BENDI ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo’ inatarajiwa kufanya onesho maalumu la kuzindua ukumbi wao unaojulikana kama Bongo Resort uliopo Kimara Dar es Salaam, Julai 7, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Kamarade Ally Choki, alisema, onesho hilo litafanyika kwa ajili ya kuzindua ukumbi wanaoumiliki kwa sasa, ambao zamani ulikuwa ukijulikana kama White House.
Alisema, katika uzinduzi huo, bendi ya Extra Bongo itasindikizwa na kundi la Coast Modern Taarab, iliyo chini ya Omary Tego, Baikoko kutoka Tanga, Hussein Machozi, Sheta na Tunda Man, ambapo kiingilio kitakuwa ni sh 7,000.
Aidha, alisema, katika tamasha hilo, Extra Bongo itatumbuiza nyimbo za zamani kama vile ‘Double Double’, ‘Tatu mara tatu’, Fikiri Madinda, Regina Zanzibar huku nyimbo mpya ikiwa ni ‘Mama Shuu’, ‘Bakutuka’, ‘Watu wa Falsafa’, ‘Ufisaidi wa Mapenzi’ na ‘Mtenda akitendewa’.