MAJAJI wa shindano la kusaka vipaji wa Epiq Bongo Star Search 2012, jana wametoa somo la muziki kwa vijana waliojitokeza katika usaili kuwania nafasi ya kuwakilisha mkoa huu katika shindano hili kubwa zaidi la kuimba nchini.
Majaji hao, Salama Jabir, Master J na Ritha Paulsen, ambao wamekuwa katika tasnia ya muziki kwa muda mrefu, wametumia muda mwingi kuwashauri vijana kuhusu mbinu za kufanikiwa katika muziki.
“Tunawaeleza kuhusu soko la muziki na aina ya miziki ya kuimba ili wafanikiwe, hiyo ni sehemu ya kazi yetu, lakini pia vijana wengine tumewashauri kujiunga na fani nyingine ambazo tumeona wana vipaji, kama uigizaji au uanamitindo,” alisema Jaji Mkuu, Ritha Paulsen.
Vijana wengi waliojitokeza, waliwapongeza majaji kwa elimu hiyo ya muziki huku wakibainisha, wamefurahia ushauri huo na utawasaidia katika kujiendeleza kisanaa. “Unajua hawa majaji, wamefanya hili zoezi kwa miaka mingi, hivyo ni wazoefu na wakikwambia huwezi, jaribu kitu kingine, unapaswa kuelewa,” alisema mmoja wa washiriki, Baraka Juma.
Jiji la Mwanza ndilo lilitoa mshindi wa mwaka jana, Pascal Cassian, huku pia likiwa lilishawahi kutoa mshindi mwingine miaka ya nyuma, hali iliyowafanya vijana wengi waliojitokeza kuwa na matumaini makubwa.
Akiuzungumzia Mkoa wa Mwanza, Ofisa Biashara wa Zantel, Sajid Khan, alisema shindano la mwaka huu ni zaidi ya kutafuta vipaji.
“Kama unavyoona, tuna shughuli za utoaji damu zinaendelea hapa, ambapo Mwanza zaidi ya mikoa yote, naona hamasa imekuwa kubwa sana,” alisema Khan.
Mshindi wa mwaka huu atajinyakulia sh milioni 50 na mkataba wa kurekodi kutoka Zantel.