TUME ya Mabadiliko ya Katiba imewasisitizia wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano inayoitishwa na tume hiyo ili watoe maoni yao kwa uhuru na uwazi.
Ufafanuzi huo unakuja ikiwa ni siku chache tangu kuzuka malalamiko ya baadhi ya wananchi wakidai kuwa tume hiyo imeweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaotoa maoni katika mikutano yake inayoendelea katika mikoa minane.
Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid, alisema jana kuwa tume ingependa kupata maoni ya kila mwananchi na hivyo haiwezi kuweka ukomo kwao kutoa maoni katika mikutano inayoitisha.
Ufafanuzi wa tume hiyo unafuatia taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikinukuu baadhi ya wananchi wakilalamika kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeweka kikomo cha idadi ya maswali na watu wanaotakiwa kutoa maoni yao katika mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi.
Taarifa hizo ziliongeza kuwa tume imekuwa ikitoa nafasi kumi tu kwa wananchi wanaopaswa kuuliza maswali yasiyozidi kumi katika mkutano mmoja na kwamba katika baadhi ya wilaya, ikiwemo Biharamulo yenye kata 15, ni kata sita tu ndizo zilizofikiwa na chombo hicho.
“Katika baadhi ya wilaya, kama Kusini Unguja na Bahi mkoni Dodoma, tume imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano hadi kufikia mitatu badala ya miwili kwa siku. Hatua hizi zinalenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao,” amesema Assaa katika taarifa yake kwa vyombo habari.
Kuhusu mikutano iliyofanyika wilayani Biharamulo, Assaa alisema tume ilipanga na imefanya mikutano sita kuanzia Julai 2 hadi 4 mwaka huu, na jumla ya wananchi 267 walitoa maoni yao kwa mdomo na wengine 265 walitoa maoni yao kwa maandishi.
Kwa mujibu wa katibu huyo, vituo ambavyo mikutano hiyo ilifanyika ni Kelenge, Movata, Nyamigogo, Runazi, Nyakanazi na Biharamulo mjini.
“Katika mikutano hiyo na mingine yote tume haikuweka na haitaweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaopaswa kutoa maoni,” alifafanua Assaa na kuongeza kuwa tume inatambua kuwa wananchi wana shauku kubwa ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Hata hivyo, katibu huyo alisema kuwa ingawa tume ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo, jiografia ya nchi na muda ambao tume imepewa, jambo hilo halitawezekana na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo tume itafanya mikutano kama ratiba iliyotolewa inavyoelekeza.
Akifafanua kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya kata hazitafikiwa na tume, alisema tume haikupanga ratiba ya mikutano ya kukusanya maoni kwa kuzingatia kata, bali eneo ambalo linaweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya kata moja.
Pamoja na kutoa maoni yao kupitia mikutano, tume pia imewaomba wananchi kuendelea kutumia fursa nyingine kuwasilisha maoni yao kama tovuti ya (www.katiba.go.tz), barua pepe (maoni@katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 1681, Dar es Salaam na S.L.P. 2775, Zanzibar.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kufanya awamu ya kwanza ya mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa minane Julai 2 Julai mwaka huu, na inatarajiwa kumalizika Julai 30 katika mikoa hiyo ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.