TIMU ya soka ya Nyanda za Juu Kusini imetinga fainali ya michuano ya 18 ya shule za msingi (UMITASHUMTA), baada ya kuilaza Kaskazini Magharibi kwa mikwaju ya penalti 3-2 katika mechi ya nusu fainali ya kwanza iliyochezwa jana asubuhi kwenye viwanja vya Shirika la Elimu mjini hapa.
Kwa ushindi huo, Nyanda za Juu Kusini itasubiri mshindi kati ya Kaskazini Mashariki na Ziwa, ambao walikuwa wakiumana jana jioni, kwenye fainali itakayochezwa kesho asubuhi uwanjani hapa.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na upinzani mkali, hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilikuwa suluhu ya bila kufungana kabla ya kuamuliwa kupigwa matuta, ambako penalti za ushindi za Nyanda za Juu Kusini zilipigwa na Casian Mlula, Adam Mbena na Mohamed Kasim huku Herman Luhwago akikosa, wakati zile za Kaskazini Magharibi zikifungwa na Martin Emanuel na Abdul Suleiman huku Jacob William na Calvin Msafiri wakipoteza.
Katika netiboli, wenyeji Mashariki imetinga fainali baada ya kuichakaza Kaskazini Mashariki kwa magoli 25-17 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa jana asubuhi, ambako sasa itavaana na Nyanda za Juu katika fainali itakayochezwa kesho asubuhi huku Kaskazini Magharibi ikitafuta mshindi wa tatu dhidi ya ziwa.
Michuano hiyo inayoshirikisha kanda 11, itafikia tamati kesho ambapo itachezwa fainali ya soka na netiboli.