HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Madaktari, serikali acheni utoto

Ruhazi Ruhazi

 

NINACHOKIONA katika hili sakata linaloendelea la mgomo wa madaktari ambalo linaingia katika wiki ya pili ni utoto na kuendeleza hulka ya kibinadamu ya kutokubali kukosa na baadaye kuomba radhi.

Ni wanaadamu wachache sana wenye hulka na tabia ya kukiri makosa hadharani na kukubali kuomba radhi kwa kosa hilo kama jinsi ambavyo inajidhihirisha hivi sasa.

Hulka hii ya kibinadamu tunafundishwa katika vitabu vitukufu vya dini kwamba ilianza tangu kwa baba yetu Adam na mkewe, Hawa au Eva, ambapo walipomkosea Mungu Muumba wao hakuna aliyekubali kuomba radhi badala yake kila mmoja akabisha na kutumia mtindo wa kujitetea kwa kumtupia lawama mwingine.

Maandiko yanatumbia kuwa baada ya Mungu kumuita na kumuuliza “Adam kwa nini umekula tunda nililokukataza?”, baba yetu Adam alijibu kwa kusema “Si mimi, ni huyu mwanamke uliyenipa” akimaanisha Hawa.

Hawa naye alipoulizwa na Mungu swali lile lile la kwa nini umekula tunda nililokukatazeni badala ya kumuanguki Mungu na kumuomba msamaha lakini naye akajaribu kujitetea kwa staili ile ile aliyofanya mumewe Adam kwa kusema ‘Si mimi bali ni huyu nyoka uliyemtuma,” akimaanisha shetani aliyewadanganya kuwa wakila tunda lile watakuwa na akili nyingi na kuishi milele.

Tunazidi kuambiwa na maandiko hayo matukufu kuwa majibu hayo ya kiburi ndiyo yaliyomuudhi Mwenyezi Mungu naye akaamua kuwatimua kutoka peponi na kuwatupa humu duniani huku akimuahidi Adam kula kwa jasho lake na Hawa kuzaa kwa uchungu, wakati nyoka akitajwa kuwa adui yao na pindi watakapokutana naye atawagonga katika visigino nao wakimuwahi wamuue kwa kumpiga kwenye kichwa chake.

Kwa hakika mfano huu unaotoka kwenye maandiko matukufu ya vitabu vya Mwenyezi Mungu, hauna tofauti hata kidogo na jinsi ambavyo suala zima la mgomo lilivyo ambalo kwa nyakati tofauti tumewashuhudia madktari wakiitupia lawama serikali na serikali nayo kwa upande wake ikiwatupia lawama madaktari.

Sote tunafahamu kuwa pande mbili hizi kwa muda mrefu zilikuwa kwenye mazungumzo, tangu ulipomalizika mgomo wa kwanza wa madaktari uliosababisha vifo vya wananchi masikini wa nchi hii wasio na hatia, uliofanyika Februari mwaka huu.

Binafsi kama nilivyoandika Muarobaini wa wiki iliyopita wakati mgomo huu ulipokuwa katika siku za kwanza ni kwamba ninaupinga kwa nguvu zote au niseme siwaungi mkono hata kidogo madaktari katika mgomo wao huu ambao unasababisha wananchi wengi wanyonge kufa kila uchao kwa kutotibiwa.

Hata hivyo lazima niseme katika hili serikali inafanya utoto kwa sababu kila kiongozi wa serikali hata hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ilijikita kuzungumzia zaidi suala la madai ya mshahara tu jambo linaloonekana ni kutka kuwaaminisha wananchi kwamba madaktari wetu wamedhamiria kuwaua wananchi kwa kudai maisha mazuri.

Swali ni je, hilo la mshahara ndilo pekee wanalodai madaktari au kuna mengine wanayodai? Na je, ni lipi kati ya hayo ndilo linaloweza kuchukuliwa kama hoja kuu katika madai yao na je, ni kweli serikali imetatua mambo saba kati ya 10 waliyokuwa wakiyataka madaktari kama alivyosema Rais Kikwete?

Madaktari bingwa nao walivunja ukimya na kusema ukweli unapotoshwa sana katika mgomo wa madaktari na kwamba kwa kuwa ukweli unapotoshwa waliitaka serikali kuwarudisha kazini madaktari wote waliogoma vinginevyo nao watagoma kwa sababu mzigo wa kuwahudumia wananchi utabaki mikononi mwao na pia wanaamini wananchi wengi watakufa kwa kukosa huduma ya madaktari.

