MSTAHIKI wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi, kuna wakati aliwahi kusema baadhi ya wabunge wa mkoa huo, wanafikiri kwa kutumia makalio.
Haikuwa lugha nzuri, lakini nadhani alitaka kusema wabunge hao wanafanya au kuzungumza mambo bila kutumia akili.
Juzi Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na Mkuu wa Mkoa, Stella Manyanya, alitoa hoja isiyofaa bungeni.
Sitaki kutumia lugha ya Masaburi, lakini binafsi nahoji utimamu wa akili wa mbunge na mkuu wa mkoa huyo wa Rukwa.
Nirejee kidogo kile alichokisema Manyanya wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Kwanza mkuu wa mkoa huyo alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinahusika kuchochea mgomo wa madaktari na pia kinahusika na kumteka, kumpiga na kumtesa mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Nchini, Dk. Steven Ulimboka.
Pili alienda mbali na kumlaumu Dk. Ulimboka kwa kuwa kinara wa mgomo huo na kwamba Mungu amemnusuru kwani angekuwa Adolf Hitler wa Tanzania.
Kwa akili ya kawaida, haingii akilini kwamba CHADEMA ndiyo waliochochea mgomo na ndiyo waliohusika kumteka na kumpiga kiongozi wa mgomo huo.
Swali la kujiuliza ni kwamba kama CHADEMA ndiyo waliochochea mgomo na kufanikiwa, sasa iweje tena haohao wamteke Ulimboka aliyewasaidia kufanikisha mgomo huo na kuwa shujaa wao? Ili iweje?
Lakini kibaya zaidi mbunge na mkuu wa mkoa huyo ametoa kauli hiyo huku akijua fika kwamba tayari serikali anayoiongoza mkoani Rukwa imeshaunda tume kuchunguza tukio hilo.
Baada ya kauli hiyo mkuu huyo wa mkoa aliendelea na kuchafua zaidi hali ya hewa pale aliposema waliomteka Dk. Ulimboka, walivalia magwanda ya CHADEMA.
Baada ya hapo Bunge lilichafuka, kiti cha Spika kilichoongozwa Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba kiliyumba kabisa kuongoza Bunge.
Katika hali isiyo ya kawaida, Mabumba alitumia lugha ya matusi kwa wabunge kama John Mnyika na kutishia kuwafukuza nje ya ukumbi wabunge wote wa kambi ya upinzani. Hii yote ilitokana na kauli chafu ya Manyanya.
Manyanya anamlaumu Dk. Ulimboka kuongoza na kushiriki mgomo huo. Ama kweli nyani haoni kundule.
Niwakumbushe kidogo. Mbunge na mkuu wa mkoa huyo ndiye aliyekuwa mmoja kati ya vinara wa mgomo wa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wakati huo ikiongozwa na Net Group Solution.
Sababu za mgomo huo Manyanya anazijua. Leo anamlaumu na hata kumcheka Dk. Ulimboka.
Ninachokiona mimi, mbunge na mkuu wa mkoa huyo, amelewa madaraka. Ana kila sababu ya kutoa kauli za kujikomba kiasi cha kulamba viatu vya aliyempa ulaji huo.
Na hili ni tatizo la kuteua watendaji kwa kuzingatia kujuana bila kujali uwezo.
Jana wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ikichangia hotuba ya Ofisi ya Rais, iliyowasilishwa na Waziri Celina Kombani, Makamu Mwenyekiti, Paul Rwanji, alizungumzia suala la uteuzi wa watendaji.
Alisema na hapa nanukuu: “Aidha kamati inapendekeza nadharia (concept) ya Peter Principle
(Never promote somebody to his/her highest level of incompetence) kutumika wakati wa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu wa serikali.
“Kamati inakubaliana na nadharia hiyo kwa imani kwamba tunapozungumzia uwezo wa mtu kumudu majukumu yake tusisahau kwamba uwezo huo una ukomo kutokana na uwezo kiakili (IQ), sifa na uzoefu.
“Hivyo mamlaka ikikosea na kumteua mtu kushika madaraka asiyostahili ni wazi kwamba mhusika atashindwa kumudu madaraka aliyopewa.”
Swali langu, uteuzi wa Manyanya ulizingatia nadharia hiyo?