KAMPUNI ya Mwanzoa Promotions ya jijini Tanga, katika mikakati yake ya kuendeleza michezo mkoani humo hususan masumbwi, imeandaa mapambano ya ubingwa wa Afrika Mashariki yatakayorindima Iddi Mosi na Pili.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mwazoa Promotions, Ally Omar, hiyo ni moja ya mikakati ya kunyanyua vipaji vya wanamichezo wa Jiji la Tanga.
Alisema, maandalizi yamekamilika na mabondia wapo katika hali nzuri ya ushindani, ambako Iddi Mosi kwenye ukumbi wa CCM Hall, Said Mundi wa Tanga atazipiga na Habibu Pengo kutoka Dar es Salaam kugombania ubingwa wa Taifa wa TPBC, Super Feather raundi 10.
Mapambano mengi yatawakutanisha Jumanne Mohamed wa Tanga na Ali Bugingo wa Dar es Salaam Light raundi 10, huku Haji Juma wa Tanga akivaana na Mwaite Juma wa Dar es Salaam, Super Fly raundi nane.
Omar aliongeza kuwa, mapambano hayo yatatnguliwa na uale ya utangulizi yatakayoshirikisha mabondia kutoka vitongoji mbalimbali vya Jiji la Tanga.
Mkurugenzi huyo alisema, Iddi Pili kwenye ukumbi wa Pweza, kutakuwa na pambano kubwa la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, kati ya Alen Kamote wa Tanga na bondia toka Uganda, litakalokuwa na raundi 10 huku Zuberi Kitandula wa Tanga akizitwanga na Sadiki Abdulazizi wa Dar es Salaam raundi 10, wakati Jay Jay Ngotiko wa Tanga atapimana ubavu na Juma Afande kutoka morogoro.