“BINADAMU wanapotendewa mabaya huyaandika kwenye marumaru; wanapotendewa wema, huandika kwenye mchanga.” Maneno haya yanayotoka katika kitabu cha Historia ya Mfalme Richard III, kilichoandikwa na Mtakatifu Thomas More aliyetangazwa mtakatifu na Baba Mtakatifu Pio IX mwaka 1935.
Maneno hayo yananipeleka hadi kwa Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani ‘Profesa Maji Marefu’ ambaye binafsi, naona alikuwa na hoja nzuri kuhusu mkasa uliomkumba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, lakini akaileta kwa njia mbaya na hivyo, kuua hadhi ya hoja yake yote.
Akizungumza katika moja ya vikao vya mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma hivi karibuni, Profesa Maji Marefu, alisahau kidogo hoja iliyokuwa mezani (bungeni) akaamua kutoa hisia zake dhidi ya mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.
Akaliambia Bunge kuwa, Dk. Ulimboka amestahili kipigo alichopata kutoka kwa watu waliomteka, kumtesa, kumpiga na hata kumjeruhi kwa kadiri ya kutisha kwa kuwa amekuwa akichochea na kuwaongoza madaktari wenzake kugoma na kusababisha vifo na adha kwa wagonjwa hivyo, alistahili ili naye ajue mateso wayapatayo wengine.
Kabla hajakamilisha kusema alichokusudia, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimzuia na kumtaka ajikite katika hoja iliyo mezani maana suala la mgomo wa madaktari lipo mahakamani. Siku iliyofuata, Maji Marefu alizungumza na waandishi wa habari na kukaririwa akisema, alinukuliwa vibaya na badala yake, akamsifia Dk. Ulimboka na kumpa pole nyingi.
Kimsingi, kuomba radhi ni jambo jema maana si utamaduni wa Waafrika na hasa Watanzania, kushangilia kifo cha mtu au mateso hasa mauti yanapomkumba mtu katika hali au mazingira ambayo hayakuwa ya kutenda uhalifu.
Katika makala hii, nitajaribu kusema nilichoamini kwamba ndicho Profesa Maji Marefu alichotaka kukisema, lakini ‘akakosea njia’ kuonesha mwelekeo wa kushangilia kitendo cha Dk. Ulimboka kufanyiwa unyama na hata kutelekezwa katika msitu wa pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Ninachokiona kwa Maji Marefu, ni kama vile alitaka japo kwa shingo upande, kuuambia umma kuwa, maumivu anayoyapata sasa Dk. Ulimboka, yatamfanya ahisi uhalisia wa maumivu, mateso na hata mauti yanayowakumba wagonjwa kutokana na juhudi zake za kuchochea mgomo wa madaktari ili wasiwatibu wagonjwa nchini.
Kwa mang’amuzi yangu, naona Maji Marefu alikuwa na mwelekeo wa kuwaambia jambo Watanzania hasa kutokana na wingu lililotanda la akina nani walimteka na walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari maana linazidi kuchanganya vichwa vya wengi ikiwa ni pamoja na kuwapotezea mwelekeo kiasi cha kusahau adha wanayoipata wagonjwa waliogomewa kupewa matibabu na madaktari.
Hii imesababisha kuibuka hoja za kutabiri na kupapasa papasa katika kumuonea huruma na bahati mbaya, hilo limesasabisha kuanza “kupakana uchawi”. Hilo, linawahusisha baadhi ya watu na baadhi ya vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi na wengine wakihukumu kuwa, serikali ina mkono wake katika tukio hilo.
Upo uvumi kwamba baadhi ya watu au vikundi vya ndani au nje ya nchi, wanawapa baadhi ya madaktari fedha, ili wahamasishe wenzao kugoma wakilenga kuifanya nchi isitawalike.
Tunaposamehe kauli ya Profesa Maji Marefu na hasa tunapokumbuka mashambulizi aliyofanyiwa Dk. Ulimboka, tumtafute mchawi tukikumbuka kuwa, kama kweli kipo kikundi ”kinachomwaga mapesa” kufadhili na kuchochea mgomo wa madaktari, basi hapo hapo panaweza kujitokeza uwezekano mkubwa wa madaktari hao kudhulumiana wenyewe kwa wenyewe au kuwapo dalili za kufichuana kwamba nani anafanya nini akisaidiwa na nani na kwa njia ipi.
Kwa msingi huo, ninajawa shaka kuwa huenda tukio hilo limefanywa na wanaodaiwa kutoa pesa hizo kwa sababu zao, au limefanywa na watu ndani ya makundi yao ili wazifaidi hizo pesa au wafiche jambo.
