WAPO Watanzania ambao hawajawahi kutibiwa kwenye hospitali za serikali hapa nchini na hawajui kabisa adha wanazopata wagonjwa wasiokuwa na uwezo wanaokwenda kutibiwa na madaktari tunaoshindwa kukaa nao meza moja kumaliza mgomo.
Madaktari wazalendo ili waweze kukidhi mahitaji yao muhimu hawawezi kutulia kwenye hospitali moja, wanahaha huku na kule ili kuhakikisha kuwa wakimaliza kazi za ajira zao walizopangiwa wanakimbilia kwenye hospitali binafsi kujitafutia kipato cha ziada.
Wengine wakimaliza kazi zao za ajira wanakimbilia kwenye hospitali wanazomiliki wenyewe, maduka ya dawa au zahanati za taasisi binafsi yakiwamo madhehebu ya dini ili mradi kila mmoja anafanya jitihada za kupambana na hali ngumu ya maisha yanayoweza kuwatofautisha na kada nyingine.
Wapo madaktari, wauguzi na idara nyingine za tiba wamekimbilia nchi za nje kwenda kufanya kazi huko kwa lengo lile lile la kuhakikisha kuwa wanajiongezea kipato chao na kuondokana na adha ya umasikini inayoikumba kada hiyo ya wasomi lakini wanakosa hamasa ya kazi kutokana na danadana zinazopigwa na serikali huku wakiwashuhudia wanasiasa waliogeuka mabilionea kwenye nchi inayodaiwa kuwa haina kitu.
Kada ya madaktari ni muhimu kwa kuwa inagusa moja kwa moja uhai na maisha ya binadamu, kada ya utabibu haipaswi kuchezewa kabisa tofauti na kada nyingine zinazojihusisha na utoaji wa huduma za kijamii, hii kada ni nyeti kama ambavyo si viongozi wala makabwela ambao hukwepa kwenda kuokoa maisha yao.
Serikali kwa upande wake inatambua kuwa taifa lolote huru haliwezi kuendelea kama wananchi wake wengi ni wagonjwa na wanakufa kwa kukosa matibabu sahihi, wanakufa kwa sababu madaktari wamegoma, wanakufa kwa sababu wauguzi hawawezi kufanya kazi bila madaktari.
Kama nilivyosema kwenye kundi la Watanzania, wapo ambao tangu wazaliwe hawajawahi kufika na kutibiwa kwenye hospitali za makabwela, hospitali za madaktari ambao ili waweze kulipwa posho zao na vitendea kazi bora lazima wagome ili kuishinikiza serikali iwalipe.
Upepo wa mgomo unaoendelea hapa nchini ni hatari kwa mustakabali wa nchi, ni hadithi ya Daudi na Goliath, haiwezekani na haiwezi kuingia akilini kama kundi moja la wanasiasa (wabunge) ambao kwa kuwepo kwao bungeni wanayaona maisha ya uswahilini magumu, yana gharama kubwa na wamekuwa wakiomba kuongezewa posho.
Lakini inakuwa vigumu kuyaingiza mawazo ya madaktari wazalendo kwenye vichwa vya wanasiasa waliopewa mamlaka ya kutunga sheria wawapo bungeni, eti wanafungwa na mahakama na hawawezi kuthubutu kuzungumzia adha zinazogusa mgogoro huo huku serikali ikionekana wazi kutoa ushahidi wake nje ya mahakama wakiangalia sinema ya Daudi na Goliath.
Kibaya na kikubwa kinacholeta tofauti ya maisha kati ya viongozi wa juu serikalini na wabunge wanapougua ni rahisi sana kukimbilia nchi za nje kwenda kutibiwa, hususan nchini India ambako Tanzania imejiweka wazi kuwa nchi hiyo ndio yenye uwezo wa kuokoa maisha ya viongozi wa serikali na si vinginevyo.
Kama hali iko hivyo na wakubwa hawa waliopewa madaraka na wananchi hawaguswi moja kwa moja na mahangaiko makubwa hadi vifo vinavyowakumba wananchi wasiokuwa na hatia waliolazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, waliolazwa Dodoma, waliolazwa Arusha, Mbeya na kwingineko hali hiyo hawaioni.
Laiti viongozi wetu wangekuwa wanaona moja kwa moja huzuni na majonzi yanayowakuta ndugu za wagonjwa waliowapeleka wagonjwa wao hospitalini wakijua wazi kuwa watapona lakini hurudi nyumbani bila ndugu zao huku wakiuziwa majeneza yanayotengenezwa na kuuzwa nje ya milango ya hospitali, Bunge letu linapaswa kubadili hoja na kujikita kwenye hoja nzito ya mgomo.
Laiti viongozi hawa wangejua kuwa migomo hii ya madaktari ni mauti kwa watu maskini, serikali isingekuwa inachukua uamuzi wa haraka wa kuwafukuza au kuwasimamisha kazi madaktari wa vitendo, suluhu ni kutafuta kiini cha matatizo ya msingi ili wananchi wasife.
