logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 10 septemba 2006
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1
Turuhusu udini ututenganishe?
Jeff Msangi


MTANZANIA mwenzangu,

Leo nina mada ngumu kidogo. Mara nyingi nimejiepusha na mijadala ya namna hii. Lakini hilo halina maana kwamba sisikii wala sielewi nini kinaendelea juu ya mada yangu ya leo. Udini.

Mojawapo ya mambo ambayo sisi kama Watanzania, hususan tunapokuwa nje ya nchi, hatuishi kujivunia ni suala la kutobaguana kwa kutumia dini wala kabila. Ilifikia mahali ikawa kama ni kosa la jinai kumuuliza mwenzako ni kabila gani au dini gani. Udini na ukabila si misingi ya taifa letu. Utanzania tuliuweka mbele zaidi.

Misingi hiyo iliwekwa na waasisi wa taifa letu, wote kwa pamoja, mababu na mabibi zetu. Sifa nyingi zaidi zimwendee hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa sababu tupende au tusipende, alikuwa kiongozi wa nchi yetu, kiongozi wa kweli.

Mataifa ya nje yaliyowahi kutuheshimu, yamefanya hivyo kwa kuzingatia umoja wetu, hata kama umekuwa wa kinadharia zaidi kwenye nafsi zetu. Tumeonekana wamoja hata kama baadhi yetu, katika makundi mbalimbali tumeshindana kitabia.

Kama Mtanzania hapa Canada najawa na furaha sana ninapokutana na Mtanzania mwenzangu. Kwa bahati nzuri Kiswahili kimechangia sana katika kudumisha au kupalilia umoja wetu.

Hatukuchekeana kwa minajili ya dini wala kabila. Hili lisimaanishe kwamba mambo hayo hayajapewa kipaumbele na baadhi ya watu, ila cha msingi na muhimu sana ni kwamba hatukuwa tunayapa nafasi ya kutuelekeza jinsi gani tuhusiane na binadamu wenzetu, Watanzania wenzetu.

Hali ya kutokuwa na udini au ukabila imedumu kwa muda mrefu japokuwa vuguvugu za udini na hata ukabila zimekuwa zikichomoza na kupotea. Hii ni hali halisi ya ubinadamu popote pale. Hatufanani na si wote tunaopendana na kuheshimiana bila kujali imani na dini. Mambo nasikia yanabadilika, hofu inaanza kuingia na ndiyo maana siwezi tena kukaa kimya.

Raisi wetu na makamu wake wa raisi hivi sasa ni Waislamu. Kama ni Waislamu kwa majina au imani, ni Mungu peke yake anayeweza kujua hilo. Tanzania si nchi ya Kiislamu na wala falsafa yake haifungamani na dini yoyote.

Wakati mwingine huwa nahoji hata ule utaratibu wa kuapisha viongozi wetu kwa kutumia Kurani au Biblia wakati serikali yenyewe haina dini yoyote.

Unaapa kuilinda katiba ambayo inatamka wazi kwamba haina dini wala kabila! Haina shaka, hiyo ni baadhi ya minyororo ya ukoloni na utumwa ambao baadhi yetu hawachoki kuukumbatia. Hii ni pamoja na viongozi wetu ambao masuala kama hayo wangeweza kuyabadili baada ya uhuru au hata sasa.

Katika siku za karibuni mijadala ya kuhoji vigezo anavyotumia Rais Kikwete katika kuteua viongozi imeshika kasi. Yanayosemwa ni mengi, ndiyo maana nadhani wakati umefika tukumbushane sisi ni kina nani.

Dini na ukabila ni silaha ambazo zimetumika katika nchi duniani kuondoa mshikamano na umoja. Utengano, vita, mifarakano mingi imetokea kwa sababu ya udini.

Je, sisi kama Watanzania tumefikia mahali tumeanza kuwaonea wivu wenzetu wanaochinjana na kupigana vita isiyoisha kwa sababu ya imani za kidini bila kuwa na ushahidi kwamba dini hii au ile itawapeleka peponi?

Hisia niliyonayo ni kwamba kuna watu wanatumika kueneza sumu ya udini. Kuna mamluki ndani yake. Ni kina nani? Wanataka nini? Maswali haya ni magumu ila majibu mepesi niliyonayo ni kwamba, watu hao wanataka Tanzania iwe kama nchi zilizo na migogoro isiyoisha.

Hivi tumesahau kwamba dini zote tunazoziruhusu ziongoze fikra zetu zililetwa na wakoloni ambao walizitumia vizuri kututawala? Hatukumbuki kwamba dini zenyewe zina upungufu mwingi tu na kwamba wazee wetu wa zamani (waliokuwa na dini zao za asili) walipojaribu kuhoji walipewa majibu kwamba “ni dhambi kuhoji.”

Leo hii ukinikataa mimi kwa sababu za udini au ukabila, huoni kama unakuwa umejifunga kwenye minyororo ya utumwa wa akili?

Inawezekana Rais Kikwete ameteua viongozi wengi Waislamu. Sina takwimu rasmi. Lakini je, dini ya mtu ina uhusiano gani na utendaji wake? Kama fulani amechaguliwa kwa dini yake na si uwezo wake wa kiutendaji kwanini tusiseme, tusifungue kesi kutaka aondolewe pindi tunapoona kwamba kazi hawezi?

Tujiulize, lipi muhimu kwetu hivi sasa, dini au uchapaji kazi ili taifa letu lisonge mbele? Je, anayeeneza hii sumu ya udini, ni nani kama si adui yetu namba moja?

Mifano ya madhara ya mifarakano ya kidini ipo lukuki. Tuanze sasa kujifunza kutokana na makosa. Tusipofanya hivyo tunatafuta balaa na tutakuwa wajinga kuanza kutoana macho kwa sababu za dini.

Tunayo kazi ya kujenga nchi yetu. Hizi dini za mapokeo tumeshazikubali, kuziruhusu ziturudishe nyuma kama zilivyorahisisha kutawaliwa kwetu na wakoloni, hasa wakati huu tunapojua mahali tulipokosea, ni kosa ambalo hatuwezi kuwa na visingizio kwamba hatukujua, hatukuona likija. Jumapili njema.

jeffmsangi@sympatico.ca
www.harakati.blogspot.com

h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2006 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa mkwepu na makunganya, slp 15261, dar es salaam, tanzania
simu +255-22-2120604  •  faksi +255-22-2126234