Kwa mang’amuzi yangu, kama kuna mgawo haukwenda sawa, basi madaktari wenzake hasa vinara wa mgomo wamegeukana na kumdhuru, au waliwaajiri au kutuma wawakilishi kulipiza kisasi au “kumzima” asitoe siri huku wakiamini kuwa, ”zigo la lawama” litatupwa kwa wengine maana mhusika alishajijengea mazingira yasiyoeleweka kwa kusababisha madhara kwa jamii.
Binafsi siwatetei wanaoshukiwa kuwa “wachawi” lakini pia, sijapata hoja nzito ya kumfanya mtu makini aamini kuwa, Ulimboka hakuwa na maadui wengine.
Ni kwa msingi huo, jamii isikubali kulishwa maneno na mawazo ambayo hayajathibitishwa na vyombo husika maana wakati mwingine, wezi ndio hao hao hupiga yowe. Jamii yetu sasa iwe na utaratibu mzuri kuwatazama vinara wa migomo au maandamano ili kubaini yaliyo ndani yao au msukumo wa nje kwa kulinganisha na aina ya maisha wanayoishi katika jamii.
Watanzania wakumbukwe kuwa, mataifa mengi sasa yanatumia njia nyingi kuwafanya wananchi kuvurugana wenyewe kwa wenyewe ili mataifa hayo yapate faida mbalimbali zikiwamo za kuuza silaha, kuchimba madini na kutorosha wanyama huku wakijdai kuleta misaada, kumbe wanakuja kunyonya rasilimali za nchi.
Mataifa hayo yanafanya hivyo, kwa kuchochea na kutukuza malalamiko bila kuona mafanikio na kwa ujinga wetu na kama mazuzu, tunakubali kusombwa na wazawa wenzetu kuendesha tunachoita nguvu ya umma.
Kadhalika, nashawishika kuamini kuwa waliomdhuru Dk. Ulimboka ni wale waliochukizwa na migomo; aliouitisha awali, au huu wa sasa kwamba, hasira zinazidi kuwapanda kadiri wanavyoshuhudia mateso na hatimaye, ndugu zao wanakwenda, wanakufa kifo kisicho na utetezi.
Huenda wengine wanaonja mateso ya makali ya maisha baada ya wale waliowategemea kufariki kutokana na mgomo wa Ulimboka na wenzake.
Hili nalo, linanipa shaka kwamba, kadiri madaktari wanavyoendelea kuiasi jamii kwa kuigomea kuipa huduma za tiba, ndivyo wanavyotengeneza hasira zaidi ya jamii dhidi yao na kuhatarisha usalama wao na familia zao, kwa sababu kwa hali inavyoendelea jamii itaungana na kujichukulia sheria mkononi dhidi yao kwa sababu nao wanaonekana kujichukulia sheria mkononi kwa kugoma kinyume cha sheria.
Kwa msingi huo, ninawaomba hao wataalamu wa afya zetu, warudishe moyo wa Kitanzania na hivyo, kuwafikiria wenzao akiwamo Dk. Steven Ulimboka, wanaoteseka kwa maumivu huku wakijua kwamba nao wanaweza kuumia au kupata masaibu ya kiafya maana na wao hawana mwili wa chuma au kama hawaamini wamuulize mwenzao.
Wanaharakati wanaojua kutetea haki hata vyura na mijusi wa Kihansi, watambue tofauti ya thamani ya mtu na vyura na kukubali ukweli kuwa, wanachokifanya madaktari wanaogoma, kinatuangamiza na hivyo, washike mabango kutetea uhai wakijua wanachokifanya madaktari kinahatarisha usalama wa wetu.
Wanaharakati wanapaswa kufahamu na kutambua kwamba, kadri muda unavyopita jamii inajawa hasira na chuki dhidi ya madaktari, kwa sababu wanachokidai ni nyongeza si kwamba hawapati kitu na kwamba wasipoongezewa leo au kesho watakufa kama ambavyo wanaacha wagonjwa wanakufa!
Ingawa siungi mkono mtu yeyote kufanyiwa unyama aliofanyiwa Ulimboka na bado nasikitika na kumpa pole, nimefurahishwa na taarifa aliyotoa mwenyewe kuwa anahisi maumivu makali mwilini mwake maana sasa naye ni mgonjwa.
Kabla hajasafirishwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu, Dk. Ulimboka alinukuliwa akisema kuwa ingawa na maumivu makali, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri ikilinganishwa na siku zilizopita.
Hadi sasa ninaamini kuwa, Dk. Ulimboka anasikia maumivu, kama ambayo Watanzania wengine wamekuwa wakiyapata na hata kusababisha wengine kupoteza maisha, kutokana na juhudi zake na wenzake kusisitiza, kushawishi na kuhakikisha kuwa, madaktari wanagoma hata kuwapa “panadol” wagonjwa wakiwamo majeruhi wenye hali kama yake. Ndugu zangu, hujafa, bado hujaumbika na adhabu ya kaburi aijuaye ni maiti.
