HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Potelea mbali, nani anajali!

Absalom Kibanda

 

HILI ni taifa tajiri kiraslimali ambalo kwa bahati mbaya, ukwasi uliojaa kitakwimu umeshindwa kulifanya liondokane na laana ya unyonge na umaskini ambayo imelitafuna kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Nimelazimika kuianza makala hii kwa maneno hayo si kwa sababu nyingine bali kwa sababu ya kuyaangalia na kuyatafakari matukio kadha wa kadha yanayolikumba taifa letu katika siku za hivi karibuni ambayo sina shaka hata kidogo kwamba, iwapo ungejengwa utamaduni wa kuzitumia vyema raslimali tulizonazo huenda tusingefika hapa tulipo leo.

Utajiri huo mkubwa wa kiraslimali wa taifa hili ndiyo uliosababisha miaka mitano iliyopita, mwanasiasa kijana na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe azindue kile Azimio la Songea lililokuwa na makusudi ya kulinda kuboresha matumizi endelevu ya raslimali za taifa.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba, azimio la Zitto lilipata upinzani wa kwanza mkubwa ndani ya mioyo ya viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya kupokewa kwa namna ya kufumbiwa macho na kupuuzwa na makada na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wa serikali yake.

Hulka za kimazoea zilizogeuka na kuwa utamaduni wa kudumu wa viongozi wa umma na wale wa serikali katika kukwepa kutimiza wajibu wao ipasavyo na kwa umakini sambamba na tabia za kudumu za wananchi kuyapuuza masuala ya msingi na kushabikia masuala ya hovyo hovyo ndizo ambazo zimetoa mwanya wa kupwaya kwetu kama taifa.

Ni wazi kwamba kwa hali tuliyofikia leo, hakuna aliye na jeuri ya kumnyoshea kidole mwenzake kwa kiwango cha kumfanya anayefanya hivyo akaonekana mkamilifu na mtu anayetimiza wajibu wake ipasavyo kwa viwango vya Yesu aliyehubiri habari za kibanzi na boriti.

Wakati tukiwalaumu Kikwete na jeshi la viongozi wenzake serikalini kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kiwango cha kupachikwa kila aina ya majina mabaya, nyuma ya pazia, wananchi wanaotupa lawama hizo wenyewe wamekuzwa na kukua katika mazingira ya uvivu, kuchukia kazi na kufikiria maisha ya mkato kwa Kiswahili cha mtaani ‘mishe- mishe’

Katika mazingira ya namna hiyo, si ajabu hata kidogo kuwaona viongozi wakitumia mamilioni ya shilingi katika kununua uongozi wa taifa hili, ukianzia na ngazi ya urais hadi uenyekiti wa mtaa kwa kiwango cha kujiuliza ni nini kilicho nyuma ya fursa wanazozipigania kwa kiwango cha kuwa tayari kutoa uhai wa mtu au watu wengine!

Siyo jambo la kushangaza hata kidogo kwamba, watu walio nyuma ya unyama aliofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka msingi wake ni hofu ya watu kupoteza madaraka waliyonayo kutokana na mgomo wa madaktari.

Hivi katika nchi ambayo dhamana ya madaraka ya umma imegeuka na kuwa mtaji wa ulaji na kuchuma mali, ni kiongozi wa namna gani ambaye yuko tayari kufikwa kirahisi na kile kilichowafika aliyekuwa Waziri wa Afya, Haji Mponda na Blandina Nyoni ambao walipoteza fursa za kuongoza kwa sababu ya akina Ulimboka?

Kwa watu wenye hulka za namna hiyo na ambao kimsingi wameshindwa kutimiza ipasavyo wajibu wao ikiwa ni pamoja na kusahau kwamba uongozi ni dhamana ya kazi, kinachoweza kikawajia haraka haraka akilini kwa kiwango cha kuwatia hofu ni matukio ya hivi karibuni ya kuanguka kwa tawala kadha wa kadha za Kiafrika ambazo kwa miaka mingi zimekuwa madarakani kwa hila.

Nitakuwa mtu wa mwisho kupigwa na butwaa iwapo uchunguzi utakaofanywa mbele ya safari na tume huru, utakuja na matokeo ambayo kwa mara ya kwanza utazalisha watuhumiwa wa mwanzo wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu dhidi ya binadamu iliyoko The Hague, Uholanzi.

Tunaweza tukakuna vichwa na kuzusha ubishi usio na mwisho wa kuhoji ni nani anasema kweli au yuko sahihi kati ya serikali na madaktari wakati tunapoyaangalia matukio ya mfululizo wa migomo ambayo yamegharimu maisha ya wananchi wengi walio.

Ingawa ni ukweli kwamba hata katika hatua tuliyopo leo tumeshayasikia majibu ya kusononesha, yenye ukakasi na maudhi kutoka pande mbalimbali zinazokinzana, bado ukweli unaweza ukajionyesha dhahiri kwamba kumekuwa na hali ya kila mmoja kushindwa kutimiza ipasavyo wajibu wake ipasavyo.

Uduni wa mazingira ya kazi katika hospitali nyingi za umma unaoambatana na ukosefu wa vitendea kazi, majengo na ofisi zilizochakaa kwa kukosa matengenezo kwa kiwango cha kuhatarisha afya za madaktari, manesi na wagonjwa ni moja ya sababu ambazo zimegeuka kuwa ajenda za mgomo usiokoma wa madaktari.

