HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 10 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

‘Waathirika 1,697 wa mabomu Mbagala wanalipwa’

JIBU LA SWALI LA MBUNGE Kigamboni

na Mwandishi wetu, Dodoma

 

SERIKALI imeanza kulipa fidia kwa wananchi wa Mbagala ambao hawakupatiwa fidia ya awali kutokana na tathmini ya pili kubaini kuwa walikuwa na haki ya kulipwa.

Hayo yalibainishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi, akisema kuwa katika kipindi hiki, wananchi 1,697 walionekana kuwa wanastahili malipo hayo.

“Kati ya wananchi 2,575 waliolalamika kuwa tathimini haikuwapitia, serikali imehakiki na kubaini kuwa jumla ya wananchi 1697 walionekana wanastahili kulipwa fidia ya jumla ya sh bilioni 2.2 na tayari fedha imeshapelekwa katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam tangu Juni 6, mwaka huu,’’ alisema Lukuvi.

Lukuvi alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM), ambaye alitaka kujua ni vigezo vipi vilitumika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Mbagala waliokumbwa na mlipuko wa mabomu.

Mbunge huyo pia alihoji serikali itawalipa lini wahanga wa mabomu hayo ambao hawakufanyiwa tathmini na sababu za baadhi ya watu kulipwa hundi ya sh 1,000.

Lukuvi alikiri kuwa yako matatizo makubwa katika ulipaji wa fidia kwa wananchi ikiwamo wizi na udanganyifu kutoka pande zote.

Kwa mujibu wa Lukuvi, zoezi hilo awali lilionyesha kuwa fidia iliyopaswa kulipwa ilikuwa ni sh bilioni 12 lakini baadaye ilibainika kulikuwa na malipo hewa na hivyo tathmini kamili ikaonyesha kuwa zilitakiwa sh bilioni 7.7 tu.

Alisema watathmini waliokwenda kufanya kazi hiyo walikuwa wakiwalazimisha baadhi ya watu kusimama katika nyumba ambazo si mali yao na kuwaahidi kuwa zitakapolipwa fedha hizo wangegawana nusu kwa nusu.

Akizungumzia malipo kwa wananchi wa Gombolamboto, alisema baadhi ya wananchi wamekataa nyumba walizojengewa na serikali na badala yake wanataka fedha jambo ambalo linaifanya serikali ifikirie namna ya kuzungumza nao.



juu