HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 23 septemba 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Vita Kuu Uchaguzi Mkuu 2010: Mwandosya mtegoni

•  Vijana wajiandaa kumng'oa jimboni Rungwe

na Mwandishi Wetu, Mbeya

 

MAJALIWA ya kisiasa ya wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, sasa yamo shakani, baada ya kuanza kwa mikakati ya wazi ya kuwang’oa.

Wabunge hao, Dk. Harrison Mwakyembe wa Kyela na Prof. Mark Mwandosya wa Rungwe Mashariki, tayari wamekwisha kutangaziwa hali ya hatari na Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM), ambayo imeanza mikakati ya wazi ya kunadi wagombea wanaotarajiwa kuchuana nao katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Taarifa kutoka ndani ya umoja huo ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, zinaeleza kuwa UVCCM mkoani hapa imetangaza kukataa kuitwa ‘vijana ni taifa la kesho’ na imedhamiria kuweka wagombea wake katika majimbo yote ya uchaguzi ambayo hata hivyo yanashikiliwa na wabunge wa CCM kwa sasa.

Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka CCM mkoani Mbeya, vimeeleza kuwa, mkakati wa kuwaangusha wabunge hao unasimamiwa na kutekelezwa na UVCCM na unalenga zaidi kuhakikisha Prof. Mwandosya na Dk. Mwakyembe wanapoteza nafasi zao za ubunge mwakani.

Uchunguzi wa muda mrefu wa mwenendo wa kisiasa mkoani hapa uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, tayari mpinzani wa Prof. Mwandosya ameanza kupigiwa chapuo la wazi na kundi la wana-UVCCM ambao kwa siku kadhaa sasa wamekuwa katika shamrashamra za kusherehekea ushindi wa kamanda mpya wa umoja wao, Stephen Mwakajumilo, anayetajwa kuwa ndiye anayeandaliwa kuchukua nafasi ya Mwandosya mwakani.

Gazeti hili limewashuhudia baadhi ya wanachama wa UVCCM wakifanya vikao vya siri katika kumbi mbalimbali za sterehe mkoani hapa, ambavyo vimekuwa vikitawaliwa na ajenda ya mkakati wa kukabiliana na vigogo hao.

Katika kikao cha hivi karibuni ambacho kilidaiwa kuandaliwa kwa ajili ya kumpongeza kamanda mpya wa UVCCM, Mwakajumilo, ilielezwa na baadhi wa washiriki kuteuliwa kwa kamanda huyo mpya ni ishara kwamba anaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana mkoani humo, ambao wanaamini kuwa hawezi kulinganishwa na Prof. Mwandosya kiushawishi ndani ya chama.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa vijana hao katika mazingira ya wazi yanayoonyesha kuwa hawamuungi mkono Prof. Mwandosya, wameweka wazi nia yao ya kuwa na kamanda mpya wa mkoa, ambaye watamuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani, kwa sababu ni mfadhili wao kiuchumi.

Katika kikao kingine kilichoshuhudiwa na mwandishi wa gazeti hili, kilichofanyika kwenye baa iliyoko eneo la Soko Matola, viongozi kadhaa wa UVCCM walionekana kumzunguka Mwakajumilo, ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa, Reginald Msomba, kama ishara ya kuwalinda viongozi wao hao.

Mwakajumilo ambaye ni mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mbeya, anadaiwa kuwa na ushawishi wa kutosha ndani ya UVCCM kutokana na ukwasi alionao.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa za mkoani hapa wameeleza kuwa, anaweza kutoa ushindani mkubwa kwa Prof. Mwandosya, ambaye katika chaguzi zilizofanyika miongo miwili iliyopita hakupata upinzani ndani ya chama chake, hata kutoka vyama vya upinzani.

Mbali ya Prof. Mwandosya, mbunge mwingine anayeonekana kuwindwa na wana-UVCCM mkoani Mbeya ni Dk. Mwakyembe, ambaye amekuwa akidaiwa kuwa na mkwaruzano wa muda mrefu na Mkuu wa Mkoa huo, John Mwakipesile.

Mvutano wa Dk. Mwakyembe na Mwakipesile unadaiwa kuwa turufu muhimu kwa UVCCM ya kuhakikisha hapati nafasi ya kuwa mgombea wa chama hicho mwakani, kwa maelezo kuwa ni mmoja wa watu wanaokidhoofisha chama kwa kuendeleza vita ya chini kwa chini baina yao.

Aidha, vita ya ufisadi ambayo Dk. Mwakyembe ni mmoja wa makamanda wake, nayo inadaiwa kuwa moja ya mambo yatakayohatarisha wadhifa wake huo iwapo majeruhi wa vita hiyo ndani ya chama chake wataamua kuunganisha nguvu zao kupambana naye.

Uchunguzi zaidi wa gazeti hili, umebaini kuwa wanachama wengi wa UVCCM wanatarajiwa kujitokeza katika kupambana na wabunge wa sasa kwenye uchaguzi wa mwakani lakini kati yao, ni wawili tu wanaotajwa kuishi mkoani humo, huku wengine wote wakitajwa kuishi nje ya mkoa huo.

Inaelezwa zaidi kuwa, Michael Mponzi, ni mmoja wa vijana ambao ni wakazi wa Mbeya, anayetajwa kuwa atajitosa kuwania ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mchungaji Luckson Mwanjale.

Mponzi ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini katika idara ya utoza ushuru wa maliasili.

Vijana wengine wanaotarajiwa kujitokeza katika majimbo mengine (majina yanahifadhiwa) tayari wameanza kupigiwa chapuo juu ya mchakato wa nafasi hiyo, lakini wameshindwa kuthibitisha maamuzi yao, kwa madai kuwa ni mapema mno.

Tanzania Daima Jumatano ilipowasiliana na Katibu wa UVCCM Mkoa , Rodha George, ili aweze kuthibitisha taarifa hizi, alieleza kuwa, vijana ni taifa la leo, hivyo kitendo cha kujitokeza kuwania nafasi za maamuzi ni haki yao ya msingi.

“Ni kweli vijana wengi wamejitokeza na kuonyesha nia ya kuwania nafasi za ubunge katika majimbo yote yaliyopo mkoani hapa, baada ya kujitathmini na kujua kuwa wanatosha katika nafasi hizo na wakati ukifika wanatarajia kujitangaza,’’ alisema katibu huyo.

Roda alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wanawake ambao ni wanachama wa jumuiya hiyo ya UVCCM kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za maamuzi, ikiwamo kuomba nafasi za upendeleo za kuteuliwa katika viti maalumu vya ubunge.

“Nawaomba wanawake wenzangu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za maamuzi, ikiwamo nafasi ya ubunge wa kuteuliwa, hasa kwa kipindi cha mwakani, maana chama kimeongeza nafasi zaidi ya kumi kutoka nafasi mbili za ubunge wa kuteuliwa kwa vijana wa kike, kutoka katika jumuiya yetu,’’ alieleza katibu huyo.

Mkoa wa Mbeya unaongozwa na wabunge wa CCM katika majimbo yote 11 ya uchaguzi.

Wabunge hao ni Mbunge Benson Mpesya (Mbeya Mjini), Mchungaji Luckson Mwanjale (Mbeya Vijijini), Prof. David Mwakyusa (Rungwe Magharibi), Prof. Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki) na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela).

Wengine ni Dk. Lucas Siame (Mbozi Magharibi), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Dk. Guido Sigonda (Chunya), Victor Mwambalaswa (Lupa – Chunya), Gideon Cheyo (Ileje) na Estherina Kilasi (Mbarali).



juu