WADAU wa michuano ya Polisi Jamii kutoka kata nane za Wilaya ya
Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam wameomba michuano hiyo isogezwe mbele hadi Julai 9 badala ya kuanza jana kama ilivyopangwa.
Wakizungumza katika sherehe za uzinduzi wa michuano hiyo iliyofanyika katika ofisi za Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, juzi, wadau hao walisema, sababu ya kuomba michuano hiyo isogezwe mbele ni kutoa fursa ya kujiandaa zaidi kwa ajili ya kuwania zawadi ya sh milioni moja itakayotolewa kwa mshindi wa kwanza katika soka.
Mwakilishi wa wadau hao, aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdul,
kutoka Kata ya Mwananyamala, alisema kutokana na umuhimu wa michuano hiyo na aina ya zawadi iliyopangwa, haitakuwa vema kwa timu zao kushiriki pasipo kuwa na maandalizi mazuri.
Awali Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi ya Kinondoni, (OCD), Mrakibu Mwandamizi (SSP), Willbroad Mutafungwa, alitaja zawadi kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu kuwa ni sh milioni moja, sh 500,000 kwa wa pili na 250,000 kwa mshindi wa tatu.
Licha ya zawadi hizo, SSP Mutafungwa alisema, kila timu itakayoshiriki itapewa jezi pamoja na usafiri wa kwenda na kurudi wakati michuano hiyo ikiendelea.
Mbali na zawadi hizo, pia kutakuwa na zawadi mbalimbali kwa timu bora, mchezaji bora na timu yenye nidhamu zaidi.
Mutafungwa aliongeza kuwa, kabla ya michezo hiyo kuanza, kutakuwa na utoaji wa elimu kwa timu husika juu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, mbinu za kujikinga na kuwakinga wengine na uhalifu, pamoja na elimu ya kujihami na maambukizi ya magonjwa hatarishi, ikiwamo ukimwi.