HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Tatizo ni kubwa zaidi ya mgomo wenyewe

Mwema Vedasto

 

MADAKTARI wamegoma kwa ajili ya kudai masilahi yao, na pia kwa ajili ya kudai mazingira bora ya kazi. Ni kipindi kigumu kwa wagonjwa na kwa ndugu wa wagonjwa. Mtu ambaye hajaugua au asiye na ndugu mwenye ugonjwa hatari, anaweza asielewe kiundani uchungu wa zahama hili. Pia yule mwenye uwezo wa kupata huduma hii bila kutegemea hizi hospitali zihudumiwazo na walio kwenye mgomo anaweza pia asielewe uchungu wa kinachoendelea.

Rais wa nchi amesema madai ni mazito mno. Jumla ya fedha zote ambazo daktari mmoja anataka alipwe, kulingana na hotuba ya rais, ni takriban shilingi milioni saba kwa mwezi!. Rais amesema hiki ni kiwango kikubwa mno, na serikali kamwe haiwezi kulipa na hivyo wanaogoma, waache tu kazi kwa kuwa mwajiri wao si tajiri wa kiwango hicho.

Mpaka muda huu ninapoandika ukurasa huu, sijajua madaktari wametoa jibu gani kwa hotuba hii ya mkuu wa nchi. Kama fedha hizo ni nyingi au ni kidogo, kwamba serikali inaweza kuwalipa au haiwezi sijui. Lakini mpaka madaktari kuamua kudai mambo hayo, inawezekana ni kwa sababu wameona matundu mengi mno yanayopoteza fedha za nchi. Fedha hizo zikikingwa, zaweza kuongeza kipato chao.

Lakini swali lingine linafuata; Fedha zote walipwe wao madaktari tu? Ndugu zangu, pale serikali inapokuwa na uwezo haba, uwezo dhaifu wa kuongeza pato la nchi, na kutumia vibaya kile kidogo kinachopatikana, ni wazi wafanyakazi muhimu wanaolipwa fedha kidogo watakasirika. Wameanza madaktari. Walimu nao ingawa kelele zao zimekuwa za muda mrefu, wanafuata. Kisha atafuata nani?

Laiti kama kusingekuwepo tabaka la wachache wanaolipwa posho nyingi, wakipewa magari makubwa hata kama wanayo ya kwao binafsi, wakipewa nyumba kubwa za kifahari, hata kama wanazo za kwao, wakipewa posho ya mavazi hata kama mshahara kazi yake ni kununua nguo, naamini migomo isingetokea. Pia migomo isingetokea kama kusingekuwepo na kundi kubwa la watu wanaofanya kazi nyepesi lakini ndio hao wanaolipwa kuliko kila mtu. Kundi kubwa la mawaziri ni mfano mzuri.

Hivi huwa waziri kama wa Maendeleo ya jamii, kazi zake za kila siku ni zipi? Wizara ya aina hii ina Naibu waziri, Katibu mkuu, na maofisa, wote hao wanalipwa mengi kati ya hayo yaliyoorodheshwa hapo juu – nyumba, gari, posho - na mengine tusiyoyafahamu. Kuna naibu waziri wa wizara ambazo haieleweki hata waziri wake anafanya nini, sembuse yeye naibu.

Waziri kama wa wizara ya kazi anapokwenda ofisini huwa anakwenda kufanya nini? kubuni namna ya kuongeza ajira? Lundo lote hili la maofisa wanaolipwa fedha nyingi bila kuonekana kama ofisi zao zina tija, yaweza kuwa sababu za wafanyakazi wetu kushindwa kuamini kuwa kweli serikali haina fedha.

Ndugu zangu, tatizo lililopo ni zaidi ya kumpa daktari kile anachodai. Alichokisema Rais, ni kweli. Kwamba hawa wakipewa hicho wanachodai, je na watumishi wengine itakuwaje? Lakini hilo jibu la rais, hata kama ni la kweli, ni jibu lisilotoa suluhisho lolote. Suluhisho ni kuondoa hawa watu wanaolipwa isivyolingana na wafanyacho. Suluhisho ni kuishi maisha ya kawaida kwa hao wakuu. Suluhisho ni kukusanya fedha. Kila siku tunasikia kuwa madini hayatusaidii. Hapo bado hujazungumzia maeneo yanayoingiza fedha nzuri kama ngorongoro, Kilimanjaro, nk.

Ni kweli inawezekana kabisa kwamba ikiwa daktari atalipwa hivyo vyote anavyodai, na mfanyakazi mwingine yeyote anayepunjwa, naye atadai aongezewe. Kwa hiyo, kwa maoni yangu, hakuna jibu la mkato kwa madai ya madaktari. Inahitajika kwanza usuluhishi wa haraka kwa kuwa watu wanakufa. Haina maana kuwafukuza kazi wakati ukweli ni kwamba hata hawa madaktari waliopo hawatoshi. Kuwafukuza ni kuongeza tu kundi la watu wenye hasira. Na hizi habari kwamba wataitwa madaktari wa kigeni kuziba pengo la hawa wa kwetu, ni kituko kingine. Watalipwa nini?