Yumkini hali hii ya kukatisha tamaa inayoweza ikavumilika iwapo tu viongozi wangeonyesha na kuonekana wakijali na kuisikitikia ni moja ya mambo ambayo yamechochea hulka za uasi za kibinadamu miongoni mwa madaktari ambao baadhi yao wamepata fursa kusoma au kutembelea na kujionea wenyewe mazingira yalivyo katika hospitali nyingine binafsi ndani ya nchi au zile za umma huko ughaibuni.

Kama hiyo haitoshi, machungu ya kazi kwa madaktari yanakuwa makubwa kwao wanapowaona viongozi wa kisiasa na kiserikali ambao walipaswa kuwa watu wa mwanzo kuyajua na kuyafanyia kazi machungu yanayowakabili wakiwa ni watu wa mwanzo kuwapuuza au kutowajali kwa namna tofauti.

Hivi ni kitu gani kinatokea katika fikra za daktari mwenye elimu nzuri aliye wodini anapowaona viongozi wenye wajibu wa kuboresha mazingira yake ya kazi akizipa kisogo hospitali na kutowajali wao (madaktari) na wakati huo huo wao wenyewe (viongozi hao) na familia zao wakitibiwa nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Kwa daktari ambaye anajua ukubwa wa gharama za uchunguzi wa afya na matibabu katika hospitali za Afrika Kusini, India, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Marekani na kwingine ambako viongozi na familia zao huenda, ni jambo lisiloingia akilini kuona akipuuzwa na watu hao hao ambao kimsingi walipaswa watambua thamani ya kazi au wito wake kwa vitendo.

Si ajabu hata kidogo basi, kuwaona madaktari wakijikuta wakilazimika kufumba macho na kufikia hatua hata ya kuwasahau mamia kama si maelfu ya wagonjwa maskini wanaoteseka na kufa kwa sababu ya migomo yao.

Katika mazingira ambayo madaktari wanalazimika kuiacha taaluma adhimu waliyosomea na kuingia katika siasa kwa namna walivyofanya kina Profesa David Mwakyusa, Hamisi Kigwangalah, Faustine Ndugulile na Dk. Lucy Nkya kama njia ya kumudu maisha na kutimiza ndoto zao, ni rahisi kabisa kwao kufikiria mgomo kama njia muafaka ya kuwalazimisha viongozi wa umma kufikiri na kuchukua maamuzi sahihi.

Ingawa ni jambo rahisi na pengine sahihi kwa viwango fulani, kuwalaumu madaktari kwa kutojali maisha ya wagonjwa wanaowatelekeza kila wanapogoma, tunapaswa pia kuwa wepesi kuwanyoshea vidole viongozi wanaotuongoza kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa maana ya kujua vipaumbele.

Haitoshi kwa Rais kutamka kirahisi tu kwamba, serikali haiwezi kamwe kumlipa daktari mshahara wa shilingi 3,000,000/- wakati huo huo yeye mwenyewe akiwa hayuko tayari kujifunga mkanda na kupunguza wingi wa safari za nje ya nchi na matumizi mengine ya anasa ambayo serikali anayoiongoza inaonekana kuendekeza.

Katika mazingira ambayo serikali inaonekana dhahiri kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo na kupoteza mabilioni ya fedha kwa ufisadi na kwa kukopa fedha nyingi tena kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo hayalengi kuboresha maslahi ya watu wa aina ya madaktari, ni rahisi sana kwa makundi ya kijamii au kiuchumi kuchukua maamuzi yanayoumiza sana kama yale yanayofanywa leo na madaktari.

Hivi Rais Kikwete na viongozi wenzake serikalini wanafikiri nini kinatokea katika vichwa vya madaktari wakati wanapolisikiliza Bunge na kumsikia Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, akihoji ni kwa kazi gani hasa deni la taifa limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 22 mwezi Mei mwaka huu kutoka kiwango cha shilingi trilioni 10.5 mwaka 2009/2010?

Ni kwa nini madaktari wasigome, walimu wasilalamike na polisi wasiendelee kusononeka chini chini (tuombe sana Mungu wasishawishike kugoma) wanapomsikia mchumi, Dk. Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, akisoma ripoti ya utafiti inayoonyesha kwamba serikali inapoteza kiasi cha shilingi trilioni 1.7 kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi na kutokana na vitendo vya utoroshaji wa fedha na mali nje ya nchi?

Tungekuwa na taifa la viongozi wanaojali na wenye uchungu wa kweli na nchi hii, tungewaona wakichukua hatua za wazi na dhahiri za kupunguza hujuma dhidi ya raslimali zetu, tungewasikia wakipunguza matumizi makubwa ya anasa yanayojumuisha safari za nje zisizo na tija, matumizi ghali ya magari ya kifahari ikiwa ni pamoja na kukomesha kabisa misamaha hewa ya kodi.

Siku taifa hili litakapopata viongozi shupavu wanaojali na kutambua wajibu wao huko tuendako, wenye uwezo wa kuwa na maono, fikra na maamuzi sahihi na magumu, basi huo ndiyo utakuwa ukomo wa udhaifu wa viongozi tulionao, mwisho wa uzembe katika taasisi zetu na hakika tutakuwa tumefikia tamati ya upuuzi wa leo wa chama kilicho madarakani. Tupambane tufike huko.



juu