MKE wa Waziri Mkuu, Mama Regina Lowassa, amesema Tanzania ina haja ya kujifunza kutoka Vietnam, hasa katika suala la kutunza kumbukumbu za matukio ya kitaifa yanayohusu kina mama.
Alisema Tanzania tunaweza kuhifadhi historia na kuonyesha jinsi ambavyo wanawake wa Tanzania wameshiriki katika mambo mbalimbali ya kitaifa yakiwamo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akizungumza jijini Ho Chi Minh baada ya kuzuru nyumba ya makumbusho ya sanaa ya uchoraji (Fine Arts Museum) inayoendeshwa na wawawake, Mama Lowassa alisema inabidi tutambue vipaji walivyonavyo wanawake wa Kitanzania na tuvienzi, ili kutunza historia ya nchi.
“Kuna mambo mengi ambayo wanawake wameyafanya katika siasa au hata michezo lakini hayajawekwa vizuri kihistoria, … watu kama Bibi Titi, Nzaeli Kyomo wamefanya makubwa Tanzania … inabidi mambo haya yahifadhiwe, ili watoto wetu waweze kupata mahali pa kujifunza…,” alisema.
Alisema kuna kina mama wengi wenye vipaji, lakini kwa vile hakuna anayewatambua, mambo mazuri wanayoyafanya yanapotea kwa vile hayawekewi kumbukumbu yoyote.
Akiwa Hanoi, Mama Lowassa alitembelea kijiji cha hariri cha Van Phuc (silk village) na kuona jinsi wanawake wanavyotengeneza hariri kwa kutumia viwanda vidogo vidogo ambavyo viko uani mwa nyumba zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake cha Vietnam, Bibi Ha Thi Kheit alimweleza Mama Lowassa kuwa asilimia kubwa ya viwanda hivyo vya hariri vinamilikiwa na wanawake na kwamba wapo ambao wameweza kutoa ajira kwa wengine kupitia miradi hiyo.
Alisema kazi hiyo ya kutengeneza hariri imekuwapo kwa zaidi ya miaka 1,000 kwa kutumia mashine ndogondogo ambazo zimekuwa zikiboreshwa mwaka hadi mwaka. Pia wanawake hao wanamilki viduka mbele ya nyumba zao ili kuhakikisha wateja wanapata mali wanazozalisha papo hapo.