Kwa kuwa serikali haikutii madaktari bingwa nao wameamua kugoma, hali inayoongeza madhara kwa wananchi na pengine tayari kuna ongezeko la vifo vya wananchi wanyonge, narudia tena kwamba viongozi wa serikali wanalichukulia hili kwa uzito mdogo kwa sababu hakuna kiongozi hata mmoja kati ya wale wakuu wala familia zao anayetegemea kutibiwa katika hospitali zetu.

Ukisikiliza madai haya ya madaktari bingwa yanafanana na kile walichokisema madaktari na ukiiangalia hotuba ya Rais Kikwete na mawaziri waliozitoa kwa nyakati tofauti utagundua kwamba walipaswa kufikia muafaka kwa mazungumzo tu na si kwa mgomo uliopo.

Rais Kikwete alituambia kuwa kati ya Aprili 10, 2012 na Mei 30, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari na katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa, ambayo ni 1. Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara. 2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.

3. Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara. 4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara. 5. Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari. 6. Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,000 kwa mwezi.

7. Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya. 8. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. 9. Viongozi wa kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje. 10. Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini. 11. Huduma za afya ziboreshwe nchini na 12. Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.

Wakati serikali ikisema kuwa nusu ya madai yao yameshafanyiwa kazi madkatari kwa upande wao wanasema kuwa hakuna hata moja lililofanyiwa kazi na kwamba wanao ushahidi wa kimaandishi na kwamba wanadhani umefika mahali wanadhani ukweli huo uwekwe hadharani, ili wananchi wajionee ukweli.

Ninajiuliza kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi, aliyoitoa tarehe 30 Juni, 2012, kwamba serikali haitaweza kuwalipa madaktari nyongeza ya mishahara wanayoitaka na wasiotaka kufanya kazi waache na kwenda huko wanakodhani watalipwa vizuri, pia nikichambua kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni kwamba “Liwalo na Liwe” na baadaye akaliarifu bunge kwamba katika kukabiliana na mgomo huu serikali imewaagiza madaktari kutoka nje ya nchi na kwamba imeshawatengea sh bilioni 200.

Hapo tunapata swali kwamba fedha hizi nyingi zitatoka katika fungu gani la matumizi? Pia iwapo fedha hizi zipo ni kwa nini zitumike sasa kwa ajili ya kuwaagiza madaktari wa dharura watakaokuja kutoka nje ya nchi? Kwa nini hazikutumika kuboresha mazingira bora waliyokuwa wakidai madaktari na serikali ikawaambia madaktari na wananchi kwa ujumla kwamba huu ndio mwisho wa uwezo wetu wa kuboresha?

Hivi huu ujio wa madaktari hawa wa dharura utakuwa ni ufumbuzi wa kudumu na kuleta madaktari kutoka nje wakati hatuna vifaa ni faida au hasara kwa wananchi na taifa kwa ujumla? Ukosefu wa vifaa tiba bora vilivyokuwa vikililiwa na madaktari wetu mpaka wakaamua kugoma utakuwa umemalizika?.

Jumuiya ya madaktari nchini kupitia kwa Katibu Mkuu wake Dk. Edwin Chitage wameweka msimamo wao wakiitaka serikali kuwaleta haraka madaktari kutoka nje huku akisisitiza kwamba hawapo tayari kurejea kazini.

Naamini kwamba hili ndilo lililowasukuma madaktari bingwa nao kutangaza mgomo kupitia kwa Katibu wao, Dk. Catherine Mng’ong’o ambaye alisema wanaungana na madaktari kugoma kwamba nao sasa wanaanza rasmi mgomo waliouanza mwishoni mwa wiki iliyopita huku wakisisitiza kuungana kwa mabingwa wa hospitali za Muhimbili, MOU, MUHAS na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kama ni kufukuzwa kazi na serikali basi na ianze na wao.

Dk. Catherine alisema kuwa wamesukumwa pia na kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Steven Ulimboka ambaye alitekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya, aking’olewa meno, kucha, kuvunjwa mbavu, mikono na kutekelezwa kabla ya kuokototwa na msamaria mwema aliyewezesha kufikishwa Hospitali ya taifa Muhimbili na ukosefu wa vifaa vya kutosha kulazimisha ahamishiwe nchini Afrika ya Kusini kwa vipimo na matibabu zaidi.

Kwa hakika hiki kinachofanyika katika mgomo huu ni kama mchezo wa watoto, lakini nasikitika kwamba viongozi wa juu wa serikali yetu wanajitia upofu wa kutoona athari iliyo mbele yetu, wananchi wanazidi kutengenezewa vifo kwa migomo, walianza kugoma madaktari, sasa wanaungwa mkono na madaktari bingwa, tusipopata ufumbuzi wa haraka huenda kesho wakagoma pia wauguzi, nini kitakachofuata baada ya hapo?



juu