VIONGOZI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wametakiwa kuhakikisha wanaondoa migongano na migogoro kwa kukaa meza moja na si kusengenyana ambako kutasababisha chama kubomoka.
Akizungumza jana wakati wa kuwakabidhi ofisi viongozi wapya wa UVCCM Kata ya Tandika jijini Dar es Salaam, Katibu Kata wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho, Sudi Mlilo, alisema kuwa maneno ya pembeni ndio yanayoleta mtafaruku katika vyama vya siasa.
Mlilo pia aliwataka viongozi hao kutokubali kuyumbishwa na watu wanaotaka kuiharibu CCM pamoja na wale wanaowatumia kipindi cha kutafuta madaraka akisema kuwa mwisho wa siku wakishapata huwasahau.
“Kama mtakumbuka tumekaa miaka mitano bila kuwa na viongozi wa vijana katika kata hii kwa sababu ya misuguano sasa ninyi mnatakiwa muwe makini na msikubali kugombanishwa na watu wanaowatumia kutafuta madaraka na hivyo mkaivunja CCM,” alisema.
Naye katibu mhamasishaji na chipukizi wa kata hiyo, Benjamin Mapunda, aliwataka viongozi hao kutumia kanuni zaidi na kutambua wajibu wao.
Viongozi hao waliochaguliwa ni Seif Hassan Seif ambaye anakuwa mwenyekiti, katibu wake ni Hadija Msoka, Naima Waziri na Shemaya Boro walichukua nafasi za ujumbe wa kamati ya utekelezaji.