SERIKALI imesema kama kuna ulazima wa kuwaachisha kazi wafanyakazi wa viwanda mbalimbali vilivyobinafsishwa basi serikali itakuwa tayari kubeba jukumu la kulipa mafao yao.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Viwanda na Bishara, Pereila Silima, wakati akijibu swali la Mbunge wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA).
Katika Swali la msingi la mbunge aliitaka Serikali kueleza kuwa ni lini itakamilisha kazi ya kushughulikia malalamiko ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa viwanda mbalimbali hapa nchini.
Akijibu swali hilo Naibu huyo alisema kuwa wafanyakazi walioachishwa kazi katika viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Ubungo Spinning Mill, Polyasacks, Tanzania Dairies na zana za kilimo (UFI) walilipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria.
Alisema madai yaliyokuwa Tanzania Sewing Thread Manufacturers yalilipwa kupitia ufilisi uliofanywa na Benki ya Rasilimali (TIB).
Kwa upande wa kiwanda cha maziwa cha Tanzania Dairies hicho kiliwekwa chini ya ufilisi wa lililokuwa shirika la utafiti na ushauri wa maendeleo ya viwanda (TISCO) ambapo wafanyakazi walilipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria ya ufilisi.
Aidha alisema wafanyakzi wa kiwanda cha nguo cha urafiki hawakupunguzwa kazi kwa sababu mkataba wa ubinafsishaji ulibainisha wafanyakazi waendelee na ajira.
“Kama kuna ulazima wa kuwaachisha kazi ukijitokeza basi serikali itabeba jukumu la kulipa mafao hayo,” alisema.
Alisema pamoja na kuwalipa mafao wafanyakazi waliopunguzwa kazi, serikali imeendelea kupokea madai ya mapunjo kutoka kwa waliokuwa wafanyakazi wa viwanda na mashirika mbalimbali yaliyobinafsishwa na yamekuwa yakishughulikiwa kulingana na hoja na vielelezo vya mhusika kwa kuzingatia sheria.
Naibu Waziri huyo alibainisha kwamba baada ya wizara hiyo kwa kushirikiana na (CHC) kufanya uchambuzi wa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo vimefungwa na kubadiliswa matumizi, waraka wa baraza la mawaziri umeandaliwa ili kujadili katika ngazi ya pili ya maamuzi.
Alisema Serikali imewaruhusu baadhi ya wawekezaji kubadili matumizi ya viwanda pale ambapo mabadiliko yalionekana kuwa na manufaa kwa taifa.