KATIKA kipindi cha mwaka 2010 na 2011 nchi ya Tanzania ilikabiliwa na changamoto kubwa iliyotokana na ukosekanaji wa umeme wa uhakika.
Katika nchi yoyote ikiwa na tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika ni dhahiri kutakuwa na matatizo mbalimbali ya kiuchumi, ikiwa ni kwa mtu mmoja mmoja au kwa taifa kwa ujumla.
Wizara ya Nishati na Madini mara kadhaa imekuwa ikipata lawama kutokana na kutofuatilia suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na wananchi , wanasiasa na hata wanaharakati kutuhumu hata uongozi uliokuwa madarakani kwamba umeshindwa kufanya kazi ya kutatua tatizo hilo.
Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambapo katika Wizara ya Nishati na Madini alichagua waziri mmoja na manaibu waziri wawili huku kila mmoja akipewa sekta yake ya kufuatilia ikiwa ni pamoja na madini na Nishati.
Kwa sasa Watanzania wengi wamekaa mkao wa kula kuangalia utendaji wa viongozi hao kama kutakuwa na utatuzi wa suala hilo ingawa kwa sasa kumeanza kuleta matumaini.
Hata hivyo ilizungumzwa kwamba kwa kipindi kirefu tumekuwa tukitegemea umeme wa chanzo kimoja kikubwa cha maji.
Hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alifungua kituo cha kufua umeme wa MW 105 unaoitumia gesi asili.
Hii ni kutokana na kutaka kuepuka matumizi ya chanzo kimoja cha umeme ikiwa ni maji ambapo anasema jumla ya MW 561 sawa na asilimia 41 ya umeme wote unaotumika wakati huu na dizeli MW 260 sawa na 19% ya umeme wote ambao alisema ndio unaotumia fedha nyingi kwenye sekta ya uzalishaji wa umeme.
Profesa Muhongo anasema kuwa mitambo ya kituo hiko kipya ni mali ya Serikali ambayo imegharimu dola za Marekani millioni 124,895,988 .
Hata hivyo hakusita kuwashukuru serikali ya Norway kupitia kampuni ya GEIK waliodhamini kupata mkopo kutoka benki ya HSBC na kujenga kituo hiko.
“Uwekezaji huu wenye thamani kubwa ni kielelezo kingine kinachoonesha dhamira nzuri ya serikali ya kutatua tatizo la umeme ambalo limekuwa sugu na la miaka mingi,” anasema Prof. Muhongo.
Anasema baada ya uzinduzi huo mitambo yote ya gesi iliyopo Dar es Salaam na Mtwara itazalisha umeme wa jumla ya MW 554 sawa na asilimia 40 ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo kwa sasa MW 1375 huku akieleza serikali inahitaji sana kupunguza utegemezi wa umeme wa maji ambao kwa sasa hautabiriki na umesababisha nchi kukosa umeme wa uhakika mwaka hadi mwaka.
Profesa Muhongo anasema kuwa hadi kufikia sasa gesi asili ya jumla ya futi za ujazo trilioni 26.99 (26.99 cft, sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4.86) huku akiahidi kuwa utafutaji bado unaendelea.
Anasema serikali inatayarisha sera ya gesi kwa kutumia wataalamu watanzania ambayo itajadiliwa na wadau wengi wakiwemo weyeji wa Mtwara na Lindi ili kuwezesha kuwa na msingi mzuri wa maandalizi ya muswada wa gesi na kanuni zake kwa manufaa ya taifa.
Hata hivyo anasema licha ya kutumia vyanzo vingine mbalimbali serikali imeamua kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme ifikapo mwaka 2015 -2016 na kupelekea kupata umeme wa kutosha katika wingi usiopungua chini ya MW 200.
“Vile vile serikali imeamua kutumia vyanzo vingine zaidi vya kupata umeme wa uhakika kutoka kwenye upepo , jua na jotoardhi, jitihada hizi ni kuhakikisha kwamba nishati ya uhakika inapatikana ili kutimiza malengo ya maendeleo yetu yaliyoanishwa kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ambayo yanakusudia kuifanya nchi zenye kipato cha kati cha dola za Marekani 3,700-12,000,” anasema Prof. Muhongo.
Anasema pamoja na Shirika la Umeme kuimarisha na kuendeleza ongezeko la ujenzi wa vituo mbalimbali vitakavyoimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji tayari anasema imeanza kutekelezwa.
Prof. Muhongo anasema kuna mradi mkubwa wa msongo wa kilovoti 400 utakaotoka Iringa hadi Shinyanga huku akieleza kuna mipango ya kupanua msongo wa KV 400 kuunganisha Dar es Salaam, Tanga, Moshi, Arusha na Singida.
Katika ufunguzi huo pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO), Injinia William Mhando anasema shirika hilo lilisaini mkataba wa ununuzi na utekelezaji na Kampuni ya Jacobsen AS kutoka Norway Septemba 27 mwaka 2010 ambapo mkandarasi alikuwa na jukumu kubwa la kuleta mashine za kufua umeme, kufanya kazi za ujenzi kuzifunga hadi kukamilisha na kukabidhi mtambo kwa ukamilifu.
Anasema ujenzi huo ulikamilika Mei 2012 na kukamilisha kufanyika kwa majaribio Juni mwaka 2012.
Injinia Mhando anasema kituo kimeanza uzalishaji wake Juni 29 mwaka huu ikiwa inachangia katika gridi ya taifa MW 105 kikiwa na mashine tatu aina ya STG 800 zilizotengezwa na Kampuni ya Siemens kutoka Sweden.