Siitetei Serikali lakini pia siamini kuwa inaweza kutaka kuzima moto kwa petroli ndiyo maana itakuwa inakata tawi la mti ililokalia yenyewe. Ndiyo maana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema, “Mazingira ya tukio hili bado yana utata mwingi, yanahitaji uchunguzi wa kina, kila mtu anasema lake, mwingine hili na wengine wanasema Serikali ndiyo imehusika.”
Waziri Mkuu akasema serikali imekuwa ikishirikiana na Dk. Ulimboka katika mchakato wa kumaliza mgogoro kati yake na madaktari na mazungumzo yamekuwa yakienda vizuri. “Mimi nasema kama ni Serikali basi tutakuwa ni watu wa ajabu sana, Serikali tufanye ili iweje?” anahoji Pinda.
Kwa akili ya kawaida, inakuwa pia vigumu kuwahusisha Polisi na Usalama wa Taifa (kama taasisi, labda mtu binafsi) katika mkasa wa Ulimboka, kwa sababu taasisi hizo nyeti hazina mgogoro wowote na madaktari.
Ndiyo maana nashauri kuwa, hao wanaoitwa vinara, waitwe, wahojiwe na hata ikibidi, wawekwe kwenye uangalizi maalumu wa kuchunguzwa ili kubaini ukweli kwa manufaa ya pande zote mbili zinazohusika na mgomo na hasa, kwa manufaa ya umma wa Watanzania.
Nasema hivyo kwa sababu hadi sasa siamini kuwa madaktari wanaogoma sasa na wale wa awali, ni Watanzania kweli; waliosoma kwa kodi za Watanzania na kwamba, wanachodai ni nyongeza ya mshahara na marupurupu na si kwamba hawapati kitu kabisa. Kwamba nyongeza, ndiyo inawafanya wahalalishe watu kufa bila hata kupewa kidonge kimoja. Siamini kabisa!.
Kwa sura hii, ninashawishika kuamini kuwa wataalamu wetu hao wameingizwa na kupandikizwa “roho ya kigeni” wakauza utu wao na utu wetu; wakasahau fadhila za baba, mama na ndugu zao wengine waliowaleta duniani na kuwalea na kinyume chake, wakajipa thamani iliyotukuka ya kutaka kuenziwa kuliko uwezo wa jamii yao. Maana kumdai mzazi anayelala kwenye nyumba ya makuti akujengee ghorofa ni sawa na matusi na kebehi kwa sababu alikuzaa na kukupa fursa ya kustawi.
Mahali popote duniani, inauma sana kuona madaktari wanagoma wakidai nyongeza, huku maisha ya watu yakiteketea na wakati huo huo, wagomaji wanatetewa na wanaojiita wanaharakati wa haki za binadamu. Nashangaa haki gani za binadamu isiyojali haki ya mgonjwa kulindwa na hasa, kuishi.
Tangu miaka ya nyuma na sehemu mbalimbali, walioondokewa na ndugu, jamaa au marafiki zao kama mazao ya migomo ya madaktari, wanajiuliza wasipate majawabu sahihi kwamba, ni ubinadamu upi unaodai nyongeza ya mshahara au masilahi kwa gharama ya uhai wa mwenzako na kumwacha mgonjwa analia kwa maumivu kama ndugu yetu Ulimboka anavyohangaika ingawa yeye amezungukwa na kuhudumiwa na wale marafiki zake waliogoma kwa gharama ya uhai wa ndugu na jamii yao na bado waliogoma wameona hawatoshi, wamemsafirisha nje ya nchi. Ni Watanzania wangapi wanamudu kutibiwa nje ya nchi!
Kwa msingi huo, tuviache vyombo husika vifanye kazi yake kubaini waliohusika na unyama huo na hivyo, tuache kunyoosheana vidole na kupakana ‘uchawi’. Kila anayetaka kufanya hivyo dhidi ya mtu au kikundi kingine, ajiulize kuwa ni kwa nini yeye, chama au kikundi chake kisiaminike kuwa ndicho kilichofanya hayo.
Ifahamike kuwa, yeyote anaweza kuhusika katika tukio hili na kwamba sio madaktari wote wanaopenda kugoma maana wengine wana ubinadamu na subira lakini wanatishwa na hao viongozi. Pia, hakuna anayejua aina ya Dk. Ulimboka sirini kama amekosana na mtu au watu na wakatumia nafasi hiyo kulipiza kisasi wakijua kuwa wamepata mwamvuli wa kujifichia.