HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatatu, 20 agosti 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Kusajili ‘mapro’ bila kujaribiwa, vipimo

Ruhazi Ruhazi

 

KAMA kuna kioja katika soka yetu, ni kitendo cha viongozi wa klabu hasa za Simba na Yanga, kuamua kusajili wachezaji kwa mamilioni ya fedha bila kuwafanyia majaribio wala vipimo vya afya kama ambavyo huwa kwa klabu nyingine duniani.

Sote tumeshajionea madhara ya usajili wa aina hii ambao unaishia kuzitia klabu gharama na hasara kubwa zisizo za ulazima wowote kama ilivyowahi kutokea misimu kadhaa iliyopita kwa klabu hizo mbili ambao licha ya kusajiliwa kwa fedha nyingi, wameshindwa kutoa mchango uliohitajika.

Mfano mzuri, ni usajili uliofanywa na viongozi wa Simba mwezi uliopita wa kumsajili kwa mbwembwe kiungo Nkanu Mbiyavanga kutoka DR Congo ambaye baada ya kuchezeshwa mechi chache za Kombe la Kagame, ikabainika ni bomu.

Usajili wa Mbiyavangu, ni mwendelezo wa madudu ya msimu wa usajili yanayofanywa na viongozi wa klabu hizi kubwa nchini chini kila mwaka kwa mwavuli wa kamati zao za usajili ambazo hazifuati kanuni za usajili zinazotaka mwongozo wa benchi la ufundi chini ya Kocha mkuu.

Jukumu la benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, hupendekeza majina ya wachezaji anaowahitaji kulingana na udhaifu wa kikosi chake, kocha hupendekeza wachezaji iwe kwa majina au sifa na jukumu la uongozi ni kuwaagiza wasakaji vipaji wa klabu, kuwasiliana na wachezaji hao iwe kupitia kwa viongozi wa klabu zao moja kwa moja kupitia kwa mawakala wa wachezaji husika.

Baada ya zoezi la kuwapata, wachezaji hao huitwa kwenye majaribio na wanapofaulu hupimwa afya zao na jopo la madaktari nia ikiwa ni kuepuka kumsajili mchezaji majeruhi ambaye ataigharimua klabu badala ya kuisaidia kutimiza malengo yake.

Kichekesho kilichopo kwenye klabu zetu ni kwa viongozi wetu hawa kupuuza mapendekezo hayo ya makocha badala yake kuwasajili wachezaji wanaowataka wao kwa nia ya kuwafurahisha ama kujaribu kupunguza ghadhabu za wanachama ana mashabiki wa klabu hizo.

Siasa hizi za soka, ndizo ambazo ziliwafanya viongozi wa Simba kumsajili Mbiyavanga, bila ya kumfanyia majaribio wala vipimo vya afya, hupaswa kupata muda wa kuwafuatilia wachezaji hao na kwa wale wasiofahamika ku na usiofuata na siku chache baadaye kumuacha moja kwa moja bila ya kuwafanyia majaribio wachezaji wa kigeni.

Mwaka 1996, Dunia ilikumbwa na fadhaa baada ya kukwama kwa usajili wa mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Nigeria, Nwakwo Kanu, aliyebainika kuwa na tatizo la moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi na jopo la madaktari wa klabu ya Inter Milan ya Italia.

Taarifa hizo zililiwashtua waafrika wengi hasa ikizingatiwa kuwa mchezaji huyo aliweza kuandika historia kwa kuing’arisha Nigeria iliyoweza kuandika historia kwa kutwaa taji la Olimpiki mwaka huo wa 1996.

Kanu aliyekuwa akiichezea Ajax Amsterdam ya Uholanzi, alifunga mabao mawili katika mechi ya nusu fainali walipoilaza Brazil kwa mabao 3-2 kabla ya kufunga pia katika mechi ya fainali waliyoshinda 4-3 na kutwaa medali ya dhahabu.

Inter Milan iliridhia kutoa kitita cha dola mil 4.7 ili kumsajili Kanu ambaye kabla ya uhamisho huo, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka barani Afrika, lakini baada ya kubainika kuwa na tatizo hilo usajili wake ulisitishwa kwa muda na klabu ya Inter kukubali kugharamia matibabu yake.

