HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
ijumaa, 14 septemba 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Hongereni SAA kufikiria kujenga kituo cha sanaa

Shabani Matutu

 

MADA ya leo ningependa kutoa hongera kwa Chama cha ‘Sherehe Arts Association’ (SAA), kwa malengo yao ya kufikiria kujenga kituo cha sanaa (SAA Centre) ikiwa ni njia ya kuboresha sanaa na ustawi wa maisha kiuchumi.

Wanachama hao wameiweka mipango yao hadharani wakati mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Katiba, MC Richard Kwayu alipokuwa akisoma risala mbele ya mgeni rasmi katika semina elekezi ya siku moja iliyoandaliwa na SAA, kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Budget, Kunduchi, Dar es Salaam.

Semina hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali zinazolikabili soko la biashara, kukuza ubunifu wa sanaa kwa wateja, masoko na elimu ya mitandao ya kijamii.

Katika risala hiyo iliyokuwa ikigusa hisia za wasikilizaji ilieleza namna kituo hicho kitakavyokuwa muhimu kwa kuwa wanatarajia kitawasaidia kuwa na ofisi za uhakika na kuendesha biashara mbalimbali pamoja na Chama chao cha Kuweka na Kukopa(SACCOS) kilichosajiliwa.

SAA wanasema ili kukamilisha mipango yao hiyo wametoa wito kwa wahisani kujitokeza kusaidia kwa kuwatoa hapo walipo na kuwawezesha kukamilisha ndoto zao.

Kikiwa kimeanzishwa mwaka 2001 kimeweza kuonesha mafanikio na kuwa na malengo mazuri na yenye faida kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

Wanafikiria kuongeza matawi zaidi ili kiweze kuwa cha kitaifa, kuongeza vyanzo vya mapato, kubuni njia mpya za sanaa na masoko na kutekeleza malengo yake yote yaliyoainishwa katika katiba.

Moja ya mafanikio ni kuwezesha kupata SACCOS iliyo na usajili wa kudumu, kuwa na matawi kwa baadhi ya mikoa.

Katika hotuba ya Mama Bilali anawashukuru SAA inayoundwa kwa kuwajumuisha wasanii mbalimbali wakiwamo washereheshaji ‘MC’, Wapigisha muziki ‘DJ’, wapishi, wapambaji, waoka keki, wapuliza tarumbeta, wapiga picha mnato na kutembea kwa kufikiria kufungua chuo cha sanaa ikiwa ni pamoja na matawi kwa nchi nzima.

Anasema dhamira hiyo ni njema na inahitaji kutekelezwa vema kwani itachangia kubuni ajira na kuongeza mapato kwa wananchi hivyo kuwezesha kuondokana na umaskini.

Pia amewapatia rai ya kupenda kujiendeleza kielimu kwa sababu fani zinabadilika na kukua siku hadi siku.

Chama cha SAA kinaundwa chini ya uenyekiti wa MC Goydon Lukuwi, Makamu wake ni MC, Steven Mwakajumba, Katibu Mkuu ni MC Brycen Makena, Katibu Msaidizi ni Tumaini Mwandembwa, Mhazini ni MC Arcado Nchinga na Naibu Mhazini ni MC Brigita.



juu