NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, amewapongeza waandaaji wa Tamasha la Usiku wa Matumaini lililokuwa na lengo la kuchangia mfuko wa elimu ili kuzidi kupiga hatua zaidi.
Tamasha hilo lilifanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na kupambwa na burudani mbalimbali ikiwamo pambano la soka katika ya wabunge mashabiki wa Simba na Yanga, ambako Naibu Waziri huyo aling’ara vilivyo na kikosi chake cha Simba.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi, Makalla alisema, anamshukuru Mungu kwa wadhifa alionao, hasa katika wizara hiyo na aliyemteua hajakosea kwa kuwa anaimudu ipasavyo.
“Mimi nawezasema, pele limepata mkunaji, maana ukweli ni kwamba wizara hii hawajakosea kabisa kunipatia mimi kuisimamia,” alisema Makalla.
Makala ambaye pia ni Nahodha wa timu ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge Fc na Nahodha wa Wabunge Mashabiki wa Simba, alisema kuwa hawajakosea kumchagua kwa kuwa hata yeye michezo anaijua kucheza.
“Nadhani umeona, mimi nimeingia dimbani na nimecheza na ndiyo maana nasema Wizara hii ni pele limepata mkunaji,” alisema.
Alisema, kutokana na umuhimu wa mchezo huo katika jamii, wametoka bungeni bila ya kujali hakuna posho yoyote kutoka kwa waandaji hao, kutokana na mchango huo kwenda katika sekta ya elimu ambayo inawahusu pia na wao kama viongozi wa nchi.
Aidha, Makalla aliwapongeza wabunge wote wa Simba na Yanga kwa kujitolea na kushiriki katika mchezo huo, ikiwa ni pamoja na sehemu yao ya kujenga mwili na kujiweka vema kiafya.
Naye Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani ‘Majimarefu’, alisema kuwa kutokana na mapenzi aliyonayo kwa Simba na nchi yake, ndiyo sababu kubwa iliyomsukuma kucheza pambano hilo licha ya kuwa mgonjwa wa mkono.
“Mie mkono kama unavyouona, ulivunjika na bado sijapona, ila naendelea vizuri lakini kutokana na mapenzi na Simba na nchi yangu, pamoja na wachezaji kuwa wachache, ikanilazimu kucheza hivyo hivyo ila namshukuru Mungu tumeshinda,” alisema Majimarefu.