa mzigo mzito kwa kufundishwa masomo saba tofauti na uwezo wao wa kujifunza.

Masomo yanayofundishwa kwa sasa kwa darasa hilo la kwanza ni pamoja na somo la Kiswahili, Kiingereza, Hisabati, Stadi za kazi, Tehama, Haiba na Michezo na somo la Sayansi.

Wakati huo huo, Naibu huyo Waziri ametoa agizo kwa maafisa elimu wa wilaya na mikoa yote nchini kuzifunga shule zote ambazo hazina usajili pamoja na vituo vya elimu vya uchachoroni na kwamba ni marufuku kudahili wanafunzi ifikapo Januari 2013.

Mbali na hayo, Mullugo pia alizungumzia siasa zinavyoathiri wanafunzi hali kadhalika suala zima la mavazi ambalo alisema kuwa maadili ya walimu yameshuka hasa wenye shahada ambao baadhi yao wanavaa milegezo.

Alisema walimu hao wanapaswa kuonywa na wakikaidi watafukuzwa kazi.



juu