SERIKALI bado imeendelea kupata kigugumizi cha kuwarejesha vyura wa Kihansi ambao hawapatikani popote duniani waliopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisisitiza kuwa vyura hao watarejeshwa bila kutaja ni lini.
Awali, vyura hao ambao kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Anne Maembe, walipaswa warejeshwe mwezi huu, lakini jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Membe alishindwa kutaja siku ambayo vyura hao watarejeshwa na kwamba bado kuna hatua zinafanyika.
Aidha, kumekuwepo na utata wa nchi ambayo vyura hao walipelekwa. Wakati habari zilizopita zikidai kuwa vyura hao ambao huigharimu serikali karibu sh milioni 100 kama gharama ya kuwatunza, walipelekwa nchini Marekani, jana Membe alisema walipelekwa Ujerumani.
“Kihansi kuna maporomoko makubwa ambayo husababisha mvuke, mvuke ule ndiyo husaidia kustawisha mayai yao. Vyura wale wako Ujerumani ambako waliwaomba baada ya kuwaondoa ili kuboresha mazingira yao, lakini kule Ujerumani wameshindwa kuzaliana kutokana na mazingira,” alisema Maembe.
Vyura 500 walipelekwa nchini Marekani takribani miaka tisa iliyopita na kwamba watakaporejeshwa watafikia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo kila awamu watakuja vyura 200.
Maembe alisema kuwa vyura hao watafikia UDSM na wataishi kwa muda katika hifadhi maalamu waliyojengewa kabla ya kupelekwa katika kituo kingine kilichojengwa Kihansi na baadaye ndipo watapelekwa katika bonde la Mto Kihansi walipokuwa wakiishi awali.
Kwa mujibu wa Maembe, vyura hao wamezaliana na kufika 3,000 na kwa sasa, Kihansi hakuna hata chura mmoja wa aina hiyo aliyebaki.
Katika hilo, serikali imekuwa ikitumia zaidi ya sh milioni 100 kama sehemu ya gharama ya kuwatunza vyura wa mradi wa Kihansi.
Wadau wengine wanaochangia mradi huo ambao kwa sasa ni sehemu ya urithi wa dunia, ni Serikali ya Marekani ambayo pamoja na kuchangia fedha taslimu ambazo hazijawahi kuwekwa bayana hapa kwetu, hutoa pia wataalam na vifaa mbalimbali vinavyohitajika kuwatunzia viumbe hao hadimu duniani.
Mratibu wa Mradi wa Kuhifadhi Bonde la Kihansi (LKEMP) ambao uko chini ya Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Dk. Fadhila Khatib, aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema kuwa Tanzania inalazimika kuchangia kiasi cha dola za Kimarekani 75,000 kwa mwaka (takribani sh milioni 97) kwa kuwa imeridhia makubaliano ya Jumuiya ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WSCS).
Kwa mujibu wa mratibu huyo, taifa linawajibika kulinda usalama wa vyura hao kutokana na mkataba wa kimataifa wa kutunza viumbe wa mwaka 1992, ambao Tanzania ilitia saini kuutekeleza.