Usuluhishi wa haraka ufanywe. Baada ya usuluhishi kupatikana, basi serikali iwajibike na kujirekebisha. Kujirekebisha kwa kuonyesha wazi kuwa hakuna kundi la watu wanaolipwa mno bila uwiano na kazi zao, na pia hakuna wanaoteuliwa kupewa kazi ambazo hata wao wenyewe wakiulizwa huwa wanafanya nini wanapokwenda asubuhi ofisini wanaongea mambo ya nadharia tu.

Fujo na machafuko hutokea pale ambapo madai magumu kama haya ya daktari hayafanyiwi kazi. Kuyafanyia kazi kwa kuangalia si madaktari pekee bali na maslahi ya makundi mengine ya watu. Bado hatujafikia hatua mbaya sana kiusuluhishi na kujirekebisha. Bali tunavyozidi kuchelewa, ndivyo na usuluhishi wenyewe utakuwa mgumu huko mbele ya safari.

Ubabe na kauli nyingine zisizo za kirafiki hazisaiidii chochote. Zinaongeza uhasama, zinaongeza vifo zaidi. Fikirieni kuhusu fujo za Misri na kwingineko. Na kihistoria, pale mfumo unapokuwa mbovu, ni lazima mfumo huo utengeneze wenyewe sababu za kuporomoka kwake. Kumbe si madaktari au mfanyakazi mwingine yeyote anayeporomosha mfumo mbovu bali ni ubovu wenyewe wa mfumo.

Wakubwa wanapozubaa na kuacha kuchukua hatua stahiki, wanatengeneza maafa. Ni wazi kuwa baada ya maafa, maisha yaweza kuwa mazuri baada ya wahalifu kuadhibiwa na demokrasia kuchukua mkondo wake wa kweli. Lakini gharama hizi za kusubiri kanuni za kihistoria ziturekebishe, ni kanuni za hatari mno.

Fikiria hasira zinazowapata wagonjwa, zinazowapata ndugu wa watu wanaokufa wakati wanajua tiba ipo, ila ni kutokuwajibika tu kwa watu. Kuacha kuchukua hatua za usuluhishi mapema, ni kuongeza kundi la watu wengi zaidi wenye hasira na mabao ni vigumu sana kuwa – organize na kuwaweka katika meza ya suluhu.

Kuacha kurekebisha mfumo mzima unaotengeneza matabaka, ni kuporomosha amani. Na ikishafikia hapo, wa kulaumu wala sio wanachama wa upinzani. Lawama ni za uongozi unaokwepa wajibu. Kazi isiyo na tija inayofanywa na kundi la wakuu wa mikoa linalokwenda Dodoma kusikiliza waziri mkuu ni namna nyingine ya kuonyesha jinsi watu wasivyo na kazi zenye tija. Katika dunia ya sasa, hapa Tanzania bado ni lazima kila mkuu wa mkoa aende Dodoma kumsikiliza waziri mkuu. Hizi e- mail, hizi simu, hizi fax, kazi yake nini? Hawezi kubakia mkoani kwake na kumsaidia waziri mkuu kujibu hoja akiwa huko?

Ni ujinga mwanasiasa kusimama na kulaumu tu kwamba “kuna watu wanataka kuvuruga amani ya nchi tuliyoachiwa na Mwalimu Nyerere” bila wao wenyewe kujitahiidi kuishi kama huyo Nyerere. Hawajui kwamba amani hutengenezwa, na hutengenezwa kwa mfumo usiojenga matabaka, bali kwa mfumo wa kushirikishana kilichopo na kufanya kazi kama huyo Nyerere alivyokuwa. Nyerere na CCM yake ni tofauti na hawa wa leo na CCM yao. Ya Nyerere ilijenga amani. Hii inabomoa.

Mbunge alisimama bungeni akalalamika kwamba kuna mabasi madogo ya wabunge, yasiyo na kiyoyozi ambayo huwapeleka kwenye miradi mbalimbali wawapo bungeni . “Hayana kiyoyozi. kwa hadhi ya mbunge, gari hii haimfai, kwani inambidi avue koti kwa kuwa gari haina AC (kiyoyozi)”! Mbunge huyu mwanamke akasema kwa kuwa kila mbunge ana gari lake, basi kila mbunge atiliwe mafuta kwenye gari yake mwenyewe yenye AC badala ya kupanda mabasi yasiyo na hadhi. Kazi ya kuvaa koti na kukaa kwenye Air conditioner! Hawa ndio wanavunja amani ya nchi, hawa ndio wanachochea migomo.

Mfumo unaojenga tabaka ufumuliwe, na hapo madai ya madaktari na ya makundi mengine yatakoma.



mwemav@yahoo.com Sms 0784774069
juu