JANA katika gazeti hili kulikuwa na habari iliyosomeka kuwa ‘Ikulu yawakataa viongozi wa dini’. Katika taarifa hiyo Ikulu ilisema kuwa hawana sababu ya madaktari kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali.
Ikulu ilifikia kutoa kauli hiyo baada ya siku chache viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kujitosa katika sakata la mgogoro wa madaktari unaoendelea nchini.
Ikulu ilikwenda mbali zaidi na kusema kuwa viongozi hao wa dini mara zote wanapoomba kukutana na viongozi wa serikali akiwamo rais hawapitii kwa mtu yeyote, isipokuwa huomba moja kwa moja na kukubaliwa.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mgomo wa madaktari umekwisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini, jambo ambalo ni jema sana.
Sisi tunaamini kuwa sakata hili mgomo wa madaktari bado ni zito na linalohitaji juhudi za pamoja, ikiwamo hatua iliyofikiwa na viongozi wa dini kuomba kukutana na Ikulu ili kutatua tatizo hilo linalohatarisha maisha ya Watanzania wasio na hatia.
Tunatambua kuwa Ikulu isichukulie suala hilo kwa wepesi, ni jambo linalohitaji kuonyesha dhamira ya dhati kutafuta suluhu ambayo haiwezi kupatikana bila kukaa na kujadili kwa mara nyingine.
Tunaamini kupitia mazungumzo kuna kushindana kwa hoja za nguvu, si nguvu za hoja na mwishowe tutapata muafaka kwa masilahi ya taifa na wananchi wake.
Hatukubaliani na sababu zilizotolewa na Iluku, kudai kuwa mgomo umekwisha huku ikionesha wazi kuwa madaktari hawana ari ya kufanya kazi na hata wale wanaosemekana kuendelea na kazi wanaonekana wazi kuwa wapo katika mgomo baridi.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kuwa Watanzania wa hali ya chini ndio wanaopata tabu za kukosa matibabu pindi wafikapo katika hospitali za rufaa, tofauti na viongozi ambao wengi hutibiwa nje ya nchi na hawaathiriwi na mgomo huo.
Hatuamini kuwa kuonyeshana ubabe au kutunishiana misuli ili kuona nani mwenye nguvu kunaweza kulitatua tatizo hilo.
Tunaomba Ikulu itumie busara na hekima ili kuhakikisha huduma katika hospitali zetu zinarejea kama awali kuliko kuendelea kulumbana kusikokuwa na tija kwa taifa.
Tunasema kuwa kuna umuhimu wa Ikulu kurudi na kupitia upya taarifa iliyotolewa na viongozi wa dini ambao ni watu muhimu katika mchango wa taifa hili.
Tunafahamu kuwa Ikulu imekuwa wakati wote ikithamini na kuwashirikisha viongozi wa dini katika masuala mbalimbali ya nchi yetu, hivyo hata katika hili kuna haja ya kuwapa nafasi ya kukaa meza moja na kutatua matatizo ya madaktari.
Tunaiomba serikali itathmini kauli ya viongozi wa dini katika sakata hili kuliko kutaka kuonyeshana ubabe, kwa kuwa kutokana na mapambano ya pande hizi mbili wanaoumia ni wananchi wa hali ya chini.