Ieleweke wazi daktari mwenye njaa hawezi kuwahudumia vizuri wagonjwa na kwa vyovyote hata kama atajing’ang’aniza kufanya kazi ya kutibu ni dhahiri kuwa ataifanya kazi hiyo chini ya kiwango na hiyo ni hatari kubwa kwa maisha ya mgonjwa hasa wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa ya hatari zikiwemo ajali mbaya za barabarani zinazotokea kila kukicha.
Kuna kila sababu ya kuiambia serikali kuwa inapaswa kudharau au kushindwa kutoa fedha za kutosha kwenye sekta nyingine lakini si hii ya afya ambayo ndio tasnia pekee ya tiba inayogusa moja kwa moja uhai wa mtu, wengi mijini na vijijini wanakufa kwa kukosa vifaatiba sahihi.
Ipo haja ya kuangalia pande tatu za uhai wa binadamu, kama serikali ipo inakuwaje mambo haya yatokee tu kwa sababu eti fedha za kulipa posho za madaktari hazipo, malipo ya madaktari kuitwa zamu (Oncall allowance) hakuna wakati madaktari hawa wanaofanya mazoezi ya vitendo wana wakati mgumu ndio wanaokesha na wagonjwa.
Hakika katika sekta ya afya ni kosa kuichezea kada hii ya madaktari wa vitendo kwa kuwa hawa ndio madaktari wanaoandaliwa kushika vitengo nyeti na ndio hao hao wanaokimbilia nchi za nje zikiwamo za kusini mwa Afrika hasa Botswana, Namibia na kwingineko wanakokwenda kutafuta maisha bora.
Ni jambo la kustaajabisha serikali inatumia fedha nyingi kuwasomesha madaktari lakini inashindwa kutumia fedha hizohizo kuwawekea mazingira mazuri ya kazi na kusababisha migomo ya mara kwa mara kuzuka, migomo inayowatia hofu wagonjwa na wengi wanapoteza maisha kwa kukosa matumaini.
Huu si mchezo mzuri unaochezwa kati ya serikali na madaktari, hakika mchezo huo wa kutunishiana misuli unawaumiza zaidi wananchi, wananchi ndio wanaoumia, kukosa tiba sahihi na wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kutibiwa kwa wakati.
Kitendo cha watu hawa kudai haki zao wanazostahili kuzipata kihalali na upande wa pili ambao ni serikali unaposimama na kutumia ubabe badala ya kuweka utaratibu mzuri wa kulipa posho na kuboresha mazingira ya kazi hakuonyeshi kuwagusa viongozi wanaotegemea zaidi kwenda kutibiwa nje ya nchi pale wanapougua.
Umefika wakati wa serikali kuwajali na kutambua mchango unaotolewa na madaktari wazalendo wanaowahudumia kwa wingi wananchi wa kawaida na hakuna kundi linaloweza kujivunia ushindi kwenye mapambano hayo kama watu wanaendelea kufa kwenye hospitali za serikali.
Wale wenye uwezo wanakimbilia kwenye hospitali binafsi na hawa ndugu zangu makabwela ndio waliojazana kwenye hospitali za Temeke, Mwananyamala na Muhimbili na ndio kimbilio la wananchi wengi walioshindwa kutibiwa mikoani na hatua yao ya kuokoa maisha imeelekezwa kwenye Hospitali ya Taifa.
Jibu linaloweza kumaliza mtafaruku huu wa migomo ya madaktari lipo kwa kuwa serikali ipo na kama serikali ipo inatambua fika kuwa ni idadi gani ya kada ya wataalamu wa afya wanatoka vyuoni na kuanza mazoezi yao ya vitendo sambamba na uwepo wa bajeti inayoweza kukidhi ulipaji wa posho na uboreshaji wa vifaatiba.
Kutokuwepo kwa mipango sahihi na madhubuti ndiyo chanzo cha kuifanya migomo hiyo iendelee na hujirudia mara kwa mara, haipimwi kwa uwezo wa waziri mhusika katika wizara hiyo kwa kuwa kila waziri aliyeongoza Wizara ya Afya hukumbana na hali hiyo kinachopaswa kubadilika hapo ni mfumo wa watendaji katika kutatua migomo ya madaktari.
Mawaziri wanaweza kubadilika kila wakati lakini ni vigumu kuubadili mfumo wa watendaji katika wizara wanaochangia kuwepo kwa migomo hiyo wanajua kwa nini madaktari wanacheleweshewa malipo yao, wanajua fika athari zinazoweza kujitokeza endapo wataalamu hao wanapogoma, hayo yote yanapotokea wanaoumia ni wananchi.
Sekta ya afya ni nyeti kama nilivyosema awali lakini isiwe kikwazo kwa kuwa viongozi wa juu serikalini, wabunge na wenye uwezo wanapougua wanakimbilia nchi za nje, ‘Mnyonge mnyongeni ‘lakini haki yake mpeni vinginevyo mgomo huu hauwatesi madaktari kwani ndio hao hao wanaoendelea kufanya kazi kwenye hospitali binafsi zinazotoza fedha nyingi.