HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Kiti cha Spika utata mtupu

Edson Kamukara

 

NI ukweli ambao wachache hawapendi kuusikia lakini nitajificha kwenye kalamu yangu niusema sina jinsi. Kiti cha Spika wa Bunge kina udhaifu mkubwa kwenye kutoa uamuzi baina ya wabunge wa chama tawala na wapinzani.

Nalisema hili bila woga na ndiyo maana sijifichi mbali na kalamu yangu kwani hahihitaji mtu kuwa na shahada ya chuo kikuu ndipo utambue kuwa Spika Anne Makinda, Naibu wake, Job Ndugai na wenyeviti Jenister Mhagama na Sylvester Mabumba wanapwaya kimaamuzi kwa kuegemea kukilinda chama chao cha CCM.

Tulikwisha kuandika juu ya hili muda mrefu na wahusika wakajitetea na hata wengine kutupigia simu za kututisha, lakini kwa vile kazi yetu ni kuonya basi leo narudia kusema kuwa kiti cha Spika ni utata mtupu, hakijapata mrithi makini tangu alipoondolewa Samuel Sitta kimizengwe.

Sitajielekeza kwenye mifano ya mbali bali nirejee matukio machache ya hivi karibuni kwenye mkutano wa Bunge unaoendelea. Ni dhahiri kuwa CCM wamejipanga kimkakati kukifanya chombo hicho kama jukwaa la kisiasa kupigana vijembe na wapinzani baada ya kugalagazwa huko nje.

Tulishuhudia wakati wa kujadili bajeti ya serikali ya mwaka 2012/2013, baadhi ya wabunge wengi wa CCM akiwemo na mweka hazina wao, Mwigulu Mchemba, wakiwatukana wapinzani matusi ya kila aina hadi kufikia hatua ya kuishika hotuba ya maoni yao na kuitupa chini lakini kila ulipoombwa mwongozo wa kiti, wahusika walifumba macho na masikio.

Wako kina John Komba, Livingstone Lusinde na wengineo wa CCM walidai wabunge wa CHADEMA ni vichaa wapimwe akili, lakini kiti cha Spika kwa tafsri yake hilo si tusi ila wapinzani maneno yao ndiyo matusi.

Kesho yake, wakati akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alipoanza kutaja kuwa rais ni dhaifu hata kabla hajafafanua, uliombwa mwongozo na kumlazimisha afute kauli yake na mwishowe alitolewa nje.

Tumemwona Mnyika kwa siku tatu mfululizo akijaribu kuomba mwongozo wa Spika akitaka suala la mgomo wa madaktari lijadiliwe bungeni, lakini wenye serikali yao dhaifu hawataki kuumbuka, hivyo akadhalilishwa kwa kukalishwa chini mambo yakasonga.

Hilo tukafunga macho likapita tukajua Ndugai alipitiwa na pepe mchafu. Ijumaa iliyopita wabunge wa upinzani Felix Mkosamali, Moses Machali na John Mnyika, waliomba miongozo wakihoji matusi ya mbunge wa CCM aliyewatukana wabunge vijana na kutaka afute kauli.

Kama ilivyokuwa kwa Ndugai, Spika Makinda naye alitia pamba masikioni, akafumba macho na kujifanya kichwa ngumu, akawalazimisha wabunge hao kuketi chini, kisha akawasindikiza na maneno ya kuwadhalilisha.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, eti wabunge wa upinzani wanaomba mwongozo kwa lengo la kutaka wananchi wawaone wanavyojua kupoteza muda, na kwamba vyombo vina habari vinakimbilia kuwaandika huku vikiponda kiti kuwa kinapendelea upande wa CCM.

Binafsi napenda kwanza nimsamehe Spika Makinda kwa matusi aliyotutukana wanahabari katika harakati hizo za kutaka kukwepa ukweli wa kiti chake kutotenda haki. Ushauri wangu kwake na wasaidizi wake ni kuwataka watambua kuwa ubunge hausomewi ila sisi tunatumikia taaluma tuliyoisotea darasani.

Juzi jioni, mwenyekiti wa Bunge, Mabumba naye aliendeleza wimbi lile lile la kuonesha udhaifu wa kiti cha Spika, pale aliposhindwa kuwakemea Waziri Mary Nagu, na wabunge Stella Manyanya na Nchemba, waliyotoa kauli za uongo bungeni kuwa CHADEMA ndio wanachochea mgomo wa madaktari.

Kwa udhaifu aliouonesha Mabumba nadhani hata watoto wa chekechea walimcheka, alivyomtoa nje Machali na kuacha kuwabana Manyanya na Nchemba watusaidie kuthibitisha uchochezi wa CHADEMA kwenye mgomo wa madaktari.

Nimesema kuwa leo sina haja ya kuzunguka, hivyo Bunge letu kama litaendelea kuendeshwa kwa misingi hii ya ‘saidia serikali ya CCM isianguke’ kwa kupuuzia hoja za wabunge wa upinzani na kuwapa nafasi wale wanaotukana ndio waonekane kwa umma, tutarajie kuona jambo ambalo halijawahi kutokea tangu uhuru likitokea bungeni.

Chimbuko lake litakuwa ni wabunge wa CCM wanaowazidi nguvu Spika na wasaidizi wake, wakidhani wanaisaidia serikali yao kumbe wanaisindikiza kwenye anguko. Yetu nayawe macho kwenye upuuzi huu unaofumbiwa macho bungeni, maana sasa Watanzania wanaelewa.



edkamukara@yahoo.com/ 0788452350/ 071471715
juu