Mchezaji huyo alifanyiwa upasuaji wa moyo uliofanikiwa sana na aliweza kurejea dimbani na kusajiliwa na Inter ambayo aliweza kuichezea kwa miaka minne tangu 1996 –1999 na baadaye akauzwa Arsenal ya England aliyoitumikia kuanzia mwaka 1999 hadi 2004 akiichezea jumla ya mechi 119 na kufunga mabao 30.

Mfano huo unatuthibitishia ulazima wa kuwapima wachezaji na kwamba, kwa mfano huo huo tuliona jinsi ambavyo Yanga waliweza kumsajili mchezaji mwenye matatizo ya majeruhi Patrick Kataray Mujalay mmoja wa wachezaji wenye vipaji kuwahi kutokea katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kataray, nyota kutoka DR Congo, alikuwa kila akiingia dimbani, anawakuna vilivyo wanachama na mashabiki wa Yanga kutokana na uwezo wake wa kuumiliki na kuufanyia mpira apendavyo, lakini majeruhi hayakumruhusu kwani alikuwa akiumia mara kwa mara.

Kama hiyo haitoshi, Yanga wakamsajili kwa mbwembwe kiungo mshambuliaji James Chilapondwa kutoka Malawi, lakini kutokana na na kutozingatia utamaduni wa kuwapima wachezaji wake, majeruhi yalimfanya nyota huyo kuachwa huku akiwa hajatoa msaada.

Kama hiyo haitoshi, Yanga ilifanya tena usajili kama huu wa Simba kwa Mbiyavangu, ilipomsajili mshambuliaji mwenye mwili mkubwa kama mcheza mieleka Robert Jama Mba kutoka Cameroon, ambaye alisifiwa sana alipotua Jangwani, lakini akishindwa kuisaidia timu.

Mchezaji huyo alikuwa mzigo dimbani hana anachokifanya zaidi ya kukimbia kimbia jambo lililowafanya Simba kuanza kuwatania katika kila mechi wanazoshuka dimbani na matokeo yake Yanga waliamua kukatisha mkataba na kumrudisha kwao.

Madhara hayo ya kuwasajili wachezaji wa kigeni bila kuwajaribu na kuwapima, yataendelea kuzigharimu Simba na Yanga kwa miaka nenda rudi kama hawatabadilika, pia yataendela kuwapoteza fedha nyingi na hatimaye kubaki wakawalaumu makocha wao kwa kutoipa mafanikio.

Kwa hakika, utamaduni huu ungetekelezwa Simba wasingemkosa kirahisi mlinzi Mbuyu Twite ambaye inaonekana sasa wanakaribia kumkosa kwa kusajiliwa na watani zao Yanga, ambao nao wamerejea kosa lile lile la kumsajili bila ya kumjaribu wala kumpima.

Kasumba hii ya kuwapenda zaidi nyota na makocha wa kigeni, ndio uliowafanya Yanga wakampachika sifa zisizo zake Dunsan Kondic, ambaye walimpa jina la ‘Professor’, lakini mwisho wa siku wakabaini kuwa alikuwa kocha wa kawaida kabisa na asiye na mafanikio makubwa huko atokako.

Nadhani, viongozi wa klabu mbili hizi na nyingine nyinginezo nchini, watakuwa wamejifunza vya kutosha kutokana na makosa waliyofanya kwani kusajili wageni kumekuwa kukizuia vipaji vya nyota chipukizi wazawa kuonekana, hivyo kuiathiri hata timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.

Kuvurunda kwa Mbiyavangu na mabao yaliyofungwa na chipukizi Said Bahanunzi katika michuano ya Kagame, ni somo kwa viongozi wa klabu zetu waone haja ya kutoa nafasi kwa vipaji vya vijana wa vikosi vya pili kama wale wa kikosi cha Simba kilichotwaa ubingwa wa michuano ya BancABC Sup8r kwa kuifunga Mtibwa Sugar 4-3.



juu