HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 15 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Silima: Watajeni askari wanaoficha taarifa za wauzaji gongo


na Nasra Abdallah

 

WANANCHI wametakiwa kuwafichua kwa majina askari polisi na watu wote wanaoficha taarifa za wauza pombe haramu ya gongo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa tukio la wananchi saba wa Mtaa wa Mbuyuni uliopo Kata ya Kigogo, Kinondoni kupoteza maisha na baadhi yao kunusurika baada ya kunywa pombe hiyo.

Silima ambaye jana aliamua kutembelea eneo hilo na kukutana na viongozi na wananchi wa kata hiyo, alisema inawezekana kuwa miongoni mwa wateja wa ‘gongo’ ni askari polisi, hivyo wananchi wanapaswa kuipatia wizara taarifa dhidi ya watu wanaojishughulisha na biashara hiyo.

Pia aliwataka wananchi hao kushirikiana na jeshi hilo pamoja na viongozi wao katika maeneo wanayoishi kuunda vikundi imara vya ulinzi shirikishi vitakavyosaidia mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu na uhalifu kwa ujumla.

Kuhusu vifo hivyo, waziri huyo amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake kwa kina, ili kubaini chanzo kilichosababisha vifo hivyo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuanzia siku ya tukio hilo, Polisi ilifanya msako katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakamata watu 12 wakiwa na lita zaidi ya 180 za pombe hiyo.

Kwa mujibu wa Kenyela, lengo lao mbali na kukamata wauzaji wa gongo, pia watahakikisha wanakamata mitambo inayotengeneza pombe hiyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watakaobainika.

Gongo hiyo inadaiwa kutengenezwa na mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Hekima, ambaye pia ni mmoja wa watu waliokufa katika tukio hilo.



juu